Harmonize asawazisha bao la Diamond

Monday September 14 2020

 

By NASRA ABDALLAH

Amesawazisha bana. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli kumvalisha kofia msanii Rajabu Abdul maarufu kama Harmonize.

Rais Magufuli alifanya tukio hilo leo Jumatatu Septemba 14 katika mkutano wa kampeni za urais wa chama hicho wilayani Chato mkoani Geita.

Harmonize amevalishwa kofia na Rais Magufuli leo Jumatatu ikiwa ni siku chache tangu afanye hivyo kwa msanii Diamond Platnumz alipotumbuiza kwenye kampeni za CCM Uwanja wa Kirumba mkoani Mwanza.

Katika tukio hilo mara baada ya Diamond kumaliza kuimba wimbo wa Moto, Rais Magufuli alimuita apande jukwaani alipokuwa na alipofika alicheza naye wimbo huo kidogo na kisha kuvua kofia aina ya pama yenye rangi ya kijani iliyo na maandishi ya CCM.

Tukio hilo lilizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii, hususani kwa mashabiki wa Diamond ambao walijuwa kwamba Rais Magufuli anamkubali sana msanii huyo ndio maana kampa heshima ya kumvalisha kofia.

Kitendo cha Rais Magufuli kumvalisha kofia Diamond kiliwaibua mashabiki na wapenzi wa msanii huyo mkubwa Tanzania ambao walikuwa wakimkejeli Harmonize ambaye alijiengua katika lebo ya WBC Agosti mwaka jana.

Advertisement

Hata hivyo, ni kama mgombea huyo ameyasikia majigambo ya pande hizo mbili, na leo Septemba 14, 2020 ameamua kusawazisha kwa kumvalisha kofia Harmonize na hii ni mara baada ya msanii huyo kumaliza kuimba wimbo wa Magufuli.

Kama alivyofanya kwa Diamond, alisimama na kumuita msanii huyo ambaye alikuwa kavaa nguo kama za kijeshi kisha  kumvalisha kofia na kumuacha ashuke chini kuendelea kutumbuiza.

Advertisement