Mashabiki wamvamia Ronaldo uwanjani

Muktasari:
- Miongoni mwa mashabiki aliyeruka uzio alimvaa nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ureno na kumpiga busu.
Geneva, Uswis. Mshambuliaji nguli wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuvamiwa na mashabiki uwanjani.
Miongoni mwa mashabiki aliyeruka uzio alimvaa nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ureno na kumpiga busu.
Ronaldo akionekana kushikwa na mshangao alipigwa busu hilo na shabiki wa kiume kabla ya kupiga naye picha kwa kutumia simu ya mkononi.
Pia mmoja wa mashabiki alimvaa mshambuliaji huyo na kumkumbatia kwa furaha huku Ronaldo akiwa ameduwaa.
Matukio hayo yalitokea katika mchezo wa kirafiki uliomo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambao Ureno ilichapwa mabao 3-0 na Uholanzi mjini Geneva, Uswis.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani, Ureno ililazimika kucheza pungufu uwanjani baada ya beki Joao Cancelo kulimwa kadi nyekundu.
Nahodha wa Uholanzi na libero wa Liverpool, Virgil van Dijk aliongoza vyema kupata ushindi mnono.
Van Dijk alifunga bao na mengine yakiwekwa wavuni na mshambuliaji nyota wa zamani wa Manchester United, Mephis Depay na Ryan Babel.
Kocha Ronald Koeman amepata ushindi wa kwanza tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo ya Uholanzi huku akimteua Van Dijk kuwa nahodha wake.
Wakati mchezo ukiendelea, idadi kubwa ya mashabiki walikuwa na shauku ya kuruka uzio kumvamia Ronaldo.
Hata hivyo, mashabiki hao hawakuwa na madhara kwa mchezaji huyo bora mara tano wa dunia.