Gidabuday aanika changamoto za uongozi

Arusha: Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday amesema kuwa anayeweza kujua mwisho wa uongozi wake katika shirikisho hilo ni Mungu pekee na siyo binadamu.
Alisema kuwa kumaliza muda wa uongozi wake sio torati ambayo haiwezi kubadilika bali inategemea na upepo wa unavyokwenda katika Shirikisho hilo ambalo kwa sasa mambo yanaonekena kuvurugika kwa kila kukicha.
“Jambo likisemwa huwezi kupinga kirahisi inawezekana chanzo chako cha habari alinikuta nikiongea nikiwa katika hisia tofauti kwani mwanzo wa hayo yote ni changamoto zilizoikumba kambi ya Taifa iliyopo Arusha hasa kwa wanariadha wanaokwenda Jumuiya ya Madola ndipo yalipoanzia hayo yote,” alisema Gidabuday.
Alisema changamoto zilizojitokeza katika kambi hiyo ilisababisha anyoshewe vidole kila mara, huku akilaumiwa na kufanya hata kujutia nafasi yake ya uongozi na kuanza kujua watu wanaomzunguka wana tabia za namna gani.
“kila mara nasimamia maamuzi ya uongozi imara sio kufata tamko la mtu mmoja kwani nikifanya hivyo nitakuwa kama kibaraka na mnafiki kwa viongozi wenzangu ambao hupenda haki na wenye hofu ya Mungu.”
“Kelele za nje haziwezi kuninyima nisitende vyema kwenye nafasi yangu bali ukiona hivyo ujue hata ndani ya RT kuna watu, kwani hata kambi ya Arusha watu waligoma kutokana wachache kutaka iwekwe West Kilimanjaro wakati ilishindikana.”
Aliongeza kuwa shirikisho hilo ilikuwa haina hata kijiko lakini kutokana na changamoto za wanariadha wa timu ya JKT kuondolewa kambini ndio iliwapa nguvu ya kuanza kusaka kambi yao na kupata vitanda vyao kupitia Mdhamini wa kambi hiyo.