Hii ndio tofauti ya Tenga, Karia dhidi ya Kariakoo

Tuesday March 17 2020

Hii ndio tofauti ya Tenga, Karia dhidi ya Kariakoo,LEODEGAR Chilla Tenga ,Rais wa TFF ,

 

LEODEGAR Chilla Tenga anafahamika zaidi kwa uongozi wake madhubuti kama Rais wa TFF kuanzia 2005 hadi 2013.

Lakini ni wachache wanaojua au kukumbuka kwamba kabla ya majukumu haya, Tenga alishawahi kuwa na nafasi kubwa ndani ya mtangulizi wa TFF, yaani FAT, ambapo alishika nafasi ya Katibu Mkuu.

Tenga alishika nafasi hiyo chini ya kamati ya muda, baada ya kuondolewa kwa Mwenyekiti Mohamed Mussa, aliyerithi mikoba ya Said El Maamry, 1987.

Miaka hiyo Simba ilikuwa DHAIFU sana kiasi cha kunusurika kushuka daraja siku ya mwisho ya msimu, kwa misimu mitatu mfululizo, 1987, 1988 na 1989.

Msimu wa 1990 Simba walijipanga kuhakikisha hiyo inabaki historia. Wakaimarisha kikosi ikiwamo kumrudisha nyumbani nyota Zamayoni Mogella ‘Golden Boy’, aliyetimka kuanzia 1986 akienda Volcano United ya Kenya na kukipiga pia Oman.

Simba waliuanza msimu wa 1990 dhidi ya CDA ya Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri. Zamoyoni Mogella alimpiga kiwiko mchezaji mmoja wa CDA na kuonyeshwa kadi nyekundu.

Advertisement

Wakati huo ilikuwa imetungwa sheria ya adhabu ya kufungiwa miezi 6 kwa kosa kama hilo. Basi Tenga hakusita, akamfungia Mogella miezi sita.

Simba walihangaika kuhakikisha wanamuokoa nyota wao, lakini ilishindikana. Tenga alisisitiza kwamba adhabu kwa nyota wakubwa kama Mogella, kutoka klabu kubwa kama Simba, ni somo tosha kwa nyota wengine wa klabu vingine.

Simba wakasema Tenga anawakomoa makusudi kwa sababu yeye ni Yanga. Mungu si Athumani, Said Mwamba ‘Kizota’ wa Yanga naye akampiga mtu kiwiko mtu, adhabu ikawa ile ile, bila kusita.

Kelele za Simba kwamba Tenga anawaonea kisa yeye Yanga, zikafa kifo cha asili.

Hata mwaka 2008, Tenga akiwa Rais wa TFF, wakati Yanga wamegoma kucheza mshindi wa tatu wa Kombe la Kagame, alitangaza kuwafungia miaka 3 kushiriki mashindano ya kimataifa.

Kwenye mkutano wa Kamati ya Utendaji, wazo la Tenga kuwafungia Yanga lilipata upinzani mkubwa sana. Akasimama na kuwauliza, “Hivi nyinyi wajumbe, mnadhani kuna Yanga kuliko mimi humu? Mimi nimecheza Yanga na nimekuwa nahodha wa Yanga, ila lazima waadhibiwe.”

Huko ndiko kutengemaa kwa Tenga, tofauti na ilivyo kwa Wallace Karia, Rais wa sasa wa TFF. Huwa hana makali linapokuja suala la Kariakoo.

Januari 4, Pascal Wawa wa Simba, alimkanyaga vibaya Ditram Chimbi wa Yanga, hakuchukuliwa hatua. Februari 15, Bernard Morrison wa Yanga alimpiga kiwiko Jeremia Juma wa Tanzania Prisons, hakuchukuliwa hatua za kisheria. Pia Februari 22, Jonas Mkude wa Simba, alimpiga kiwiko Ally Kombo wa Biashara United Mara...hakuchukuliwa hatua zozote.

Machi 8, Clatous Chama wa Simba alimkanyaga Feisal Salum wa Yanga...hajachukuliwa hatua za kisheria, lakini Zawadi Mauya wa Kagera Sugar alichukuliwa hatua mara moja, alipomfanyia utemi Ibrahim Ajibu wa Simba. Huo ndiyo udhaifu wa Karia dhidi ya Kariakoo.

Linapokuja suala la Kariakoo, Karia anakuwa mpole na mnyonge sana.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aliwahi kunukuliwa akidai Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi akapimwe akili...! Hii ni kauli nzito sana kutolewa na Ofisa Habari wa Klabu, dhidi ya mtu mwenye mamlaka makubwa kama Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi...lakini hakuchukuliwa hatua zozote.

Lakini nahodha wa Azam FC, Aggrey Moris, aliposema ligi inachezeshwa kama soko la samaki, akachukuliwa hatua moja kwa moja.

Kwenye dirisha dogo, Yanga iliwasajili wachezaji kadhaa, akiwamo Haruna Niyonzima. Nyota huyo Mnyarwanda, alivaa jezi namba 18 katika mechi yake ya kwanza, dhidi Simba na nyingine zilizofuata, kisha ghafla sasa anavaa namba 8, ambayo hapo awali ilikuwa inavaliwa na Mohamed ‘Mo Banka’, lakini husikii chochote.

Achana na hiyo, David Molinga alianza kwa kuvaa namba 22, lakini sasa anavaa namba 49. Yaani huku msimu unaendelea, watu wanabadili tu namba wanavyojisikia. Hii ni kinyume na kanuni za ligi ambazo zinaagiza mchezaji mmoja, namba moja ya jezi kwa msimu

Advertisement