Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubaridi hunivaa nikiwaona Salah, Victor Wanyama

Muktasari:

Biashara ya makoti na skafu za shingoni hushamiri kwa kiasi kikubwa hapa kipindi kama hiki, hata biashara ya mpira hushika kasi kwa kiasi kikubwa.

TUPO kipindi cha baridi sana nchini England; pamoja na baridi kuwa kali haipunguzi shughuli nyingine kuendelea.

Biashara ya makoti na skafu za shingoni hushamiri kwa kiasi kikubwa hapa kipindi kama hiki, hata biashara ya mpira hushika kasi kwa kiasi kikubwa.

Wakati ligi za Ufaransa, Ujerumani, Italia, Hispania na nchi nyingine zikipumzika kwa muda kadhaa kwenye? kipindi cha baridi, huku England mrundikano wa michezo huongezeka.

Timu hucheza mechi mpaka nane ndani ya mwezi mmoja na viwanja hujaza mashabiki bila kujali ni kipindi cha baridi.

Hata wachezaji huzidi kuonyesha uwezo mkubwa, uwezo ambao unawafanya wawe nguzo kwenye timu zao.

Mmoja wa wachezaji ambao msimu huu wamekuwa nguzo kubwa kwenye timu yake ni Mohamed Salah, mtu ambaye natoka naye bara moja.

Amekuwa akitukuzwa sana kwenye uwanja wa Anfield, uwanja ambao kwa msimu huu haujapata matokeo ya kupoteza kwa Liverpool.

Uwanja ambao mashabiki wa timu yake huwa hawana likizo ya kushangilia ndani ya dakika zote 90, na siku hizi wametunga wimbo maalumu kwa ajili ya Mohamed Salah.

Mashabiki hawaoni ajabu yoyote kuimba kwa furaha jina la Salah kwa sababu wanafurahishwa sana na kiwango chake.

Mchango wake umekuwa mkubwa sana msimu huu, magoli 28 akiwa amebakiza mabao matatu kuipita rekodi ya Didier Drogba ambaye anashikilia rekodi ya mchezaji kutoka bara la Afrika kumaliza msimu wa Ligi Kuu ya England akiwa na magoli 31.

Safari yake inaonekana fupi na rahisi sana kwenda kuivunja rekodi hii Drogba. Taratibu anaanza kujiwekea ufalme ndani ya timu ya Liverpool.

Ni ufalme unaomfanya aonekane kama mtu anayehusudiwa kwa kiasi kikubwa ndani ya timu ya Liverpool.

Wivu wa maendeleo hunijaa zaidi pale ninapoenda Wembley na kumuona Victor Wanyama, mchezaji kutoka Kenya, nchi ambayo ni nchi jirani na yangu Tanzania.

Ni nchi ambayo mazingira yetu Watanzania na Wakenya hayapishani kwa kiasi kikubwa lakini wao amefanikiwa kupeleka mchezaji kwenye ligi kuu ya England. Hapa ndipo ubadiridi huja na kuuvaa mwili wangu.

Kwa nini macho mpaka sasa hayajafanikiwa kutazama mchezaji anayetoka katika nchi yangu ya Tanzania? Ni kweli nchi yetu haina vipaji ambavyo vinaweza vikavuka mpaka kuja huku England kucheza angalau ligi daraja la kwanza ?

Ni kweli tumekosa mawakala ambao wanaweza kumsaidia mchezaji apate timu ambayo itakuwa daraja kwao kufika huku England? Kuna wakati nilipata faraja kwa kiasi kikubwa niliposikia Said Ndemla amefuzu majaribio nchini Sweden; moyo wangu ulianza kupata matumaini.

Nilianza kuuona mwanga kwa mbele, nilijua kwa sababu ni ngumu kwa mchezaji kutoka moja kwa moja kwenye ligi kuu ya Tanzania na kuja kucheza kwenye ligi kuu England kwa sababu ya viwango vya chini vya Fifa tunazoshika.

Kuwapo kwenye familia ya mpira wa Sweden kunakupa nafasi kubwa sana kuliko kwenda moja kwa moja kucheza katika Ligi Kuu ya England, lakini nilinyong’onyea sana niliposikia Said Ndemla wa Simba amekataa kucheza kwenye timu aliyofuzu majaribio kwa sababu timu yake ilishuka daraja kutoka ligi kuu mpaka ligi daraja la kwanza.

Niliumia sana kuona kwenye dunia hii ya ushindani kuna watu wanaoamini kupata mafanikio kwa muda mfupi, hivi hawakuona umuhimu wa Said Ndemla kucheza Ligi Daraja la kwanza la Sweden?

Hawakuamini katika juhudi? Simanzi hili nililipata hata kipindi ambacho Mrisho Ngassa aliposhindwa kufuzu kucheza katika timu ya West Ham United.

Inawezekana leo hii ningekuwa jirani wa Mrisho Ngassa na Familia yake hapa London, lakini matamanio yangu yamekuwa kinyume na ukweli ninaoushuhudia.

Ni ukweli unaoonesha dhahiri kuwa pamoja na kwamba Tanzania tuna vipaji vikubwa lakini tunakosa watu wa kusimamia na kuvipeleka sehemu kubwa hivi vipaji ndiyo maana vinakufa bila na mafanikio yoyote makubwa ndani yao. Wasimamizi ambao watawajaza nguvu ya kupigana hawa wachezaji ili wajitume zaidi na kutamani kufika mbali.

Kuna wakati huwa naona aibu kumshuhudia Victor Wanyama, siyo kwamba sipendezwi na yeye kuwepo kwenye Ligi Kuu England, ila ni kwa sababu sijawahi kushuhudia Mtanzania kwenye Ligi hii ya England.

Uwepo wa Victor Wanyama aliyetoka kwenye nchi ambayo ipo ukanda wetu unatosha kutupa imani kuwa tunaweza kufika kwenye ligi kuu ya England; inawezekana Salah ukawa mfano unaotoka mbali sana, lakini mfano wa Wanyama unatosha kutuonyesha na sisi tuna uwezo wa kufika sehemu hii inayoangaliwa na watu wengi duniani kila mwisho wa juma.

Cha muhimu wachezaji wanatakiwa kupigana kwa kufanya mazoezi kwa kujituma, maarifa huku vipaji vyao wakivikabidhi kwa wasimamizi maalumu wa wachezaji na wasimamizi ambao watawaongoza wachezaji kipi wafanye chenye afya cha kutunza vipaji vyao na kipi kisicho na afya kinachoweza kuangamiza vipaji vyao.

Wasimamizi hawa wa wachezaji wanatakiwa wawe na mawakala ambao wana maono makubwa yatakayowasaidia wachezaji kufika mbali.

Inatakiwa kuwa hivyo ili na sisi huku England tushuhudie Mtanzania ambaye atakuwa anaimbwa kwenye majukwaa ya timu anayocheza, ni furaha sana unapomwona Mtanzania mwezako akitukuzwa sana kwenye ardhi ya mgeni.

Inapendeza, lakini najaribu kuwaza ikija kutokea kama anayofanyiwa Salah, Tanzania nayo itakuwa mbali kisoka.