MB Dog: Naishi kishua kwa jina tu

Friday November 8 2019

 

By Rhobi Chacha

MIAKA 15 iliyopita tasnia ya muziki wa Bongo Fleva ilikuwa imeshikwa na mkali wa nyimbo zenye ujumbe wa mapenzi Mbwana Mohamed ‘MB Dog’. Hapa ndipo unapokumbuka nyimbo kama Latifah, Si uliniambia (Waja), Mapenzi Kitu Gani, Inamaana, Natamani na nyingine nyingi.

Unajua yuko wapi? Anafanya nini na mipango yake kwenye ishu ya muziki. Mwanaspoti limemzukia mkali huyu ambaye umaarufu wake ulikua kwa kasi mwaka 2004 kutokana na kipaji chake cha kutunga na staili yake ya kuimba ngoma kali na kuteka hisia za mashabiki.

Kumekuwa na maswali mengi kutoka kwa mashabiki wakitaka kufahamu ni nini hatma yake kwenye muziki, baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu na hapa mwenyewe amefunguka kila kitu wakati akihojiwa na timu ya waandishi wa Mwanaspoti.

MB Dog anasema ukimya wake ni kutokana na baadhi ya mambo yalimletea shida , pamoja na Kampuni ya Qs Mhonda J Entertainment aliyokuwa anafanya nayo kazi kuna mambo yalikuwa hayaendi sawa hivyo akaona asilazimishe wakati anajua kuna shida.

“Unajua kuna mambo baadhi yaliniletea shida ndio yaliyonifanya nikae kimya na kingine kampuni ya Qs Mhonda J Entertainment niliyokuwa nafanya nayo kazi ambayo ilinisaidia, baada ya kufanya nao mikataba kuna mambo mengine yakawa yameanguka ya kampuni kwahiyo vitu vikawa haviendi kama watu wanavyotaka.

“Ila naamini kutokana na muda ambao upo kwa sasa nimeanza kufanya kazi zangu binafsi ili nirudi kama watu wanavyotamani. Kuna watu wengi wanataka kunisaidia kuona narudi kwenye anga zangu za zamani. Kwa sasa najipanga zaidi kuona nafanya kazi za uhakika,” alisema MB Dog.

Advertisement

JINA LA MB DOG LINAMFANYA AISHI

MB Dog anasema kutokana na ukimya huo katika muziki, kuna vitu vingine vimekuwa vigumu hivyo, ukubwa wa jina lilipofikia anashukuru kufanya maisha yake kuwa rahisi zaidi.

“Huu ni ukweli kama nilikuwa kimya na maisha yangu yalikuwa kutegemea muziki, hicho ni kitu kimoja cha ajabu sana watu wanishangaa naishi vipi. Lakini, heshima ya jina ndilo linalonifanya hadi leo naishi ingawa kuna watu wengine wakikuona wanaanza kukubeza tu kuwa huyu mbona keshafeli maisha. Niko na familia yangu na kuna mambo mengi yanaendelea kama kawaida,” anasema.

NINI HATASAHAU

“Kitu kikubwa ambacho siwezi kukisahau ni kuwa, kuna watu walikuwa wakiniona hivi wakijua ni kama MB Dog walikuwa wanalia yaani.

Sijui walikuwa wanalizwa na mapenzi au kitu gani, nimeamini kuna kitu nilikifanya katika zile nyimbo zilikuwa zinagusa mioyo ya watu kupitia hizo kazi

“Sababu kuna watoto walizaliwa wakina Latifa, maelefu ya watu walijitokeza kupitia kazi zangu na kuna wengine walikuwa wakisikia nyimbo zangu tu wanatamani kurudiana kwenye mapenzi yao. Nilikuwa naambiwa kabisa wimbo wako umenifanya nirudiane na mke wangu ambaye tuliachana, kitu ambacho nikikumbuka huwa naumia sana, naishia kujiuliza tu kwanini nimenyamaza.

KAMA MUASISI

Ikiwa kama mmoja wa waasisi wa katika muziki, MB Dog anajisikiaje karibu kila msanii anapita mulemule na kuinuka kimaisha huku yeye akiwa kawaida?.

“Hiyo ni kazi ya Mungu unajua katika dunia, kuna maisha ameyatengeneza, kuna kupanda na kushuka hivyo huwezi kukaa juu miaka yote.

Kuna muda unarudi hivyo naamini hiyo ni sehemu ya changamoto katika maisha yangu kwa sababu kuna watu wengine nimewafundisha muziki wanaishi vizuri kupitia muziki kuliko mimi. Nafurahi kuona mbegu niliyoipanda imeota kwenye eneo sahihi na inaendelea kumwagiwa maji ili kustawi zaidi.

Usitegemee mbegu uliyoipanda iote vibaya, hivyo nafurahi sana kuona vijana wanafanya vizuri inakuwa pia changamoto kwenye akili,” anasema MB Dog.

Je unajua MB Dog anashuka kwa staili gani. Na vipi kuhusu Tip Top Connection na memba wake na pia amefunguka kuhusiana na bifu la Diamond na AliKiba. Endelea kufuatilia simuliza lake keshokutwa Jumapili ndani ya Weekend Vibe ndani ya Mwanaspoti.

Advertisement