Rekodi ambazo Salah ameweka na anazodaiwa

Muktasari:
- Mpaka sasa kuna rekodi ambazo staa huyo wa kimataifa wa Misri amezivunja katika namna ya kushangaza na kuna rekodi ambazo bado anadaiwa na anaweza kuvivunja wakati huu ligi hiyo ikiwa imebakiza mechi saba kwa kila timu kufika mwisho.
BAADA ya kufunga mabao manne katika pambano la Liverpool dhidi ya Watford wikiendi iliyopita, staa wa Liverpool, Mohamed Salah anaonekana kupita matazamio ambayo mashabiki wa Liverpool walikuwa nayo juu yake wakati akijiunga na klabu hiyo akitokea Roma katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.
Mpaka sasa kuna rekodi ambazo staa huyo wa kimataifa wa Misri amezivunja katika namna ya kushangaza na kuna rekodi ambazo bado anadaiwa na anaweza kuvivunja wakati huu ligi hiyo ikiwa imebakiza mechi saba kwa kila timu kufika mwisho.
REKODI alizoweka
Mabao mengi msimu wa kwanza
Mpaka sasa winga huyo wa zamani wa Basel na Chelsea ametupia mabao 36 katika msimu wake wa kwanza na kwa kufanya hivyo anakuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Liverpool kufunga mabao mengi katika msimu wake wa kwanza tu.
Salah amefunga mabao 28 katika Ligi Kuu, moja katika Kombe la Ligi na mengine saba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Ameivunja rekodi ya staa wa zamani wa Liverpool, Fernando Torres ambaye katika msimu wake wa kwanza Anfield 2007/08 alifunga mabao 33.
Mabao mengi zaidi msimu mmoja
Tayari staa huyu ameifikia rekodi ya staa wa zamani wa Liverpool, Robbie Fowler kwa kufunga mabao 36 katika msimu mmoja. Katika msimu wa 1995/96, staa huyo wa zamani wa England alifunga mabao 36 katika mechi 53. Bao lolote ambalo Salah atafunga kuanzia sasa litamfanya avunje zaidi rekodi baada ya kuifikia.
mabao mguu wa kushoto
wakati mashabiki wengi wakiamini Fowler alikuwa na uwezo mkubwa wa kutumia mguu wa kushoto, kwa sasa inabainika kuwa Salah ni hatari zaidi. Katika mabao ambayo amefunga msimu huu, Salah amefunga mabao 23 kwa kutumia mguu wa kushoto. Awali rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Fowler ambaye msimu wa 1994/95 alifunga mabao 19 kwa kutumia mguu wa kushoto.
Mabao mengi zaidi Ulaya
Kuna ligi kubwa tano Ulaya. England, Italia, Ujerumani, Hispania na Ufaransa. Mpaka sasa Salah ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu ya England kuliko wengine walivyofunga katika ligi zao. Salah ana mabao 28 na kwa kufanya hivyo amewazidi mabao manne Ciro Immobile, Edinson Cavani, Lionel Messi na Harry Kane ambao wote wana mabao 24 kila mmoja.
Mashuti manne, mabao manne
Katika pambano dhidi ya Watford, mashuti yote manne ambayo Salah alipiga yalitinga katika wavu. Kwa kufanya hivyo aliifikia rekodi ya staa wa zamani wa Arsenal, Andrey Arshavin ambaye katika pambano kati ya Arsenal dhidi ya Liverpool dimba la Anfield mwaka 2009 aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza na pekee katika Ligi Kuu ya England kufunga mabao manne kwa kupiga mashuti manne tu katika lango.
