Said Fella: Hiki ndo kilichompeleka Zuchu Wasafi

UKITAKA kuzungumzia muziki wa kizazi kipya, hakuna namna utaweza kuumaliza wote bila kutaja jina la Mkubwa Fella, yaani hiyo haiwezekani.

Mkubwa Fella ambaye jina lake halisi ni Saidi Fella ameutumikia muziki wa Bongofleva kwa takriban miaka 20 sasa kama mwimbaji na mwandishi, lakini uwanja uliompa umaarufu zaidi ni umeneja.

Wasanii kibao kama J uma Nature, Chege na Temba, Jux, Diamond Platnumz, Yamoto Band wote wamewahi kupitia kwenye mikono yake. Kwa sasa Fella ni mmoja wa viongozi wa msanii Diamond Platnumz pamoja na lebo ya WCB kwa ujumla, kwa maana hiyo, kwa uzoefu alionao Fella kwenye muziki, ni mtu muhimu wa kuangaliwa linapokuja suala la kutoa maoni kuhusu Bongo Fleva.

Gazeti hili lilifanya mahojiano na Fella na kumtandika maswali mawili matatu kuhusu yanayoendelea kwa sasa kwenye muziki, Fella huyu hapa anaturirika.

KURUDI KWA YAMOTO BAND

Moto uliokuwa ukiwashwa na bendi ya madogo wanne, Aslay, Mbosso, Beka Flavour na Enock Bella ulisababishwa na Fella, kwa sababu vichwa hivyo vilipatikana baada ya kuanzisha nyumba ya kulea na kusimamia watoto wenye vipaji vya kuimba ya Mkubwa na Wanawe mwaka 2011.

Lakini mwaka 2017, ikiwa ni miaka mitatu tangu bendi hiyo ianzishwe, jini-mkata-kamba aliingilia kati, bendi ikasambaratika na kila mmoja akachukua hamsini zake na kufanya muziki kama solo artist (msanii wa kujitegemea).

Hata hivyo, licha ya kwamba inasemekana wasanii hao walivunja bendi bila mikwaruzano, bado kuna tetesi zinadai baadhi yao hawako sawa — huku Mbosso na Aslay wakitajwa kuwa na tofauti zaidi. Na sio tu kutajwa kuwa na tofauti, bali vitu vingine kama vile Mbosso kutom-follow Aslay, na Aslay kutom-follow Mbosso kwenye mtandao wa Instagram vinatumika kama vielelezo vya tofauti zao za chini ya kapeti.

Mkubwa Fella alipoulizwa kuhusu uhusiano baina ya madogo hao alijibu kwamba anachokifahamu yeye ni kwamba Mbosso na Aslay na kila msanii aliyewahi kuwa Yamoto Band wana uhusiano mzuri hata baada ya bendi kuvunjika.

“Hayo ya kwamba wamegombana ni maneno ya mtandaoni, hayana ukweli wowote. Mimi ninachojua wako sawa. Na pia nataka watu wajue, Yamoto Band haijafa kwa sababu eti labda wasanii walipigana, hapana, Yamoto ilikufa kwa sababu wasanii walitaka kufanya vitu vikubwa zaidi, na wenyewe walidhani vitu vikubwa hivyo vitawezekana wakiwa wasanii wa kujitegemea,” ameeleza Fella.

Aidha, Fella ameongeza, pia kuna uwezekano mkubwa wa wasanii hao kufanya ngoma ya pamoja, na hilo litawezekana kwa sharti moja tu, kama wenyewe, kina Aslay watakubaliana kufanya hivyo.

“Watu hawajui, sio mimi niliyetengeneza Yamoto Band. Ni wasanii wenyewe waliamua. Wote walikuwa wanakaa kwenye nyumba ya Mkubwa na Wanawe, na kulikuwa na wasanii wengi tu. Lakini wenyewe wanne wakajikusanya na kuamua kuja na bendi, mimi nikabariki tu na tukawawezesha wakafika walipofika. Kwahiyo kama ambavyo waliamua kuanzisha bendi tukawaruhusu, ndivyo ambavyo tutawaruhusu kama wakitaka kuifufua au hata kufanya kolabo.” amefunguka.

SABABU ZA ZUCHU

KUSAJILIWA WASAFI

Aidha, Fella hakuacha kumzungumzia msanii mpya anayekuja kwa kasi kutoka lebo yao ya WCB, Zuhura Othuman ‘Zuchu’ na kuelezea kuwa moja ya sababu chache kati ya nyingi zilizowafanya wamsajili Zuchu ni uwezo wake mkubwa wa kuimba, kuandika mashairi mwenyewe pamoja na kutengeneza melodi (mirindimo) ya muziki wake.

“Wasanii wengi hasa wa kike hawana uwezo huo. Wengi wana sauti nzuri, wanajua kuimba sana, lakini wanachemka kwenye kuandika, wengi wanaandikiwa nyimbo, lakini Zuchu anafanya vyote hivyo na kwa uwezo mkubwa.” ameeleza Fella.

Amesema kitu kingine ni nidhamu, jambo ambalo kwao WCB wanalizangatia kuliko kipaji. Ameeleza kwamba mpaka Zuchu kupata nafasi ndani ya WCB ni kwamba amepitia vipimo vingi vya kuangalia nidhamu yake.

“Unapomuona Lady Jaydee amekuwa msanii mkubwa sio kwa sababu anajua kuimba kuliko wasanii wote, hapana, wapo wasanii wanaomzidi, lakini mafanikio yake yanatokana na heshima na nidhamu. Zuchu pia ni kati ya wasanii wa aina hiyo, wenye nidhamu ya kazi… na kama ataendelee kuwa hivo siku moja atakuwa legend kama kina Lady Jaydee.” ameeleza Fella.

Pia amesema Zuchu yupo Wasafi kwa takrbani miaka mitatu hivi na kwa kipindi chote hicho alikuwa akifanya kazi nyuma ya pazia ikiwa ni pamoja na kurekodi nyimbo zake huku uongozi ukiendelea kumfanyia tathimini.

Mbali na muziki, Fella pia ni mwanasiasa ambaye kwa sasa anagombea kwa kutetea nafasi yake ya udiwani wa kata ya Kilungule.