Ukuta wa Taifa Stars wazuia Sh132bil za WaCongo

HAKUNA aliyetegemea kuwa safu ya ushambuliaji ya DR Congo ingeshindwa kuipenya ngome ya Taifa Stars kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika juzi Jumanne ambapo wageni hao walichapwa mabao 2-0.
Hiyo ilitokana na benchi la ufundi la DR Congo chini ya Kocha Florent Ibenge kupanga nyota wote wanaotamba kwenye klabu za soka barani Ulaya huku safu ya ulinzi ya Stars ikiundwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza ligi ya nyumbani.
Katika mchezo huo, nyota wanne walioanza kwenye safu ya ushambuliaji ya DR Congo ni Benik Afobe (Wolverhampton) na Neekens Kebano (Fulham) za Ligi Daraja la Kwanza England, Firmin Ndombe Mubele (Toulouse ya Ligi Kuu Ufaransa) na Yannick Bolasie (Everton, Ligi Kuu England) huku Assombalonga Britt (Middlesbrough) na Junior Kabananga (Al Nasr) wakitokea benchi.
Kwa mastraika hao kuondoka patupu, gazeti hili limebaini mbali ya kuzuia majina hayo makubwa kutamba, ukuta wa Taifa Stars ulifanikiwa kuwaweka mfukoni nyota wenye thamani inayokadiriwa kufikia Sh132 bilioni.
Kiasi hicho cha fedha ni zaidi ya mara 100 ya thamani ya mabeki wanne wa Taifa Stars waliocheza mchezo huo ambao ni Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Abdi Banda na Kelvin Yondani.
Kwa mujibu wa rekodi na taarifa za usajili duniani, kiasi cha fedha ambazo klabu hizo za Ulaya zilitumia kuwanunua Afobe, Kebano, Mubele, Bolasie, Assombalonga na Kabananga ni Euro 47.3 millioni (Sh132 bilioni).
Tofauti na thamani kubwa ya mastaa hao, thamani ya mabeki wanne wa Stars waliocheza mchezo huo haizidi hata Sh150 milioni.