NDIO NINI SASA ZUCHU KWENDA KUJIFUNZIA KWENYE MECHI?

Tuesday July 21 2020

 

By Luqman Maloto na Dk Levy

UNAMSAJILI vipi mchezaji wa kwenda kumjaribu kwenye mechi kubwa? Hicho ndicho kilichofanywa na uongozi wa WCB, kumtambulisha Zuchu kwenye shoo kubwa Mlimani City, Dar es Salaam, wakati mtoto mwenyewe hata hajaiva. Luqman Maloto na Dk Levy wanaleta shughuli kamili kama ilivyo.

LUQMAN: Hatimaye tumemuona Zuchu na shoo yake ya utambulisho Mlimani City. Bila shaka huu ndio wakati wa kuleta yale maswali ya nani zaidi kati ya Nandy na Zuchu. Huko nyuma mlikuwa mnauliza nani bora kati ya Nandy na kivuli, maana kazi ya Zuchu jukwaani ilikuwa haijulikani, sasa kila mtu ameiona. Niongeze sauti?

DK LEVY: Sauti umuongezee nani? Ile ya Zuchu ilikuwa shoo au utopolo? Na usitake nivunje kikao hapa. Ukiendelea kumfananisha Nandy na utopolo, kikao navunja na kitakuwa hakifanyiki tena. Watu tuliandaliwa muda mrefu kuwa kuna shoo, lakini kitu cha ajabu badala ya shoo, tukaona shombo ya shoo. Mtoto hajui kuimba jukwaani. Hana chochote alichotuonesha. Na ushamba wako unataka nimlinganishe na Nandy.

LUQMAN: Kosa kubwa ambalo utaendelea kuishi nalo miaka yote ni kutojua mtu anayetoa ahadi ya kuwa bora. Ile ilikuwa shoo ya kwanza ya Zuchu. Mtoto bado chipukizi kabisa, halafu akaandaliwa bonge la shoo. Makosa ni waliomuandalia shoo. Walipaswa kuendelea kumpika kwanza aive, ndipo wamdondoshe kibabe. Wao walianza na shoo ya kibabe kupitiliza. Bado nasimama na Zuchu, alithubutu na aliweza. Kwa makosa au upungufu aliouonesha, bila shaka atakwenda kufanyia masahihisho na siku nyingine mtamkoma. Zuchu ameanza vizuri kuliko Nandy alivyoanza.

DK LEVY: Watu wasio na viambata vya kusafisha ubongo huwa wana matatizo mengi sana. Sasa hivi unakuja na hoja ya kwamba Zuchu ameanza vizuri kuliko Nandy alivyoanza. Huko nyuma hamkuwa mkilinganisha mwanzo wao, mlichongoa midomo kuwa Nandy hamuwezi Zuchu. Habari ya kusema Zuchu aliandaliwa shoo kubwa wakati akiwa bado mdogo usitake kuizungumza kama ni vile ni kitu cha kusamehe kirahisi. Walichokifanya WCB ni utapeli. Walijua kabisa Zuchu hakustahili kuandaliwa shoo ya vile, lakini wao wakaitangaza kwa mbwembwe zote. Wakatengeneza fedha nyingi. Ile ndio inaitwa kuuziwa mbuzi kwenye gunia. WCB waliwauzia Watanzania mbuzi kwenye gunia.

Tuliambiwa kuwa mbuzi yupo kwenye gunia. Watanzania kwa imani yao kwa WCB, wakatoa fedha zao, walipokwenda kukagua gunia lenyewe, wakakuta hakuna mbuzi wala mtoto wa mbuzi. Siku nyingine WCB watapata wakati mgumu sana kumuuza msanii wao wakati wa utambulisho, maana itaonekana ndio zao kutapeli.

Advertisement

LUQMAN: Ila wewe jamaa una nongwa sana. Uambiwe nini uelewe kuwa Zuchu ndio anaanza? Kwanza unatakiwa kupokea ujumbe huu; mpaka leo Nandy hajawahi kufanya shoo kama ile ya Zuchu. Maana yake hajiamini. Kwa hiyo Zuchu anajiamini kuliko Nandy. Hayo mengine ya kwamba mmeuziwa mbuzi kwenye gunia ni kimpango wenu. Tunachojua sisi WCB na kamati yetu ni kwamba tuliwaandalia shoo ya Zuchu na mlimuona Zuchu. Aliyeimba hakuwa Rihanna ni Zuchu. Kuna mambo ambayo Nandy sasa anatakiwa kujifunza kwa Zuchu ili aweze kupata mafanikio makubwa ambayo naamini Zuchu atayapata haraka kuliko yeye. Vipi uliona zawadi ya gari alilopewa?

DK LEVY: Nandy ajifunze kwa nani? Tunapoelekea sitaongea tena, utashangaa navuruga meza hapa na natawanya kila kitu ili ujue kuwa nikisema kitu huwa namaanisha. Unaposema Zuchu ndio anaanza, kwani ile shoo iliandaliwa kwa ajili ya maonesho au shoo kamili? Tungeambiwa tunakwenda kusshuhudia mazoezi ya Zuchu wala nisingekasirika. Ningejua alichokifanya Zuchu ndio mazoezi yenyewe. Wale walitwambia tunakwenda kuona shughuli ya Zuchu. Tukauziwa meza shilingi milioni tano. Wewe hujui niliingia gharama kiasi gani kugharamia totoz ziende kumuona Zuchu. Ninapolaumu ujue nipo ‘sirias’. Mimi ni mwathirika wa ile shoo kwa sababu pesa zangu zimekwenda bure.

LUQMAN: Acha nongwa za kimaskini, watu waliingia MGM Grand Garden Arena, Las Vegas kwa mabilioni na kushuhudia Manny Pacquiao na Floyd Mayweather jr, wakikumbatiana badala ya kupigana lakini mpaka leo walishasahau. Wewe unalaumu shoo ya Zuchu wakati kama kuna gharama uliyoingia ni muda wako na pesa za king’amuzi tu. Mlimani City hukwenda, na hakuna yeyote ambaye ulimlipia kiingilio. Sasa nongwa za nini? Unapaswa utulie tuli ushuhudie jinsi ambavyo Zuchu anavyobadili huu upepo. Mdogomdogo utakuja kukubali kuwa Zuchu ndiye mrithi halisi wa cheo cha umalkia wa muziki. Atampokonya mama yake, Hadija Kopa, halafu atamrithi Lady Jaydee. Wewe Konde Boy utabaki na maumivu yako.

DK LEVY: Siku nyingine ukiwa na hoja ya msingi ya kuongea na mimi uniambie nitakuja kijiweni. Kwa sasa ngoja nikuache. Muda huu unanichelewesha kwenda kusikiliza nyimbo za wanamuziki wanaojitambua, Nandy na Ruby. Usiniletee habari za wanamuziki wanaotengenezwa na kiki. Mwanamuziki wa Diamond Platnumz atakosaje kiki? Kwanza lile gari kabla hata siku haijafika, sisi tulijua kuna gari atapewa. Hata yeye Zuchu alijua kungekuwa na zawadi ya gari. Mama yake Zuchu, Khadija Kopa, alitambua uwepo wa zawadi ya gari. Yaani wananunua zawadi halafu wanakubaliana wapeane ufunguo, kisha Zuchu ajilize mbele za watu ionekane ni ‘sapraiz’. Huo utoto utafutiwe chaneli nyingine. Hakuna mtu ambaye hajaushitukia.

Advertisement