Angel Nyigu, Dansa aliyefanya balaa ndani ya Jeje,Cheche

Saturday October 17 2020

 

Ni kama wazazi walijua hapo baadaye atakuja kuwa nani.Hii ni baada ya kumpa jina la Angle Batolomeo Nyigu.

Jina ambalo limemuwezesha pia kupata jina la kisanii la ‘Angel Nyigu’ likihusishwa na sanaa anyoifanya ya kudansi ambapo ndani yake kuna ukataji mauno.

Angel Nyigu, ni mmoja ya madansa wa kike walio na maarufu katika lebo ya WCB kwa sasa na hii ni kutokana na kuonekana kwenye video nyingi za wasanii waliopo kwenye lebo hiyo ikiwemo Cheche, Jeje na nyingine nyingi.

Akielezea safari yake hadi kujikuta anakuwa dansa maarufu, Angel anasema ilianzia katika mshindano ya kusaka vipaji ya Kinondoni Search yaliyofanyika mwaka 2015, ambayo yaliandaliwa na Paul Makonda, wakati huo akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

“Katika mashindano hayo yaliyofanyika Machi 2015 nikiwa kidato cha nne niliweza kuwa msichana pekee niliyeingia fainali kwa upande wa kudansi na hapo ndipo milango ilipoanza kufunguka kwa kufanya kazi na watu na makundi mbalimbali ya kudansi na tasnia ya muziki,”anasema.

Wakati kuhusu kuwa familia ya WCB, anasema ni baada ya kufanya kazi na Queen Darleen ambaye aliku akihitaji dansa kwa ajili show iliyofanyika Mtwara na hapo ndio ikawa mwanzo wa kuwa dansa wake na ndipo uongozi ulipomuona na kumuita kufanya kazi na wasanii mbalimbali wa lebo hiyo.Ukiachilia mbali Queen Darleen, pia alishafanya kazi na Rosa Ree na Vanessa Mdee na Pam D.

Advertisement

Hata hivyo anasema kuwa kwake na Queen Darleen hakukumzua kufanya kazi na watu wengine, jambo ambalo ndio yupo hivyo hadi sasa kwani hakuna mkataba ambao amejifunga na WCB.

Mbali ya dansa pia amekuwa akiwafundisha watu staili za kucheza, ikiwemo wale wanaotaka kwenda kushuti video za wasanii.

Anajifunzia wapi staili

Angel anasema katika kazi yoyote unayofanya unapaswa kuijua na kwenda na wakati unavyohitaji, hivyo yeye mara kwa mara amekuwa akijifunza kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo youtube, facebook na Instagram ambapo huko amekuwa akipata staili kutoka kwa madansa mbalimbali duniani na vingine anabuni mwenyewe

Changamoto

Kama ilivyo kazi zingine, katika dansa anakutana na changamoto ikiwemo kazi zao kuzipata inategemea sana wanamuziki.

“Hawa ndio watu tunaowategemea sana kutupa kazi, lakini dansa kusimama kama fani yenyewe ikiwemo kuwa na show na mashindano mbalimbali ni mdogo,”anasema

Hata hivyo anasema awali jamii ilikuwa haielewei kuhusu madansa, ikiwemo yeye kupata tabu kukubaliwa katika familia, lakini kwa sasa kuna afadhali jambo ambalo wazazi pia wamekuwa wakiwaruhusu watoto wao kufanya kazi hiyo.

Matarajio yake

Angel anasema matarajio yake ni kwenda kusomea zaidi kazi hiyo huku nchi anayoingalia zaidi kwenda ni Uingereza au Marekani ambapo wameendelea katika fani hiyo.

Jingine anasema anatarajia kufungua chuo cha kufundisha madansa, kwani sasa hivi amekuwa na wanafunzi wa kusoma kwa saa mbili hadi tatu na tayari ameshafundisha watu zaidi ya 400 huku kwa siku akiwa anafundisha watu 30 hadi 40 na kila mmoja humtoza Sh5000.

Wakati akiwa na matarajio hayo anasema kinachomkabili kwa sasa ni kutaka kuongeza ujuzi zaidi kabla ya kufungua chuo hicho, kwa kuwa hataki kufanya jambo hilo kwa kubahatisha.

“Ninachoangalia ni kupata nafasi ya kwenda chuo kuongeza ujuzi, ili nikifungua chuo basi ninakuwa na uzoefu wa darasani pia, kwani kwa sasa nafanyia kipaji nilichozaliwa nacho,” anasema Angel.

Anajisikiaje kuwa WCB

Angel anasema anafurahia kuwa WCB, kwa kuwa wasanii wake ni watu ambao wanaangaliwa sana kiasi cha kumfanya na yeye kupata fursa mbalimbali katika kazi yake.

Wakati kuhusu anavyomchukulia Diamond, anasema ni mtu ambaye anapenda kusaidia vijana wenzake na kuona wanapiga hatua.

Wakati ushauri wake kwa watoto wa kike, anasema wasikubali kuyumbushwa na mtu yoyote wanapoaamini katika ndoto zao, kwani hata yeye alipata vikwazo mbalimbali mpaka kufika hapo lakini anahukuru sasa wanamuunga mkono hii yote ikichangiwa na misimamo aliyokuwa nayo.

Ni kupitia kipaji chake hicho kwa sasa anaendesha maisha yake ikiwemo kupangisha nyumba yake tofauti na awali alipokuwa akiishi kwa dada yake.

 

Advertisement