BITEBO: Nilizawadiwa makofi kwa kuwa Mchezaji Bora-2

Tuesday April 11 2017

 

By SADDAM SADICK, MWANZA

WIKI iliyopita tulianza simulizi ya nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na Pamba ya Mwanza na Taifa Stars, Khalid Bitebo ‘Zembwela’.

Nguli huyo aliweka bayana namna wachezaji wa Pamba walivyonusurika na kifo baada ya mashabiki wa Yanga kukerwa na kipigo cha mabao 2-0 walichowapa kwenye Uwanja wa Uhuru (zamani Taifa).

Zembwela alisema dalili za hatari zilianza kwa mmoja wa mashabiki wa Yanga kuvamia uwanja akiwa na kisu mkononi kwa nia ya kumchoma nacho mwamuzi, lakini mmoja ya wachezaji wa Pamba, Shaaban Katwila alijitoa mhanga na kumwokoa mwamuzi kwa kumdaka na kumng’ang’ania shabiki huyo.

Hali hiyo iliwafanya wachezaji wa Pamba kuambizana wasifunge tena mabao zaidi ya hayo mawili ili kuepusha maafa, lakini wakati wakiwa kwenye basi lao wakielekea Mwanza njiani waliviziwa na mashabiki wa Yanga na kuanza kuwashambulia kwa mawe, kiasi basi liliharibika kwa kuvunjwa vioo vyote.

Lakini, unajua Bitebo alitokea wapi mpakia kutua Pamba na ilikuwaje akapata nafasi Taifa Stars na nini mtazamo wake katika soka la kimataifa? Endelea naye...!

 

ALIKOTOKEA

Bitebo, anasema soka amezaliwa nalo kwani aliupenda mchezo huo tangu alipokuwa kinda na alivutiwa kutokana na kaka zake, Mzomwe Masoud na Tanu Athuman, walivyokuwa wakicheza timu ya Chumvi ya Uvinza Kigoma. Walimpa mzuka.

Anasema wakati kaka zake hao wakicheza, yeye alikuwa akisoma Shule ya Msingi Kiganamo iliyopo mkoani Kigoma, ambako alishaanza kucheza timu ya shule katika mechi za kirafiki na za kimashindano.

 

MCHEZAJI WA MAKOFI

Soka la zamani wakati mwingine linafurahisha sana, wakati wachezaji wa sasa wakishinda Tuzo za Mchezaji Bora hujinyakulia zawadi za fedha na vitu vingine, Bitebo yeye mwaka 1972 alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora kwenye shule yake, lakini hakupewa zawadi nyingine zaidi ya kupigiwa makofi.

“Zawadi hazikuwapo, hivyo tuzo yangu iliishia kupigiwa makofi,” anasema Bitebo kisha kuongeza: “Kaka zangu baada ya kusikia nimechaguliwa Mchezaji Bora, walininunulia viatu kwa ajili ya kuanza kucheza soka mitaani.”

Anasema kitendo hicho kilimhamasisha zaidi kujikita katika soka, kiasi kwamba hata alipokuwa amelala usiku alikuwa akiota yupo uwanjani anacheza.

 

MILANGO YAFUNGUKA

Anasema mwaka mmoja baadaye, alisafriri mpaka Mwanza kwa ndugu zake ambapo kwa kipindi kifupi tu mambo yalimnyookea baada ya kulamba shavu timu ya Biashara, enzi hizo ikifahamika zaidi kama State Trading Cooperation (STC) kabla ya kubadilishwa jina na kuwa hilo maarufu la Biashara FC.

Anaeleza kuwa timu hiyo ilikuwa tishio enzi hizo na ilikuwa na wachezaji wakali waliokuwa wakichuana vikali na klabu za Pamba na Coop United kiasi cha kuwa mwiba, kwani Biashara ilikuwa ikigawa dozi kadiri itakavyo kwa timu hizo.