Mabao mengi mechi moja
Mabao manne ya Salah dhidi ya Watford yamemuweka katika kundi moja na wachezaji wakongwe wanaoheshimika sana Anfield. Kwa kufanya hivyo, staa huyu wa Misri alifikia rekodi zilizowekwa na wachezaji wenzake wa zamani kufunga mabao manne ndani ya mechi moja ya Ligi Kuu ya England. Awali ni wachezaji watatu tu ndio ambao waliwahi kufanya hivyo. Anaungana na Fowler aliyewahi kufanya hivyo mwaka 1995 na 1996), Michael Owen aliyewahi kufanya hivyo mwaka 1998 na 2003 pamoja na Luis Suarez aliyewahi kufanya hivyo mwaka 2013.
REKODI AMBAZO HAJAVUNJA
Zimebaki mechi saba za Ligi Kuu ya England kumalizika na Salah bado ana kazi ngumu ya kufanya kufikia mambo makubwa ambayo yalishafanywa na mastaa mbalimbali wa Ligi Kuu ya England waliopita ingawa kuna uwezekano mkubwa akafikia mambo hayo.
Rekodi za Shearer na Cole
Mpaka sasa Salah analazimika kufanya kazi kubwa kuwa mfungaji bora mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England.
Ni wachezaji wanne tu katika historia ambao wamewahi kuwa wafungaji bora huku wakiwa wamepitisha mabao 30. Hao ni Andy Cole, Alan Shearer, Cristiano Ronaldo na Luis Suarez. Hata hivyo ni Cole na Shearer ndio ambao wamewahi kufunga mabao mengi zaidi ndani ya msimu mmoja. Kuna misimu tofauti ambayo walifunga mabao 34 kila mmoja na hivyo kufikia rekodi hizo.
Kama Salah atafunga mabao sita katika mechi saba zilizobaki, basi atafikia rekodi hiyo. Kama atafunga mabao saba ndani ya mechi saba basi ataweka rekodi mpya.
Rekodi ya Didier Drogba
Mpaka sasa rekodi ya Mwafrika aliyefunga mabao mengi katika Ligi Kuu ya England ndani ya msimu mmoja inashikiliwa na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na Timu ya Taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba ambaye katika msimu wa 2009/10, alifunga mabao 29 huku akiibuka kuwa mfungaji bora.
Salah anahitaji bao moja tu kufikia rekodi ya Drogba. Kwa moto alionao sasa hivi ana uwezo wa kuifkia na kuipiku rekodi hiyo.
Rekodi ya Ian Rush
Katika zama mpya, tayari Salah ameweka rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja. Hata hivyo, ana kazi kubwa ya kufanya kufikia rekodi ya staa wa zamani wa timu hiyo, Ian Rush ambaye msimu wa 1983/84 alifunga mabao 47 katika mechi 65.
Kabla hata Salah hajaifikiria rekodi hiyo bado ana kazi ya kuifikia rekodi ya mkongwe Roger Hunt ambaye msimu wa 1961/62 alifunga mabao 42. Lakini Rush pia msimu wa 1986/87 alifunga mabao 40 huku Hunt pia naye msimu wa 1964/65 alifunga mabao 37.
Rekodi ya Sam Raybould
Vipi kuhusu wastani wa kufunga mabao? Kwa kufunga mabao 36 katika mechi 41, Salah ana wastani wa kufunga mabao asilimia 0.88 kwa mechi. Bado yuko nyuma ya wakali wengine kama Sam Raybould (0.94 mwaka 1902/03), Jack Parkinson (0.94 mwaka 1909/10) na Roger Hunt (0.91 mwaka 1961/62).
Rekodi ya Suarez
Pamoja na moto huu wa Suarez, bado ana deni kubwa la kufikia rekodi ya kufunga mabao mengi ya ligi ndani ya msimu mmoja katika klabu yake ya Liverpool. Msimu wa 2013/14, Suarez alifunga mabao 31 na wakati huu ligi ikiwa imebakiza mechi saba, Salah ana mabao 28 na amebakiza mabao matatu kuifikia rekodi ya Suarez huku akiwa amebakiza mabao manne kuivuka rekodi hiyo ndani ya klabu.