VIDEO: Zuchu afunguka

Sunday September 20 2020

 

By NASRA ABDALLAH

ASIKUAMBIE mtu, licha ya uchanga wake kwenye tasnia ya muziki, lakini kwa muda mfupi tangu atambulishwe mwimbaji chipukizi kutoka WCB, Zuchu amefunika kinoma.

Mwanadada huyo ambaye majina yake kamili ni Zuhura Othman, mtoto wa nyota wa muziki wa taarabu nchini, Khadija Omar Kopa amejizolea umaarufu mkubwa na kupata wafuasi wengi kwa muda mfupii, ikiwa ni miezi minne tu tangu atambulishwe katika lebo ya WCB.

Achana na ngoma zake tisa zilizopo kwenye EP yake iitwayo ‘Am Zuchu’ aliyoiachia Aprili mwaka huu, lakini Zuchu amekuwa midomoni mwa watu hasa ukaribu wake na Diamond na naona nyota yake ilivyong’ara ghafla na kuna baadhi hawamjui kwa undani mwimbaji huyo.

Hata hivyo, Mwanaspoti limepata wasaa wa kufanya mahojiano maalum naye nyumbani kwa bosi wake, Diamond Platnumz maeneo ya Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam na kufunguka mambo mengi kuhusu yeye na mipango yake kimuziki. Ebu endelea naye upate uhondo kamili.

HUBEBA NINI KATIKA POCHI

Kama mastaa wengine wa kike huwa hawaachi pochi katika mitoko yao, Zuchu alipoulizwa kitu gani hakikosekani kwenye pochi lake, mwanadada huyo anakiri ukiacha vitu vingine, hawezi kutoka nyumbani bila kubeba dawa ya kupunguza athari ya Ugonjwa wa Pumu iitwayo inhaler.

Advertisement

Zuchu anasema amezaliwa na Ugonjwa wa Pumu na umekuwa ukimtesa na kila anapoona dalili za ugonjwa huo kumzingua, hutumia dawa hiyo inayomsaidia kupunguza athari.

“Ni bora nikose kitu chochote kwenye pochi lakini sio hizo dawa, kwani athari za pumu kwa mwenye ugonjwa huo anajua, na hii dawa hunisaidia nionapo dalili ambazo sio nzuri ukiweka kifaa hicho mdomoni,” anasema.

Alipoulizwa kama ugonjwa huo umuathiri katika kazi zake za muziki zinazohusisha matumizi makubwa ya pumzki, Zuchu anasema anajishangaa na kuamini Mungu humtendea miujiza, kwani hajawahi kukumbubwa na tatizo hilo jukwaani.

“Huwezi kuamini niwapo stejini zijawahi kukumbwa na dalili za kuweza kuathiri ufanisi wangu, ni miujiza ya Mungu na ninamshukuru kwani hili tatizo halijawahi kunikumbwa jukwaani.”

NGUO OVERSIZED DAMDAM

Ukiachilia hilo la pochi yake, Mwanaspoti lilitaka kujua aina gani za nguo anazozipenda na kimwana huyo anasema anapenda kuvaa nguo zilizo kubwa kwake (oversized).

Akieleza sababu ya kupenda nguo hizo, Zuchu anasema; “Maisha yangu napenda kuwa huru, hivyo hata kwenye mavazi napenda kuvaa zitakazonipa uhuru na ndio maana navaa nguo kubwa,” anasema Zuchu anayetamba na nyimbo za Nisamehe, Wana, Raha, Kwaru, Hakuna Kulala, Mauzauza, Ashua na hivi karibuni ameachia nyingine mbili za Linawachoma na Cheche alizomshirikisha Diamond Platnumz.

TUKIO ASILOSAHAU

Zuchu anasema kati ya mambo ambayo hataweza kusahau maishani mwake ni siku bosi wake Diamond, alipokuwa akihojiwa katika moja ya kituo cha redio hapa nchini na alipoulizwa kuhusu suala la kama ana mpango wa kumsajili msanii wa kike.

Katika majibu yake hayo anasema alijibu kwa msisitizo kuwa hana mpango huo.

“Kumbuka wakati Diamond anajibu haya, nilikuwa bado nipo benchi nasotea kutoka, kikweli iliniumiza sana na kidogo nianze kukata tamaa, lakini nashukuru wasanii wenzangu hususani Mbosso walikuwa akinipa moyo wa kuendelea kuwa na subra,” anasema Zuchu.