 

TP LINDANDA WAMBEBA

Kutokana na kupiga soka la uhakika, mabosi wa timu mbalimbali za jijini Mwanza walianza kummezea mate na Pamba ya Mwanza maarufu kama TP Lindanda ikafanikiwa kumbeba baada ya kuvutiwa naye na kumpa vishawishi.

“Pamba walivutiwa nami na kuanza kuniwinda kabla ya kuniweka faragha na kuzungumza nami kwa kina na kuafikiana kujiunga nao,” anasema.

Anasema alikubali kujiunga na timu hiyo mwaka 1974 na kuanza kuitumikia kwa mafanikio kiasi cha mwaka mmoja tu kuitwa ndani ya kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilikuwa imesheheni nyota waliokuwa wakali enzi hizo.

Mechi mbalimbali za kimataifa alizocheza akiwa na Stars zilimfanya ajitangaze, lakini kubwa ni faraja aliyoipata kwa kucheza na nyota ambao alikuwa wakiwaota na kutamani mafanikio yao, jambo lililomwongezea ari ya kufika mbali.

 

TIMU TISHIO

Bitebo aliyekuwa akicheza nafasi ya mshambuliaji, anasema enzi akicheza, soka la Tanzania lilikuwa katika kiwango cha juu na kuwapo kwa timu tishio ambazo zilifanya mashabiki wa soka kushindwa kutabiri mechi za ligi mapema.

Hata hivyo anasema miongoni mwa timu zilizokuwa tishio kwao na kilichokuwa kinawasumbua Pamba katika mechi zao ni Simba, Yanga, Coastal Union na Pan Africans, kiasi kwamba mechi zao zilikuwa zina maandalizi tofauti na nyingine.

“Hizi timu zilikuwa kali kwelikweli na hata mashabiki walioenda uwanjani walikuwa wakipata burudani kwa soka lililopigwa na timu hizo, tofauti na sasa ni rahisi kutabiri matokeo kabla ya mchezo kuchezwa,” anasema.

 

WALIOMNYIMA RAHA

Bitebo aliyestaafu soka la ushindani mwaka 1988, anasema licha ya umahiri wake uwanjani, lakini kuna baadi ya wachezaji waliokuwa wakimnyima raha kila alipocheza dhidi ya timu zao.

Kwa Simba amewataja Shaaban Baraza na Athuman Juma, wakati Pan Africans ni Mohammed Rishard ‘Adolph’, Leodgar Tenga na Mohammed Mkweche.

“Kuwapita hao ilikuwa lazima uwe jasiri kwani walikuwa wagumu kupitika,” anasema.

“Halafu walikuwa makatili kweli, ukizembea kidogo wanaweza kukupeleka nje, hasa kama ulikuwa msumbufu langoni mwao, kwa kweli niseme wazi walikuwa wakininyima raha na kila nikikutana nao nilicheza kwa umakini.

“Hata Yanga nako kulikuwa na visiki ambao ilibidi kufanya kazi ya ziada kuwapenya, kulikuwa na Hassan Gobbos na Omar Kapera ‘Mwamba’, aisee acha kabisa, siku hizi mabeki wa kazi sijui wamepotelea wapi.”

Hata hivyo anasema pamoja na ukali wa mabeki hao, bado TP Lindanda iliwagaragaza kwa sababu nyota wake akiwamo yeye walikuwa wakisakata soka kali na ndio maana haikuwa ajabu mashabiki wa Yanga kufikia hatua ya kuwafanyia fujo.

Bitebo ndio kwanza anaanza kufunguka maisha yake ya soka, lakini unajua pambano ambalo haliwezi kusahaulika kichwani mwake ni lipi? Unataka kujua lilichezwa lini? Unataka kuvifahamu pia vitendo vya ushirikina alivyowahi kukutana navyo enzi akicheza? Ungana naye Jumanne ijayo upate majibu yote.