Kesi ya Malinzi mambo yameiva

MAMBO yameiva unaambiwa. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Aprili 11 inatarajia kuwasomea maelezo ya awali vigogo watatu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), akiwamo aliyekuwa Rais, Jamal Malinzi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, kueleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Baada ya kueleza hayo, Swai aliiomba mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali ya kesi yao.
Vigogo wanaokabiliwa na kesi hiyo mbali ya Malinzi ni Katibu Mkuu Mwesigwa Selestine na Mhasibu Nsiande Mwanga.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29 mwaka jana wakikabiliwa na mashtaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha Dola za Marekani 375,418. Malinzi anakabiliwa na mashtaka 28 huku wenzake wakikabiliwa na makosa yasiyozidi manne.
Wakati kesi hiyo ikitajwa washtakiwa wote walikuwapo mahakamani na wanatetewa na mawakili, Nehemia Nkoko, Dominician Rwegoshora, Abraham Senguji na Kashindye Thabiti.
Kwa muda mrefu mawakili wa utetezi walikuwa wakilalamikia kuchelewa kwa upelelezi.