Phantom yaanza mikakati mizito

Mwanza. Baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Mkoa wa Mwanza kwa Phantom FC, Kocha wa timu, Mathias Wandiba amesema kuwa ataongeza wachezaji watano kabla ya kuanza kwa Ligi ya mabingwa wa mikoa ili kukiweka fiti kikosi chake.
Phantom ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo baada ya kumaliza mechi zake za hatua ya Tisa Bora ikiwa kileleni kwa pointi 21, ikiziacha Igoma Heroes waliovuna alama 19 na Copco pointi 15.
Kocha Wandiba alisema kuwa kwa sasa mkakati wake ni kuongeza wachezaji watano katika safu ya kipa, beki wa kulia na wa kati, kiungo mshambuliaji na straika.
Alisema kuwa licha ya kwamba wachezaji walioipa ubingwa kuwa na uwezo katika kusakata kandanda, lakini kutokana na ushindani uliopo kwenye Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, lazima aongeze nguvu.
“Kwa sasa mkakati wetu ni kuhakikisha tunajiandaa kwa ajili ya Ligi ya mabingwa wa mikoa, nitaongeza wachezaji watano ili mashindano yakianza tuwe tayari kiushindani,” alisema Wandiba.
Aliongeza kuwa kipindi hiki Phantom si ya mtu mmoja bali inawakilisha Mkoa, hivyo wadau wa soka mkoani Mwanza waungane kwa pamoja kuisapoti ili ifanye vyema.
Kocha huyo alisema kuwa licha ya kutwaa ubingwa, lakini Ligi ilikuwa ngumu kutokana na ushindani walioupata na kwamba wangezembea katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Copco Veterans wangeukosa.
“Kwa ujumla Ligi ilikuwa na ushindani, lakini tulipambana na kufanikiwa kutwaa ubingwa,niwaombe wadau tuungane kwa pamoja ili Mwanza iweze kusonga mbele,” alisema kocha huyo.