Arusha yaandaa mashindano ya riadha

Arusha: Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA) kimeandaa mashindano ya wazi ya mchezo huo kwaajili ya kuanza kusaka vipaji vitakavyochaguliwa kwenye timu ya Taifa kuelekea Mashindano ya Afrika Mashariki na Kati pamoja na mashindano ya Taifa.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi, Thomas Tlanka alisema kwa kuwa Arusha ndio tegemeo kubwa la Taifa katika mchezo huo umeamua kujiwekea utaratibu wa kuandaa mashindano ambayo itasaidia jopo la ufundi la RT kupata wanariadha kwa urahisi.
“Hakuna siri kuwa Arusha ikilala basi Tanzania nzima itakuwa ni vigumu kupata timu Bora kwa kuwa ushahidi upo wazi hata katika timu iliyokwenda Australia asilimia kubwa ni wanariadha kutoka Arusha” Alisema Tlanka.
Aliongeza kuwa mfumo wa kuandaa mashindano hayo ni endelevu na hii ni baada ya kumaliza yale maandalizi ya mbio za Nyika zilizofanyika kwa miezi mitatu mfululizo na kuweka timu ya mkoa tayari kwa mashindano yatakayojitokeza.
Ili kupata wanariadha mahili wafukuza upepo hao wataoneshana ubavu katika awamu tatu, awamu ya kwanza itakuwa Aprili saba, huku mchujo wa pili ukifanyika Aprili 28 na kuhitimisha Mei tano.
Tlanka aliongeza fahali yao ni kuona timu ya Taifa inatawaliwa na wanariadha kutoka mkoani hapa sio wa mbio ndefu pekee hata wale wanaoshiriki mbio fupi ambao ni ngumu kuwapata.
Mashindano hayo yatahusisha wanariadha wasiozidi umri wa miaka 19 katika mbio za uwanjani za 100, Mita, 200 mita, 400 mita 800, 1500, 5000 mita, 10,000 mita pamoja na miruko na mitupo.