Nabii Mswahili: Wema Sepetu kuchapwa na Kamwene! Mbona poa sana

Friday April 19 2019

 

By ELIYA SOLOMON NA OLIPA ASSA

“NCHI yetu imefikia mahali pabaya sana kwa sababu unaweza kumwona mtu anakufa kwa njaa halafu katika msiba wake watu wanapika pilau.

Pia, unaweza ukamkuta mtu masikio katoboa na pua halafu maisha hajatoboa hayo ni matumizi mabaya ya matobo, ukiona maharage yameiva basi kaa ukijua mkaa umeteketea,” hiyo ni miongoni mwa misemo iliyompatia umaarufu Nabii Mswahili.

Ndio! Huyu ni Madebe Lidai ‘Nabii Mswahili’ na kuongeza kwa kusema “huko ndiko tulipofikia Waafrika na ukiona mambo yako hayaendi basi nenda wewe.”

Nabii, ambaye alifurahishwa na ugeni wetu hakutaka makuu, alitukaribisha kijiweni kwake na kuanza kupiga naye stori huku akijipambanua kwa kusema kuwa, hapendi kuishi maisha ya milioni kama wasanii wenzake wakati kipato chake ni laki moja tu.

Katika mahojiano yake, Mwanaspoti likabaini kuwa Nabii Mswahili ambaye ni mshindi kwenye tuzo za Sinema Zetu SZIFF 2019 katika kipengele cha Mchekeshaji Bora ilimchukua zaidi ya miaka 10 kujitengeneza kabla ya kutoboa. Unajua mwanzo wake ulikuwaje? Basi songa naye hapa.

TUZO ALIYOSHINDA

Advertisement

Usiku wa Sinema Zetu, Nabii Mswahili alishinda tuzo moja ya mchekeshaji bora kwenye vipengele kadhaa ambavyo alikuwa akiwania kikiwamo kile cha Msanii Bora wa Kiume.

Mkali huyo wa misemo ambaye aliambatana na mke wake kwenye tuzo hizo wakiwa wamevalia sare za vitenge, ametoa shukrani zake za dhati kwa mashabiki zake ambao, walijitahidi kumpigia kura.

“Wasanii wengine wanaofanya comedy wanatakiwa kujifunza kupitia kwangu kwa kutengeneza filamu zenye kubeba zaidi lugha yetu ya Kiswahili. Filamu yangu ya kuchekesha ya ‘Mama Mwali’ niliamua kuja kitofauti kidogo na imenichukua muda wa zaidi ya miaka mitatu kuikamilisha.

“Mke wangu alisema kuwa lazima tutashinda tuzo moja kwa hiyo najivunia kuwa naye kwenye usiku ule ambao, utakumbukwa kwenye maisha yangu ya sanaa,” anasema Nabii Mswahili.

AMTULIZA WEMA

Kulikuwa na minong’ono mingi kwenye tuzo za SZIFF mwaka 2019 baada ya Flora Kiyombo (11) ambaye alikuwa gumzo kwelikweli kwenye usiku huo. Mastaa wakubwa wa Bongo Movie walitokwa povu na hapo jina la msemo wa Kamwene likashika kasi baada ya msanii huyo kushinda tuzo ya Msanii Bora wa Kike na kuwabwaga waigizaji wakongwe akiwamo mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006.

“Kiukweli ni vizuri kutoa heshima kwa majaji wao wameona aliyeshinda ndiye aneyefaa, Wema anaweza kuwa aliumizwa, lakini atakuwa anapata faraja kuona kuna mtoto anayekuja na anaweza kuibeba Bongo Movie kwa siku za usoni, baada ya wakati wetu kupita,” anasema Nabii Mswahili.

MTEGO WAKE

Nabii Mswahili ambaye ni Mmakonde anasema malengo yake kwenye tuzo hizo yalikuwa ni kushinda tuzo ya Msanii Bora wa Kiume ambayo ilikwenda kwa Rashid Msigala (10).

