MJUE Kocha anayeongoza kwa mataji Top Six England

Muktasari:
Kwenye Ligi Kuu England kama si makocha watatu au wanne kati ya watano waliobora kabisa duniani kwa sasa, basi wapo kwenye ligi hiyo.
LONDON, ENGLAND
LINAPOKUJA suala la makocha bora duniani, Ligi Kuu England imekuwa na mvuto mkubwa kwa makocha hao.
Kwenye Ligi Kuu England kama si makocha watatu au wanne kati ya watano waliobora kabisa duniani kwa sasa, basi wapo kwenye ligi hiyo.
Ukichukua tu timu sita zinazoshika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, makocha watano bora kabisa wanatamba.
Kuna Pep Guardiola, Jose Mourinho, Jurgen Klopp, Antonio Conte na Arsene Wenger. Lakini, unamjua mwenye mataji mengi kuliko wengine? Bahati mbaya kwa Mauricio Pochettino wa Tottenham Hotspur hayupo kwenye orodha hii kwa sababu hajawahi kubeba taji lolote tangu awe kocha. Makocha wa Top Six England wanaoongoza kwa mataji.
5. Jurgen Klopp- mataji 5
Liverpool mara ya mwisho kubeba ubingwa wa ligi ni zaidi ya miaka 30 iliyopita. Walikaribia kulibeba taji la Ligi Kuu England mwaka 2009 na 2014, lakini gundu liliendelea ikashindwa. Kwa sasa ipo nafasi ya tano katika msimamo wa ligi, ikiachwa pointi kibao na vinara Manchester City. Kocha wa timu hiyo, Jurgen Klopp alibeba ubingwa wa ligi akiwa na Borussia Dortmund na hilo linaipa matumaini kwamba kuna siku inaweza kuizindua na kubeba taji hilo inalolisaka kwa muda mrefu. Msimu huu imeonyesha upinzani mkali na ipo kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Klopp kwenye maisha yake ya ukocha amebeba mataji matano:
BORUSSIA DORTMUND:
Bundesliga: 2010–11, 2011–12
DFB-Pokal: 2011–12
DFL-Supercup: 2013, 2014
4. Antonio Conte- mataji 7
Antonio Conte mambo yake si haba pia. Kocha huyo Mtaliano alipotua tu Stamford Bridge aliifanya Chelsea kuwa na makali ya maana uwanjani.
Conte alifanya kile ambacho makocha wengi wamekuwa wakikishinda, kubeba taji la Ligi Kuu England katika msimu wake wa kwanza tu.
Msimu wake wa pili, mambo ni magumu na hafahamu kama timu yake itakamatia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Chelsea inahitaji kupambana kwelikweli kumaliza msimu ikiwa kwenye kiwango bora ili iwe ndani ya Top Four, la sivyo mambo yatakuwa magumu kwa kocha wake. Katika maisha yake ya ukocha, Conte amebeba mataji saba.
BARI:
Serie B: 2008–09
JUVENTUS:
Serie A: 2011–12,
2012–13, 2013–14
Supercoppa Italiana: 2012, 2013
CHELSEA:
Ligi Kuu England
2016/17
3. Arsene Wenger- mataji 20
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ni miongoni mwa makocha ambao wanajivunia kazi yao hiyo kutokana na kuvuna mataji mengi.
Wenger alitua Arsenal mwaka 1996 na jambo la wazi kabisa kuwa alifanikiwa kuibadili klabu hiyo kwa kuisaidia kushinda mataji 15.
Alijiunga na Arsenal akitokea Nagoya Grampus ya Japan, ambako pia alibeba mataji ya kutosha. Aliichapa Chelsea 2-1 kubeba taji la Kombe la FA msimu uliopita kuokoa kibarua chake. Msimu huu nafasi pekee iliyobaki ya kubeba taji moja tu, Europa League na atahitaji kufanya kufanya hivyo ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
MONACO:
Ligue 1: 1987–88
Coupe de France: 1990–91
NAGOYA GRAMPUS:
Emperor’s Cup: 1995
J-League Super Cup: 1996
ARSENAL:
Ligi Kuu England: 1997–98, 2001–02, 2003–04
FA Cup: 1997–98, 2001–02, 2002–03, 2004–05, 2013–14, 2014–15, 2016-17
Ngao ya Jamii: 1998, 1999, 2002, 2004, 2014, 2015
2. Pep Guardiola- mataji 22
Pep Guardiola alimaliza mikono mitupu kwenye msimu wake wa kwanza klabuni Manchester City, lakini msimu huu tayari ana uhakika wa mataji mawili, Kombe la Ligi na Ligi Kuu England amebakiza mechi chache tu kulibeba.
Alibeba Kombe la Ligi kwa kuichana Arsenal kwenye fainali. Na sasa zimebaki wiki chache tu kujibebea taji la Ligi Kuu England kutokana na pengo la pointi aliloweka baina yake na timu nyingine. Alipokuwa Barcelona alibeba kila taji ambalo lipo kwenye mchezo wa soka na alipokwenda Bayern Munich, nako alibeba mataji ya kutosha tu na kumfanya afikishe mataji 22 katika maisha yake ya ukocha.
MAN CITY:
Kombe la Ligi 2017/18
BARCELONA:
La Liga: 2008–09, 2009–10, 2010–11
Copa del Rey: 2008–09, 2011–12. Supercopa de Espana: 2009, 2010, 2011
Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2008–09, 2010–11
UEFA Super Cup: 2009, 2011. Klabu Bingwa Dunia: 2009, 2011
BAYERN MUNICH:
Bundesliga: 2013–14, 2014–15, 2015–16
DFB-Pokal: 2013–14, 2015–16
UEFA Super Cup: 2013
Klabu Bingwa Dunia: 2013
1. Jose Mourinho- mataji 25
Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho yupo kwenye presha huko Old Trafford kwa sasa kutokana na kushindwa kujihakikisha taji msimu huu. Kikosi chake kimebakiza tumaini moja tu la mataji kwa msimu huu, Kombe la FA. Lakini, mataji na Mourinho ni vitu viwili vinavyoendana. Msimu wake wa kwanza Man United huko Old Trafford alitwaa taji la Kombe la Ligi na Europe League. Msimu huu mambo hayaendi kabisa, lakini bado kuna taji linaweza kunaswa na kocha huyo. Kwenye maisha yake ya kisoka, Mourinho amebeba mataji 25 yanayotambulika.
FC PORTO:
Primeira Liga: 2002–03, 2003–04. Taca de Portugal: 2002–03. Supertaca candido de Oliveira: 2003
Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2003–04. UEFA Cup: 2002–03
CHELSEA:
Ligi Kuu England: 2004–05, 2005–06, 2014–15
FA Cup: 2006–07
Kombe la Ligi: 2004–05, 2006–07, 2014–15
Ngao ya Jamii: 2005
INTER MILAN:
Serie A: 2008–09, 2009–10
Coppa Italia: 2009–10
Supercoppa Italiana: 2008
LIgi ya Mabingwa Ulaya: 2009–10
REAL MADRID:
La Liga: 2011–12
Copa del Rey: 2010–11
Supercopa de España: 2012
MAN UNITED:
Ngao ya Jamii: 2016
Kombe la Ligi: 2017
Europa League: 2017.