Kuwanasa hadi uvunje kibubu

Muktasari:
- Barcelona, Real Madrid na Paris Saint-Germain zinachuana kuwania huduma yake baada ya kufurahishwa na kiwango chake ambapo msimu huu amefunga mabao 37 katika mechi 43 alizocheza na kuongoza kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya.
LONDON, ENGLAND
MOHAMED Salah ameripotiwa kutengewa kiasi cha Pauni 200 milioni kwa ajili ya kung’olewa huko Liverpool mwishoni mwa msimu huu.
Barcelona, Real Madrid na Paris Saint-Germain zinachuana kuwania huduma yake baada ya kufurahishwa na kiwango chake ambapo msimu huu amefunga mabao 37 katika mechi 43 alizocheza na kuongoza kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya.
Lakini, kiwango hicho cha pesa kinachotajwa kwamba atauzwa ni zaidi ya mara tano ya kile kilichotumika na Liverpool kupata saini yake wakati ilipomsajili kutoka AS Roma mwaka jana.
Hata hivyo, Salah si mchezaji pekee ambaye kama atabadilisha timu kwenye dirisha lijalo saini yake haiwezi kupatikana kwa pesa isiyofika Pauni 200 milioni baada ya kuwapo wengine hawa kibao.
Harry Kane (Tottenham)
Kiwango cha kutupia wavuni cha Harry Kane kinawafanya vigogo kibao Ulaya kuchuana kuwania huduma yake. Manchester United, Manchester City na Real Madrid zinatajwa kuhitaji saini yake kabla ya Bayern Munich kuibuka siku za karibuni na kudai inamtaka aende akachukue mikoba ya Robert Lewandowski kwenye kikosi hicho.
Lakini, ukweli upo wazi tu kama Spurs ilimuuza Gareth Bale kwa Pauni 85 milioni miaka mitano iliyopita, unadhani itamuuza Kane kwa sasa kwa kiasi gani cha pesa kwa soko hili la wachezaji lilivyo kwa kipindi hiki.
Man United na Real Madrid zinafahamu kabisa saini ya Kane haiwezi kupatikana kwa pesa isiyozidi Pauni 200 milioni.
Leroy Sane (Man City)
Sane ni kinda matata kabisa mwenye mvuto wa kumtazama kwenye soka la Ligi Kuu England hasa kutokana na uwezo wake wa kupiga mabao kwenye kikosi cha Manchester City sambamba na Mbelgiji, Kevin De Bruyne. Kinda huyo amepiga asisti zaidi ya 10 kwenye Ligi Kuu England na kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji hatari kwelikweli.
Umri wa Mjerumani huyo ndiyo kwanza miaka 22 na Man City ilimnasa kwa Pauni 37 milioni na kumsainisha mkataba wa miaka mitano wa kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Lakini, kwa sasa Sane ukimtaka tu, basi utapaswa kuweka mezani mkwanja usiopungua Pauni 200 milioni.
Dele Alli (Tottenham)
Mwaka 2017, Dele Alli alisaini mkataba na Creative Artists Agency, kampuni ya kiwakala inayowasimamia pia Jose Mourinho, Cristiano Ronaldo na Harry Kane. Kampuni hiyo inafanya kazi kwa karibu sana na Gestifute, kampuni ya kiwakala inayosimamiwa na wakala matata kabisa mwenye dili za kibabe, Jorge Mendes.
Kwa umri wa Dele Alli na kiwango chake cha mpira ni wazi kabisa ukihitaji saini yake kwa sasa kumng’oa Tottenham Hotspur, basi jipange kwa mkwanja mrefu. Dele Alli huwezi kumchomoa kwenye timu hiyo kwa ada inayopungua Pauni 200 milioni huku jina lake liliwahi kuhusishwa na timu za Real Madrid na Man United ambao ndiyo hasa inaonekana kuwa na uwezo wa kuhimili wachezaji wa bei mbaya wa aina yake.
Neymar (PSG)
Paris Saint-Germain ililipa Pauni 198 milioni kupata saini yake wakati ilipomnasa kutoka Barcelona mwaka jana. Akiwa hana hata msimu mmoja, tayari Mbrazili huyo ameshaanza kuhusishwa na mpango wa kuondoka kwenye kikosi hicho, huku Real Madrid, Manchester City na Manchester United zikitajwa kuwa kwenye vita kali ya kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo.
Ni jambo la wazi kabisa kama bei aliyonunuliwa miezi kadhaa iliyopita ni Pauni 198 milioni, bila ya shaka ukimtaka Neymar kwa sasa basi uende kuifanya PSG na pesa yako isiyopungua Pauni 200 milioni, kuna timu zinazotajwa kutaka kudaiwa kuwa tayari kulipa hata Pauni 300 milioni.
