VIDEO- Lechantre: waleteni hao

MFARANSA wa Simba, Pierre Lechantre hana presha kabisa na mechi dhidi ya mahasimu wao, Yanga. Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wanaendelea kujifua vikali ili kuiangamiza Njombe Mji na kuondoka na pointi tatu kwenye Uwanja wa Sabasaba.

Imeelezwa kuwa ushindi dhidi ya Njombe Mji Jumanne ijayo utawapa mzuka zaidi wa kupambania ubingwa na kutibua historia ya Yanga.

Mchezo wa mahasimu hao umepangwa kupigwa Aprili 29 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo mshindi atakuwa ametanguliza mguu mmoja katika vita ya kubeba ubingwa msimu huu.

Simba na Yanga kwa sasa zinakabana kileleni kwa pointi 46 huku Wekundu wa Msimbazi wakiongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, pia wana mchezo mmoja mkononi.

Hata hivyo, habari njema ni kwamba tayari kocha Lechantre akisaidiana na Masoud Djuma wameanza kuifuatilia Yanga kwa karibu ili kuangalia mbinu za kuithibiti.

Akizungumza na Mwanaspoti, Lechantre kwa mara ya kwanza amekiri kufuatilia staili ya soka la Yanga hasa kwenye eneo la ushambuliaji linaloongozwa na Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu pamoja na lile la ulinzi ambalo linaongozwa na Kelvin Yondani.

“Wana timu nzuri kwa muda niliyoiona, ina wachezaji wengi wazuri tofauti na maeneo ambayo nimeyataja, lakini si muda sahihi kuwazungumzia kwa lolote,” alisema.

“Akili yetu ipo kwa Njombe na nyingine kabla kuikabili Yanga, lakini nitaendelea kuiangalia zaidi katika maeneo hayo mawili ili kuona mambo ambayo yatatupa faida tukikutana.

“Najua mechi ya Yanga ni ngumu na nimeshaambiwa hilo, lakini itakuwa vyema kupata kwanza pointi tatu katika kila mechi ambayo ipo mbele yetu na baada ya hapo tutafanya maandalizi ya kutosha kwa Yanga.

“Kwa sasa natangeneza timu ya kucheza soka la haraka na pasi na sitataka mchezaji kukaa na mpira muda mrefu, hiyo ndio njia nzuri ya kucheza kwa sasa.”

OKWI, BOCCO USIPIME

Kwa upande wake, Djuma alisema malengo yao ni kuchukua ubingwa, lakini watatangeneza mfumo wa kuwatengenezea nafasi nyingi za kufunga kinara wa mabao, Emmanuel Okwi na John Bocco ili mmoja wao aibuke mfungaji bora. Okwi ana mabao 16 mpaka sasa.

“Nadhani itapendeza pale tunapochukua ubingwa na mfungaji bora atoke Simba, hayo ni malengo ambayo tumejiwekea msimu huu, na nina imani tunaweza kuyatimiza,” alisema Mrundi huyo.

“Kama Okwi na Bocco wakiwa wanatamani kufunga katika kila mechi zilizobaki, inaweza kuwa faida kwetu kupata pointi tatu ambazo tunazihitaji.

“Lakini, kufunga ni jambo la nafasi, hata kama Kichuya aliyefunga saba au mchezaji mwingine yeyote klabuni tunampa nafasi, hiyo yote ni katika kuona namna Simba inavyokuwa bingwa msimu huu.”