Haifai

Muktasari:
Makipa David de Gea na Pepe Reina wa Hispania pamoja na Marc-Andre ter Stegen wa Ujerumani wametoa kauli za kushangaza za kutiwa hofu na mipira ambayo itatumika kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika Russia baadaye mwakani.
MADRID, HISPANIA
INASHANGAZA lakini siri ya mtungi aijuaye ni kata. Kombe la Dunia linakaribia na tayari hofu imeanza kuwaingia makipa ambao wanatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo.
Makipa David de Gea na Pepe Reina wa Hispania pamoja na Marc-Andre ter Stegen wa Ujerumani wametoa kauli za kushangaza za kutiwa hofu na mipira ambayo itatumika kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika Russia baadaye mwakani.
Kampuni ya Adidas imepewa tenda maalumu ya kutengeneza mipira katika michuano hii na imetengeneza mipira ya aina ya Telstar ambayo kwa mara ya kwanza ilitengenezwa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 1970.
Katika kipindi cha majira ya joto mwaka huu, Telstar itasherehekea miaka 48 ya kuanziswa kwake na itakuwa inarudi kwa mara nyingine tena baada ya mara ya mwisho kutumika mwaka 1974. Hata hivyo, mipira hiyo imeanza kupata upinzani.
Kipa wa Manchester United, David de Gea ambaye anatazamiwa kukaa katika lango la Hispania katika michuano ya Kombe la Dunia Russia baadaye mwakani ameongoza makipa wenzake kulaumu jinsi ambavyo mipira hiyo imetengenezwa.
Kipa huyo amesisitiza mipira hiyo ingeweza kutengenezwa kwa namna nyingine tofauti na ingekuwa mizuri zaidi.
“Inashangaza sana. Ingeweza kutengenezwa na kuwa mizuri zaidi ya ilivyo,” alisema kipa huyo ambaye alifungwa bao moja katika pambano la kirafiki na mshambuliaji wa Ujerumani, Thomas Muller katika pambano kati ya Hispania na Ujerumani Ijumaa usiku ambalo lilimalizika kwa sare ya 1-1.
Pepe Reina, kipa wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa ni kipa namba moja wa Napoli ya Italia huku akiwa msaidizi wa De Gea katika kikosi cha Hispania alimuunga mkono kipa mwenzake huyo kuwa mipira hiyo haipo sawa.
“Nafikiria tutaona mabao kama 35 hivi ya mbali katika michuano ya Kombe la Dunia Russia, kwa sababu ni vigumu sana kuzuia mipira hiyo. Imetengenezwa kwa nyuzi ambazo ni ngumu kuushika mpira vizuri. Makipa watakuwa na matatizo makubwa na mipira hii,” alisema Reina.
Wakati De Gea na Reina na wakilalamika hivyo, kipa wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen ambaye kwa sasa ni kipa namba moja wa Ujerumani kutokana na kuumia kwa mwenye namba yake, Manuel Neuer naye alilalamika anahitaji muda kuweza kuzoea mipira hiyo.
“Mipira ingeweza kutengenezwa vizuri zaidi. Ina kasi sana. lakini nadhani itabidi tuizoee tu kuifanyia kazi mapema na kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia. Hatuna jinsi nyingine,” alisema kipa huyo mrefu ambaye anaweza kukaa katika lango la Ujerumani kama Neuer atashindwa kupona kabla ya muda kutokana na kuwa nje kwa muda mrefu.
Malaamiko ya makipa hao watatu maarufu yamekuja huku kukiwa hakuna muda wa kubadilisha mipira hiyo. Katika michuano iliyopita ya Kombe la Dunia iliyofanyika Brazil Kampuni ya Adidas ndio iliyopewa tenda ya kutumika kwa mipira yake katika fainali za Kombe la Dunia.
Mipira hiyo iliyopewa jina la Adidas Brazuca ilipelekwa kwa timu mbalimbali ambazo zingeshiriki michuano hiyo kwa ajili ya kuizoea mapema. Awali ilitumika katika michuano ya Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 20, pia ikatumika katika pambano la fainali Kombe la Ujerumani.
Kila timu ambayo ilitazamiwa kushiriki michuano hiyo ilipelekewa mipira hiyo kwa ajili ya kujiandaa kabla ya fainali hiyo na kuizoea na hakukuwa na malalamiko yoyote kuhusu mipira hiyo huku Ujerumani ikichukua ubingwa wa fainali hizo.