Ngwasuma Re-union ilifunika, Re-Union Mapacha itaweza kweli?

Muktasari:

“Tingisha kama imeisha... weka nyingine’, ‘Samaki ana vipande vingapi... vitatu.. hebu vitaje... kichwaa, tumbo na mkia.... tingisha mkiaaa,” ni kati ya vichombwezo vilivyowakumbusha mbali mashabiki pale Escape One.

KATIKA Boxing Day, yaani siku moja baada ya Sikukuu ya Krismasi 2019, mastaa waliopata kuitumikia bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ walijumuika pamoja na kufanya bonge la shoo la kukumbushia enzi pale Escape One Dar es Salaam.

Mastaa waliotamba katika bendi hiyo na baadhi yao kuondoka kwa nyakati tofauti walishangiliwa kwa kila walichofanya jukwaani.

Kuanzia Papii Kocha, Patcho Mwamba, Liva Sultan, Totoo Ze Bingwa, Jose Mara, Kardinal Gento, Malou Stonch, Ibonga Katumbi ‘Jesus’, rapa G-Seven, Pablo Masai, King Blaize hadi Elombee Kichinja na wengineo wote waliamsha kumbukumbu nzito ya zama zile za muziki wa dansi ulipokuwa ukitawala soko la burudani nchini.

Tungo tamu kama ‘Dunia Kigeugeu’, ‘Prison’, ‘Hadija’, ‘Heshima kwa Wanawake’, ‘Shida’, ‘Freedom’, ‘Neema’ na nyingine zilileta ladha ile ambayo waliohudhuria walionekana kuimisi sana.

“Tingisha kama imeisha... weka nyingine’, ‘Samaki ana vipande vingapi... vitatu.. hebu vitaje... kichwaa, tumbo na mkia.... tingisha mkiaaa,” ni kati ya vichombwezo vilivyowakumbusha mbali mashabiki pale Escape One.

Kiufupi, Wazee wa Pamba, Wazee wa Mjini, Wazee wa Ngwasuma au Timu ya Taifa, kama walivyokuwa wakijiita, walithibitisha kwamba muziki wa dansi una raha ya kipekee.

Hicho ndicho kilichonisukuma kuuliza swali katika safu hii, kumbe muziki wa dansi bado unapendwa hivi?

Ni kwa sababu katika onyesho lile mashabiki walifurika. Kwenye maegesho ya magari nafasi zilikosekana na ukumbini palikuwa hapatoshi.

Licha ya viingilio kuanzia Sh. 10,000. Sh.50,000 hadi Sh.100,000 kwa VIP, bado mashabiki walifurika. Kumbe muziki wa dansi unapendwa hivi? Hii mitazamo iliyopo kwamba muziki wa dansi umekufa inatokana na nini?

Ama ni kwa sababu vituo vya radio na televisheni vimeacha kupiga nyimbo za dansi?

Je, hiyo ndiyo sababu wanamuziki wengi wakubwa wa muziki wa dansi kupotea na kukata tamaa ya kuendelea kupambana?

Kauli za wadau wengi wa dansi wakiwamo wanamuziki na wamiliki wa bendi, watakwambia muziki wa dansi umepotea kwa sababu nyimbo zao hazichezwi kwenye vituo vya radio, televisheni na wametengwa na magazeti.

Wanasahau dunia hiyo ilishapitwa zamani. Siku hizi kuna ‘sosho media’ ambayo ina nguvu kuliko radio, televisheni na magazeti.

Wangetambua tu kwamba ubunifu na video kali vingetosha kuwafanya wapenye na kutrendi kwenye Instagram, YouTube, mitandao ya mingine ya kijamii.

Wasanii kibao wa vichekesho na kadhalika walikuwa hawajulikani hapo awali na hawajawahi kupaishwa na radio wala TV yoyote lakini wamekuwa maarufu kupitia Insta na YouTube na wanapiga pesa.

Hawa jamaa zetu wa muziki wa dansi wanakwama wapi? Mbona wengi wao hata akaunti za Insta hawana?

Wiki iliyopita, wasanii waliounda bendi ya Mapacha Wanne, ambayo enzi hizo ilipoanzishwa ilipata pigo la kukimbiwa na ‘pacha’ mmoja Charlz Baba kabla hata haijazinduliwa na kulazimika kubadilishwa jina na kuitwa Mapacha Watatu, imeibuka upya kwa ajili ya kufanya matukio maalum.

Memba wa kundi hilo, Khalid Chokoraa, Kalala Junior, Jose Mara na Charlz Baba wameibuka na Mapacha Wanne Re-Union. Pengine mara hii Charlz Baba hataingia mitini mapema.

Wamesema wameona fursa ya kufanya vizuri ndio maana wameungana tena na tayari wameachia wimbo mpya unaokwenda kwa jina la ‘Kapatikana’ ukiwa ni kama muendelezo wa wimbo waliotamba nao awali wa ‘Kuachwa’.

Re-Union ya Ngwasuma ilifunika, ambako Jose Mara pia ni memba, je Re-Union Mapacha itaweza kweli?