JAMVI LA KISPOTI : Hebu tuitafakari Yanga hii bila mkono mrefu wa GSM

Thursday February 27 2020

 Hebu tuitafakari Yanga hii bila mkono mrefu wa GSM,Ligi Kuu Bara,Yanga SC,Kocha Charles  Mkwasa,

 

By Khatimu Naheka

PALE Yanga mambo hayapo sawa kwani mashabiki wa timu hiyo hawana furaha na matokeo ya timu yao na jinsi inavyoendelea katika Ligi Kuu Bara. Yanga ipo nafasi ya nne ikikomaa na pointi 41 wakati wakiwa na sare ya nne mfululizo.

Kinachowaumiza zaidi mashabiki na wanachama wa timu hiyo ni kuona matokeo hayo kama yanawasukuma watani wao, Simba ambao wako juu ya msimamo wakiendelea kuhesabu hatua za kuchukua taji la tatu mfululizo.

Katika nyakati hizi wadau wa klabu hiyo walitarajia kuona kikosi chao kikitoa upinzani mkubwa kwa Simba katika kuchukua taji, hasa kutokana na kuvuma katika usajili wao mara mbili msimu huu kuanzia dirisha kubwa na hata dogo.

Baada ya Yanga kuanza ligi msimu huu na kucheza mechi chache, hali ilionekana wazi kwamba hawana kikosi ambacho kingekuwa na nguvu ya kufikisha malengo ambayo yalitarajiwa. Timu yao iliyumba sana kiasi hata makocha kutimuliwa kisha ajira kutua kwa Charles Mkwasa kwa muda.

Kabla ya hatua hiyo hali ilionekana wazi kwamba hali ya kuamini uongozi wa klabu hiyo inazidi kupungua kabla ya mkombozi, GSM, kuingilia kati kuinusuru klabu hiyo.

GSM baada ya kuingilia kati na kuamua kuisadia Yanga mambo yalionekana kutulia kiasi kabla ya sasa ukweli halisi kujiweka wazi.

Advertisement

Nasema ukweli kujiweka wazi kwa sababu licha ya nguvu ya GSM bado pia makosa baadhi yakajitokeza katika hatua za kuitengeneza timu hiyo.

Makosa makubwa ambayo yataendelea kuiandama Yanga ni watu kuwa na tamaa au kutokuwa makini katika kufuatilia ubora wa wachezaji wao.

Makosa haya inawezekana wapo viongozi wa klabu hiyo hawatakwepa lawama kwa kuiingiza mkenge GSM katika kuwapa majina ya wachezaji ambao hawakuwa na tija kubwa katika timu hiyo.

Kwa sasa Yanga inaonyesha wazi kwamba wapo wachezaji ambao hawakustahili hata kupewa miezi sita katika usajili wao walifanyiwa upatu katika kusajiliwa kwenye timu hiyo.

Matokeo yake sasa makosa hayo yanaighalimu timu hiyo kwa kiasi kikubwa katika mbio za kimashindano wakiumia zaidi mashabiki wa timu hiyo ambao walitarajia makubwa.

Ukiacha hilo, hata hao GSM nao wanaweza kuja kuchoka kuendelea kuwaamini viongozi na hata kufikiria kuondoka endapo makosa ya namna hiyo yataendelea.

Ukiangalia sasa katika kikosi cha Yanga huoni harakaharaka kwamba kuna washambuliaji ambao wanaweza kuitengenezea matokeo, kwani kiasi kikubwa cha washambuliaji wa timu hiyo wanalingana ubora - tena ukiwa wa kawaida zaidi.

Swali ambalo wengi tunajiuliza hawa kawaleta nani na alizingatia nini katika kuwaleta kwake? Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia suala la namna hi linamtia hasira zaidi anapoiona timu yake inateseka kwani kunaonyesha wazi hakuna ufuatiliaji mzuri wa ubora wa mchezaji kabla ya kupewa fomu ya kusaini mkataba na klabu hiyo.

Hili ni fundisho kubwa ambalo Yanga imelipitia na kwa kiasi kikubwa wanapaswa kuwashukuru GSM ambao bila hatua yao ya kuja na mpango wa kuwaleta kina Bernard Morrison na hata kumbakiza Lamine Moro pamoja na David Molinga pengine mambo yangekuwa mabaya zaidi wakati huu.

Pengine kama viongozi wa klabu hiyo wanajifanyia tathimini, basi itoshe kujiridhisha kwamba nguvu yao haikuwa kubwa kama ambavyo wengi waliamini wakati wanaingia madarakani.

Kuna mambo mengi yanaonyesha hawakuwa na ubora mkubwa kuweza kuingoza klabu kama Yanga kimafanikio badala yake ni kama walikuwa wanajaribu kuongoza taasisi ambayo hawakuwa wanajua kipi kinahitajika.

Si vibaya hatua kama hiyo pia ikawa kama fundisho kwa wanachama kuacha kufanya uamuzi kwa papara katika kuwapa dhamana viongozi ambao wanataka kuingia madarakani kuongoza klabu yao.

Naona kabisa kama si GSM, basi kulikuwa na hatua kubwa ya uongozi wa Yanga kuwa katika hatua mbaya zaidi kwa wanachama wao mpaka sasa endapo kila kitu kingeendelea

Ni vyema kufanywa kwa usimamizi wao kwani sina shaka kabisa kuwa kuna baadhi ya viongozi waliingia kimakosa katika kuongoza klabu hiyo.

Na kwa kuzingatia hilo naamini kwamba Yanga bado ina nafasi kubwa ya kuendelea kujifanyia tathmini.

Advertisement