Zari asaini mkataba mnono Bongo

Muktasari:
- Amesaini mkataba huo leo na Kampuni ya Kedz Tanzania
Dar es Salaam. Mpenzi wa zamani wa mwanamuziki Diamond Platnumz, Zari The Boss Lady ametua nchini kwa ajili ya kusaini mkataba wa ubalozi wa Kampuni ya Kedz Tanzania inayojihusisha na utengenezaji wa pampasi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo Jumatano katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam, Zari ambaye ni mama wa watoto watano amesema anashukuru kupata mkataba na kampuni hiyo.
Hata hivyo, kiu ya wanahabari ilikuwa kusikia akizungumzia uhusiano wake uliovunjika lakini alikwepa swali hilo akidai kuwa si kilichomleta.
“Unajua hii ni kazi na haihusiani kabisa na masuala ya familia, hivyo nisingependa kulizungumzia hilo leo,” alifafanua.
Zari alitangaza kuachana na mwanamuziki Diamond Platnumz Februari 14 mwaka huu kupitia mtandao wa Instagram.
Wiki mbili baadaye akihojiwa na Kituo cha BBC Swahili, Zari alisema ameamua kuachana na Diamond kutokana na sababu mbalimbali moja ikiwa ni kushikana hadharani na mwigizaji Wema Sepetu.