Bariadi Utd watinga nusu fainali kwa mbwembwe

Mwanza. Bariadi United imetinga hatua ya nusu fainali ya Ligi Daraja la Tatu mkoa wa Simiyu baada ya juzi kuwabamiza Mtoni FC mabao 3-0 katika mpambano uliopigwa kwenye Uwanja wa Halmashauri mjini Bariadi.
Katika mpambano huo ambao ulichezwa kwa upande mmoja, Bariadi United waliweza kupata bao la kuongoza dakika ya 31 ambalo lilipachikwa na Edward Michael.
Bao hilo liliwavuruga wachezaji wa Mtoni FC ambao walijikuta wakipachikwa jingine la pili dakika ya 38 ambalo tena lilifungwa na Straika Michael.
Kipindi cha pili, Bariadi United waliendeleza makali yao na kufanikiwa kupata bao la tatu ambalo liliwekwa nyavuni kwa mara nyingine na Mshambuliaji Michael ambaye alikuwa nyota wa mpambano huo.
Katika mchezo mwingine wa Ligi hiyo, Ambassador FC walifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuwatandika Ginner FC mabao 2-0 kwenye mtanange uliopigwa Uwanja wa Maswa.
Mratibu wa Ligi hiyo, Kulwa Mtebe alisema kwa ushindi huo timu ya Bariadi United imetinga hatua ya nusu fainali ambapo sasa watakinukisha na Ambassador FC.