Harmonize anavyoutafuta ufalme mpya

Muktasari:

Mwanaspoti limekuwa likifuatilia maihsa ya msanii huyu tangu aondoke WCB na kwenda kujitegemea akianzisha lebo yake ya Kondegang na ameenda kutengeneza ufalme wake yeye kama yeye.

‘UNo likiteguka huwezi kutembea, Masai rukaruka wanalinyenyekea. Chumbani kwenye shuka linanibebea, mzungu kaweuka limemkolea.’

Hiki ni kipande kutoka katika wimbo wake mpya wa UNO unaozidi kutamba kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kibao hiki ni mwendelezo wa ngoma zake anzozitoa akiwa nje ya kundi la WCB (Wasafi Classic Baby) linaloongozwa na Diamond Platinumz.

Mwanaspoti limekuwa likifuatilia maihsa ya msanii huyu tangu aondoke WCB na kwenda kujitegemea akianzisha lebo yake ya Kondegang na ameenda kutengeneza ufalme wake yeye kama yeye.

Tangu alipoamua kujiweka pembeni na Wasafi Harmonise amefanya ngoma tano tu lakini ameweza kulibakiza jina lake kwenye chati.

Ngoma hizo zimeendelea kutazamwa mara nyingi katika mtandao wa Youtube na mara kwa mara zimekuwa zikisikilizwa ndani ya muda mfupo (ON TRENDING)

MY BOO (Milioni 6)

Wimbo huu aliufanya Remix akishirikiana na Q-Chilla, aliuachia Julai 23 mwaka jana (2019), mara tu baada ya kutoka WASAFI. Ngoma hii imetazamwa na mashabiki 6,055,623 mpaka Januari 2020.

Wimbo huu ulifanikiwa pia kumrejesha kwa kishindo Chilla kwenye ramani ya muziki.

UNO (Milioni 5)

Ni wimbo ambao unapigwa kila sehemu hivi sasa kutokana na mashairi namna ambavyo ameyapangilia kuhakikisha anapeleka ujumbe mzuri kwa mashabiki zake.

Biti lake na namna ambavyo mazingira ya video yalivyo yamefanya wimbo huu utazamwe mara 5,900,238 tangu ilipopandishwa Youtube Novemba 5 mwaka jana.

Wimbo huu umekuwa ni silaha kwa Konde Boy kwani katika shoo yoyote anayopanda huwa anaamua wimbo huo uwe wa kuufungia shoo na kuwapa watu mzuka.

KUSHOTO KULIA (MILIONI 3)

Huu wimbo una mwezi mmoja tu tangu uachiwe Desemba 2 na kuwekwa Youtube. Hata hivyo, mpaka sasa umetazamwa na watu 3, 105, 389.

Licha ya kuondoka Wasafi, Konde Boy kwenye wimbo huu amemtaja kabisa Diamond ndiye amemleta mjini.

Lakini mashairi mengine ni kama anawapiga vijembe watu wengine “Wasionipenda kazi wanayo maana mi pesa ninayo”. Ikiwa ni sehemu ya mashairi ya wimbo huo.

HAINISHTUI (LAKI TISA)

Wimbo huu una siku 15 tangu uachiwe lakini umepokelewa vizuri kwa kutazamwa 923,071 kutokana na namna ambavyo mashairi yake ameyapangiliwa kwa kusema hashtuki kwa lolote ambalo linaendelea kwake.

“Leo nimepata kesho nimekosa, kazi ya mola haina makosa”.

“Huyu kampa boda mwingine kampa Verossa, vuta subra ngoja Mungu hajakutosa”.

“Majungu na fitna zigeuze changamoto, maneno mwacheni nana dawa ya moto ni moto ooh nana nana “.

“Wapo waliosema Konde anapotea lakini chombo inatia gia chombo hiyo inapepea”.

Katika ngoma hii ameonyesha wazi hana habari na mambo yanayoendelea upande wa pili (Wasafi), pia kalenga kwa wengine wasishtuke na jambo lolote ambalo linafanywa na mwenzako basi na wewe ulichukulie kwa upana mkubwa.