“Kuna uhaba wa watoto kwenye tasnia ya filamu ndiyo maana sikuchangazwa sana na Rashid kushinda tuzo ile binafsi nimechukulia poa na sikuumizwa kuikosa,” anasema.

UPENYO ULIKUWA HAPA

Baada ya kuumiza kichwa tangu 2005 akiwa kwenye tasnia ya filamu, Nabii Mswahili anasema aliona kuwa movie nyingi zimekosa utunzi wa hadithi nzuri za kuvutia na zenye misingi na tamaduni za Kiswahili.

“Hapo ndipo nilipoamua kuanza kutunga stori ambazo zitakuwa zinawagusa Watanzania moja kwa moja, kwa sababu kuna stori nzuri, lakini siyo za maisha yetu hivyo ni ngumu kuvutia watu.

“Nashukuru Mungu kwa mapokezi ambayo Watanzania wamenipokea ila kimsingi ni kwamba nimetumia miaka mingi kujitengeneza kuwa mimi,” anasema.

SIRI YA MISEMO

“Nasoma sana vitabu vya Kiswahili, huko nimekuwa nikipanua ufahamu wangu. Ni rahisi kuumiza kichwa na kutoa misemo yenye kujenga kutokana na kusoma kwangu vitabu,” anasema.

Nabii Mswahili ambaye ni mhusika wa LP Media ambayo imekuwa ikitumika kuzalisha movie zake, amezungumzia kutumia kwake wasanii wasiokuwa na majina makubwa nchini.

“Mara nyingi msanii chipukizi amekuwa akiumiza sana kichwa ili aweze kupata mafanikio, wasanii wengi wenye majina makubwa tayari wamebweteka kitu kinachopunguza ufanisi wa kazi. “Napenda sana kufanya kazi na wasanii ambao wanatafuta nafasi za kufanikiwa nadhani watu wameona movie yangu ya ‘Nabii Mswahili’ kuanzia sehemu ya kwanza hadi sita,” anasema.

JINA LAKE SASA

“Wengi wananijua kama Nabii Mswahili, mimi sio Nabii ambaye nimeshushwa na Mungu… ha ha ha ha, nataka kuwaweka watu sawa iko hivi, kuna movie yangu ambayo kwa sasa inafanya vizuri ya Nabii Mswahili.

“Kwenye hiyo movie nimecheza nafasi ya mtoto wa baba, ambaye anaitwa Mswahili nikiwa naitwa Nabii kwa hiyo ukiunganisha hap ohayo majina lazima niitwe Nabii Mswahili,” anasema.

BONGO MOVIE IMEKWAMA

Nabii Mswahili anasema kukwama kwa Bongo Movie kumechangiwa na waandaaji wengi kuangalia uzuri wa kimaumbile wa wasanii kuliko uwezo wao wa kazi.

“Nililitambua hilo 2016 pale ambapo zile nafasi nyingi za ushiriki wa wasanii kwenye movie zikibebwa na hao ambao ukiwaangaliwa kiuhalisia uwezo wao ni wa kawaida.

“Ndipo nilipoanza kufanya vurugu kwa kuja na kazi zilizofanya vizuri kwenye mazingira hayo, inatakiwa tubadilike maana Watanzania wanajua movie nzuri ni zipi maana kila kukicha wamekuwa wakitizama walotutangua. “Kama ukimuigizia hovyo hovyo ni ngumu kutoa hela yake mfukoni na kununua movie yako haina kichwa wala miguu,” .

UTAMU UNAKUJA

Unaweza ukamkuta mtu masikio katoboa na pua halafu maisha hajatoboa hayo ni matumizi mabaya ya matobo, ukiona maharage yameiva basi kaa ukijua mkaa umeteketea.

Je unafahamu Nabii huyo ana maisha gani huko kitaani kwake na vipi kuhusu familia yake. Fuatilia simulizi yake kesho Jumamosi.

Advertisement