Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kila la heri wanamichezo wetu wa Madola, msituangushe Australia

TIMU ya Taifa itakayoiwakilisha Tanzania katika Michezo ya Madola, imeagwa rasmi jana na leo Alhamisi inaanza safari kwenda nchini Australia kuanza kupeperusha Bendera ya Taifa katika Michezo ya Madola.

Msafara wa watu karibu 30 wakiwano wachezaji 16 wa Riadha, kuogelea, ngumi na mpira wa Meza pamoja na makocha watano na viongozi saba wataianza safari hiyo leo wakiwa wamebeba matarajio ya Watanzania zaidi ya 45 milioni.

Timu hiyo iliagwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ambaye aliwasisitizia wachezaji wetu watambue wana dhima kubwa ya kulibeba taifa na katu wasifikiri wanaenda Australia kutalii.

Hata Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Alex Nkeyenge alionya timu zinazokwenda kushiriki Michezo hiyo ya Madola kuwa, wasifanye vibaya na kuishia kutoa visingizio kwamba walifanya maandalizi duni.

Kwa hakika timu hiyo pamoja na makocha wao na viongozi wanaoambatana nao watambue kabisa wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanaipeperusha vyema Bendera ya Taifa kwa kuhakikisha hawarudi mikono mitupu.

Mwanaspoti linaamini, licha ya changamoto ambazo wachezaji wetu wamekutana nazo kabla ya kuanza safari hiyo, bado wakiamua na kujitoa kimasomaso wanaweza kufanya maajabu na kurejea Tanzania wakiwa na medali kadhaa.

Tunafahamu timu hiyo imepoteza kujiamini na kukatishwa tamaa na kilichotokea katika kambi ya riadha kwa wanariadha nyota na tegemeo kwa taifa kuondolewa licha ya kuwepo kwa juhudi za kutaka warejeshwe na kwenda kulibeba taifa.

Hatutaki kuamini kama siasa hizi ambazo wakati mwingine zinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya michezo nchini, kama yatawafanya waliopewa jukumu la kuibeba bendera ya Taifa kuzembea. Hapana tunaamini watapambana kwa dhati.

Watanzania wanahitaji kuona Tanzania inarudi na medali kupitia michuano hiyo, habari za kuwa wasindikizaji wa wenzetu inapaswa kubaki historia tu kwa michezo iliyopita na kwa kuwa huu ni msimu mwingine lazima tufanye kweli.

Inakatisha tamaa kweli kuona watu wenye uwezo wa kubeba medali wakiachwa nyumbani kwa sababu ya masuala ambayo yangeweza kutatuliwa mapema kwa kuzingatia kuwa ratiba ya michezo hii ilifahamika mapema, lakini bado tunawataka wachezaji waliosalia kutokuvunjika moyo na badala yake wakapambane.

Hakuna njia ya kutengeneza majina yao na heshima kwa taifa kama kufanya vizuri katika michezo hiyo itakayoanza Aprili 4-15 na kurudi na medali kuthibitisha kuwa, hawakupelekwa Australia kama watalii bali wanamichezo washindani.

Mambo yote yaliyowavunja moyo na vikwazo vyote walivyokumbana navyo wakiwa kambini katika maandaliai ya michezo hiyo, wayasahau kwa sasa na kujua jukumu kubwa lililopo mbele yao ni kurejea Tanzania wakiwa na medali.

Inawezekana isiwe kazi rahisi kutokana na ugumu wa mashindano hayo na jinsi mataifa mengine shiriki yanavyotilia mkazo na umuhimu michezo ya kimataifa tofauti na ilivyo kwetu, lakini bado wachezaji hao wakijawa uzalendo wataweza.

Alphonce Simbu na Emmanuel Giniki, hata wao walifanya vizuri katika michezo mbalimbali waliyoshiriki kutokana na uzalendo walioutanguliza, hivyo hata kina Seleman Kidunda na wenzake wa ngumi ama kina Sara Ramadhani na wengine wanaokwenda kuipeperusha Bendera ya Taifa Australia wakiamua wanaweza kung’ara.

Mwanaspoti kama mdau mkubwa wa michezo nchini tunawatakia kila la heri na safari njema msafara wa timu yetu, lakini tukiwasisitizia wanamichezo wetu kuwa, wasiende kinyonge Australia, waende kama wanajeshi waliotumwa vitani.

Katika vita vyovyote, mwanajeshi anapaswa kupigana kufa na kupona ili kulipa ushindi jeshi na taifa lake, ndivyo tunavyoamini wanamichezo wetu watapigana kufa na kupona Madola na kurejea na medali za kutosha. Hii inawezakana kabisa.

Hata hivyo, ikitokea kwa bahati mbaya watarudi mikono mitupu, bado tutawapokea kwa sababu tunajua kitu gani kilichowaangusha mapema, ila kwa sasa wavae ujasiri na uzalendo kwa masilahi na heshima ya taifa pia kwa manufaa yao!

Mungu Ibariki Tanzania, Wabariki Wanamichezo wetu.