Mauro Icardi (Inter Milan)
Staa wa Kiargentina, Mauro Icardi anatajwa kuwa mmoja kati ya washambuliaji wa kati mahiri kabisa katika soka la kisasa. Wakala wa mchezaji huyo, mrembo Wanda Nara, ambaye pia ndiye mke wa mshambuliaji huyo amekuwa akimnadi muda wake kwamba ni bonge la mchezaji na kudai huduma yake imekuwa ikiwindwa na klabu vigogo mbalimbali barani Ulaya. Kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wa mchezaji huyo kinadai kama kuna timu itahitaji saini yake, basi italazimika kulipa Pauni 100 milioni.
Lakini, mrembo Wanda amefichua kuna dili jipya atasaini mchezaji huyo na hilo likikamilika basi kwa timu itakayomhitaji baada ya hapo, basi ijipange na mkwanja unaoanzia Pauni 200 milioni. Real Madrid, Man United na Chelsea zinamtaka fowadi huyo.
Eden Hazard (Chelsea)
Supastaa wa Chelsea, Eden Hazard amekuwa akihusishwa na Real Madrid kwa muda mrefu sana.
Mwaka 2015, Kocha Jose Mourinho kipindi hicho akiwa Chelsea kabla hajatua Manchester United, alisema Hazard kama kuna timu inamtaka italazimika kulipa Pauni 200 milioni, yaani kila mguu thamani yake ni Pauni 100 milioni. Tangu wakati huo hadi sasa, Hazard bado amekuwa kwenye uvumi wa kuwindwa na Real Madrid na hilo linaweza kutokea mwishoni mwa msimu huu kutokana na mipango ya rais wa timu hiyo, Florentino Perez kutaka kushusha majembe ya nguvu tu kuifanya Los Blancos kuwa tishio msimu ujao.
Timo Werner (RB Leipzig)
Bayern Munich ilifichua inampigia hesabu straika Timo Werner aendee akachukue mikoba ya Robert Lewandowski, ambaye anaweza kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Timo bado kijana mdogo, umri wake ndiyo kwanza miaka 22 tu, hivyo kuna miaka mingi sana mbele yake ya kuendelea kulitumikia soka.
Liverpool pia inahitaji saini yake na msimu huu ameshatupia wavuni mabao 18 katika michuano tofauti aliyocheza. Lakini, kwa timu yoyote itakayojifanya kwenda kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo basi mfukoni ni lazima iwe na mkwanja unaoanzia Pauni 200 milioni.
Paulo Dybala (Juventus)
Supastaa wa Kiargentina, Paulo Dybala umri wake ni miaka 24 tu. Amekuwa akihusishwa na timu za Manchester United, Real Madrid na Barcelona ambazo zitahitaji huduma yake, lakini Juventus imeweka wazi mchezaji wake huyo hauzwi.
Kwa timu king’ang’anizi zinazohitaji huduma yake, basi zijipange kweli kweli kwa sababu Dybala hawezi kung’oka Juventus kwa mkwanja ambao haujafika Pauni 200 milioni.
Hiyo ndiyo pesa inayoweza kumuondoa huko Turin staa huyo licha ya mabosi wa Juventus kudai kama Neymar ameuzwa kwa bei ile, basi Dybala atakuwa Pauni 300 milioni.
Marcus Rashford (Man United)
Rashford ni bonge la staa na ni mchezaji mwenye viwango vyote vya kuwa straika wa kutisha kwenye soka la ulimwengu.
Si mchezaji mwenye uoga katika kuwakimbiza mabeki wa timu pinzani na mara zote amekuwa habatishi kwenye kutupia mipira wavuni. Yupo kwenye klabu kubwa kabisa duniani na umri wake wa miaka 20 unampa ruhusa ya kuendelea kuwa bora zaidi.
Real Madrid iliripotiwa kuisaka huduma yake, lakini ukitaka saini ya mshambuliaji huyo kwa soko hili la kisasa, usiende na pesa yako isiyofika Pauni 200 milioni.
Mohamed Salah (Liverpool)
Liverpool inajiweka kwenye nafasi nzuri kabisa ya kupiga pesa ndefu kutokana na kiwango cha staa wao wa sasa Mohamed Salah anachokicheza kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Anfield.
Liverpool ilimsajili mchezaji huyo kwa Pauni 34 milioni tu akitokea AS Roma mwaka jana, lakini kwa kiwango chake cha msimu huu hadi sasa tayari ameshavutia vigogo kibao wanaohitaji huduma yake, ikiwamo Real Madrid, Barcelona na Paris Saint-Germain.
Kwenye dirisha la Januari tu hapo, Liverpool ilimuuza staa wake Philippe Coutinho kwenda Barcelona kwa ada ya Pauni 142 milioni, hivyo kwa jambo hilo, kana kuna timu yoyote itahitaji saini ya Mo Salah, basi ifahamu wazi itapaswa kulipa dau linaloanzia Pauni 200 milioni kwenda juu.