Kocha Lwandamina amvutia kasi Ngoma

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Donald Ngoma, ameanza kazi na kikosi cha kwanza tayari kwa mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA, lakini kocha wake George Lwandamina, amesema bado anahitaji muda zaidi kumfanyia tathimini ya ubora.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lwandamina amesema Ngoma alianza mazoezi ya peke yake kwenye kambi yao fupi mjini Morogoro, ambapo kwa sasa ameingia katika mazoezi ya kikosi cha kwanza.
Mzambia huyo anayesaka taji la pili tangu atue Yanga, amesema anahitaji muda zaidi kufuatilia uwezo wa Ngoma kabla ya kutoa tathimini yake.
Ndani ya siku mbili kabla ya kuivaa Singida United, Lwandamina amesema atakuwa amepata picha kamili kuhusiana na Mzimbabwe huyo aliyepachika mabao matatu tu hadi sasa msimu huu.
Hata hivyo, Ngoma amemweleza Lwandamina kuwa yuko kamili kuivaa Singida United na hata mechi ya Welayta Dicha ya Ethiopia, yuko ngangari kinoma.
“Amekuwa nje kwa muda mrefu, nitatumia siku mbili kumuangalia uwezo wake kama ataonyesha kuwa sawa tutajua cha kufanya ingawa mwenyewe yuko tayari kwa mapambano,” alisema Lwandamina.
ANASA FAILI LA WAHABESHI
Katika hatua nyingine, Lwandamina msione yuko kimya kumbe amenasa nusu ya taarifa zote za Welayta Dicha ya Ethiopia watakaovaana nao Kombe la Shirikisho, baada ya tajiri mmoja kumtafutia mikanda ya mechi za timu hiyo. Lakini, Mzambia huyo ameonya kuwa Wahabeshi hao si timu ya kudharauliwa hata kidogo.
Amesema katika video za mechi mbili za Dicha alizoangalia, amebaini kuwa jamaa ni wazuri na wanaotumia mbinu ambazo ni ngumu kuwadhibiti.
Miongoni mwa mechi ambazo Lwandamina ameaziangalia ni pamoja na ya ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Zamalek na kubaini mambo kadhaa.
Alisema Dicha ina wachezaji watatu hatari zaidi na ambao Mwanaspoti ilikuorodheshea katika gazeti la juzi Jumanne akiwemo straika Djako Arafat, raia wa Togo ambaye hutumika akiwa mshambuliaji pekee pindi timu inapokuwa ugenini.
Mbali ya Arafat, mwingine ni yule Bezabih Melayu Mekengo, ambaye aliwafunga Zamalek bao la kwanza. Lwandamina amesema Mekengo ni hatari na anatakiwa kubanwa ili asifanye maamuzi karibu na lango huku pia kiungo wao Abdulsemed Usman akiichezesha timu vizuri.
“Hatutakiwi kuwadharau kabisa kwa kuwa si timu nyepesi. Tunatakiwa kuwaheshimu, lakini sio kuwaogopa,” alisema.
“Wana watu watatu hatari sana, yule mshambuliaji wao anayevaa jezi namba 10 (Arafat) anajua kuwatuliza mabeki wakiwa ugenini na wanamtanguliza mbele, lakini pia yule jezi namba 17 (Bezamih) tunatakiwa kuwa naye makini na hata yule jezi namba nane (Usman) anaijua kazi yake.”