Ben aacha maswali Instagram

Saturday October 24 2020
ben pol pic

Ikiwa ni wiki tatu tu zimepita tangu zisambae picha zake za harusi zikifuatiwa na taarifa za kuvunjika kwa ndoa yake, mkali wa R&B bongo Ben Pol ameiteka tena mitandao ya kijamii jana, safari hii ikiwa ni kwa kusambaa kwa picha zinazomuonyesha akiwa msikitini pamoja na picha ya cheti cha uthibitisho wa kubadili dini.

Ben Pol alipost picha 9 kwenye akaunti yake ya Instragam na Twitter zikimuonesha akiwa msikiti wa Masjid Ma’Moor uliopo Upanga Dar es Salaam. Na alisindikiza picha hizo kwa caption ya ‘Bismillah Rahman Rahim’ kisha tarehe ya kupost ‘23-10-2020’.

Picha ya cheti chake cha kubadili dini ilisambazwa na watu wengine mitandaoni ikionesha amebadilisha dini kutoka ukristo kwenda uislamu. Na katika cheti hicho inaonekana pia amebadilisha jina lake la kwanza kutoka Bernard kwenda Benham.

Mwanaspoti ilikwenda mbali na kumtafuta Ben Pol kwa njia ya simu ili athibitishe au kutolea ufafanuzi kile kinachoendelea mitandaoni, hata hivyo hakupokea simu yake. Pia hata alipotumiwa meseji kwa njia ya kawaida na Whatsapp Ben Pol hakujibu licha ya kwamba meseji hizo zilionekana kumfikia na kusomwa.

Aidha post ya Ben Pol imepokelewa kwa namna mbalimbali katika mitandao ya kijamii. Baadhi ya watu hasa mashabiki wameponda uamuzi wake, huku wengine wakimpongeza hususan wasanii.

Mwanamuziki Diamond Platnumz alimpongeza kwa kuandika ‘MashaAllah’, wakati Ommy Dimpoz alicomment ‘Mabrok Mabrok’. Wengine waliotoa neno ni rapa MwanaFA na Fid Q, pia muigizaji Idriss Sultan na watangazaji Salam Jabir na Dj Fetty.

HISTORIA


Kabla ya kubadilisha dini Ben Pol alifunga ndoa ya kimya kimya na mpenzi wake, mfanyabiashara kutoka Kenya anayefahamika kwa jina la Arnelisa, ndoa ambayo kwa sasa imevunjika.

Pia kuhusu imani, kwa mujibu wa karibu wa familia yao inadaiwa kuwa wazazi wake wote wawili ni wakristo wa dhehebu la Roma.

Mwanaspoti inaendelea kumtafuta msanii Ben Pol ili kupata ufafanuzi wa kinachoendelea. Endelea kuwa karibu na tovuti yetu, mitandao ya kijamii na magazeti yetu kwa habari zaidi.

Advertisement