ANAJIHISI ANA DENI

Anasema uwekezaji aliofanyiwa na WCB ni mkubwa ambapo unamuumiza kichwa kila siku namna gani ataweza kuendana nao.

Anasema msanii wa kike ni tofauti na wa kiume hata katika uandaaji wake wa video kwa kuwa anahitaji vitu vingi ikwemo kwenda saluni, makeup na mavazi.

Hii ni tofauti na msanii kama Mbosso, ambaye akishanyoa tu na akipata na nguo zake kama tano video imeisha, hivyo kiufupi uwekezaji na gharama za kumsimamia ni tofauti.

TUZO ZAMPAGAWISHA

Kuhusu uteuzi wake na kutajwa kuwania Tuzo za African Music Magazine (AFRIMMA), anasema alishtushwa alipoona kwa mara ya kwanza kuwa ni miongoni mwa wateule katika tuzo hizo.

“Yaani nilivyoona mara ya kwanza kwenye mitandao sikuamini nilijiuliza ‘like what’.

Nashukuru tayari Afrimma wamenipigia simu na tumefanya nao mahojiano kikubwa tuombeane wasanii wa Tanzania turudi na tuzo nyumbani kwa kuwa tukishinda, wameshinda watanzania.”

Wakati kuhusu suala la wasanii wote wa WCB kuingia katika tuzo hizo kasoro Lavalava na Queen Darleen, anasema bado hiyo kwa haiwavunji moyo kwa kuwa hata angeingia msanii mmoja wa WCB ni sawa na wameingia wote.

Katika tuzo hizo Zuchu ameingia vipengele viwili ambavyo ni msanii bora wa kike Afrika Mashariki na Msanii bora wa kike anayechipukia.

QUEEN DARLEEN KIROHO SAFI

Kumekuwa na maneno ya chini chini juu ya Zuchu kuonekana kama anapendelewa ndani ya WCB kiasi cha kumfunika hata dada wa Diamond, Queen Darleen, hata hivyo Zuchu alipoulizwa kama hali hiyo ilishawahi kumuudhi Queen.

Zuchu anasema haijawahi tokea na badala yake amekuwa ni mtu mwenye mapenzi makubwa na huwa anamchukulia kama mtoto wake.

‘Yaani dada Queen hata siku labda nina tukio la kufanya, yeye ndio atakuwa wa kwanza kunihangaikia kuanzia suala la saluni, kuvaa na mengine ilimradi kuhakikisha nipo sawa,” anasema.

YEYE NA DIAMOND VIPI?

Ukiaangalia ngoma mpya ya Zuchu ya Cheche aliyoimba na Diamond na namna wawili ambao wamekuwa na mitoko ya pamoja kama wapenzi mara kwa mara, Zuchu anafichua ukweli.

Anasema licha ya tuhuma hizo za kwamba anatoka kimapenzi na Diamond Platnumz, staa mwenye rekodi zake katika mahusiano na vimwana mbalimbali, ukweli ni kwamba uzushi uliopo hauna ukweli wowote na kueleza wanaheshimiana sana kama mtu na kaka yake au mtu na babaake.

“Jamani watu wameweka mabando yao, wanaandika vitu wanavyojua wao siwezi kuwazuia ila ukweli naujua mimi na mbaya zaidi hawajawahi kuwa hata na ushahidi wa picha kuthibitisha jambo hilo sasa nahangaika nao wa nini,” anasema.

MZUKA STEJINI

Zuchu anasema wakati wa kupanda stejini huwa kuna mzuka fulani unakuja kutokea tumboni ukichanganya na shangwe za watu basi ndio unavurugwa kabisa.

Akitolea mfano katika shoo ya uzinduzi wa nyimbo za CCM zilizofanyika mwezi uliopita Uwanja wa Uhuru, Zuchu anasema licha ya wasanii kukatazwa kushuka chini alikuwa anatamani kwenda kila saa kuwagusa mashabiki waliofurika viwanjani hapo kila wakati kutokana na mapenzi waliyoonyesha kwake.

“Kiukweli sio mashabiki wala uongozi wangu, wameniamini kupita kiasi hivyo nami naahidi sitawaangusha katika hili kikubwa tuombeane uzima,” anasema Zuchu.

Unajua mkwanja wake wa kwanza kwenye shoo alipewa na nani na alizifanyia nini? Basi usikosi kujua utamu wa haya yote kesho Jumatatu ndani ya Mwanaspoti.

 

 

Advertisement