Mastaa wanaopiga pesa nje ya sanaa

Muktasari:
- Kutokana na kazi zao za sanaa kuonekana kubakia palepale licha ya kupanda kwa hatua nyingi takriban miaka saba iliyopita, mastaa wengi wa fani hizi wameamua kupiga mzigo kwa kujiingizia pesa nje ya sanaa, bila ya kujali ukubwa wa majina yao wala kuangalia ni nani atawacheka au atajadiliwa vipi.
SOKO la filamu na muziki limeshuka? Hapana, sio kirahisi hivyo. Bado lipo japo linasuasua. Wasanii bado wanapiga kazi ingawa si kama mwanzo sanaa hizi zilivyoanza kuinukia.
Kutokana na kazi zao za sanaa kuonekana kubakia palepale licha ya kupanda kwa hatua nyingi takriban miaka saba iliyopita, mastaa wengi wa fani hizi wameamua kupiga mzigo kwa kujiingizia pesa nje ya sanaa, bila ya kujali ukubwa wa majina yao wala kuangalia ni nani atawacheka au atajadiliwa vipi. Pia wengi wamekuwa wakijuta kwa nini hawakuanza mapema kwani ni wazi sasa hivi wangekuwa mbali sana kimaisha.
Mwanaspoti linakulea baadhi ya mastaa wanaopiga pesa nje ya sanaa.
JACQUELINE WOLPER “Fundi Cherehani)
Hivi karibuni staa huyu wa filamu nchini, alitambua thamani ya kujituma na kujibidiisha hivyo kuamua kufanya jambo.
Hivi sasa Wolper anamiliki ofisi za kushonea nguo mbalimbali jambo ambalo linamwingizia peza na kumpa heshima.
“Niliona kabisa umuhimu wa kukaa chini na kukiri ni kitu gani naweza kufanya mbali na uigizaji wangu,ambacho kikaniingizia pesa na watu wakakifurahia, kwani nilijishutukia kwa kutambua nina kipaji kingine, kwa nini nisijaribu kufungua sehemu ya kushona nguo mbalimbali za kinamama na hata wababa?
Nimejaribu na ninaona wazi nimeweza na napiga pesa ya maana hadi najutia kwa nini nimechelewa kufanya hivi,” anasema Wolper ambaye ofisi yake ipo Kinondoni Mkwajuni.
MUDA WAKE
Anasema huamka asubuhi saa mbili na kujiandaa kwenda kwenye biashara zake. Pia anapendelea kuwepo kazini saa nne kutokana na muda huo ndio watu wengi hufika ofisini kwake kuonana naye japo kuwa kuna mafundi wa kumsaidia.
JUX
Msanii wa Bongo Fleva anayetamba na wimbo wa ‘Fimbo’, mbali na kupiga pesa kupitia muziki, pia anamiliki duka kubwa hapa Bongo.
Duka lake hilo lililopo Sinza Kamanyola na Kinondoni Studio lina bidhaa kali kama za nguo za kiume, mabegi, ribbon, sneakers, kofia na makava ya simu.
“Ukitegemea muziki tu, itakula kwako, maana sasa hivi soko limekuwa la kusuasua sana, hivyo mtu unaamua kujiongeza kutafuta pesa nje ya muziki,” alisema jux na kuongeza kuwa awali duka lake lilikuwa maeneo ya Sinza Lego, ila lilibomolewa kutokana na mwenyenyumba wake kushindwa kesi.
MUDA WAKE
Anasema hana muda maalumu wa kwenda kwenye biashara zake kwani ana wafanyakazi anaowaamini na hivyo kutokana na ubize wa kazi zingine huwa anapitia kwa wiki mara tatu au moja.
AUNTY EZEKIEL
Msanii wa Bongo Muvi. Anasema alianza mapema kujiongeza kwa kupiga pesa nje ya sanaa kwani kuna njia nyingi za kujikwamua kimaisha kuliko kusubiri malipo ya filamu na kukiri alishawahi kufungua baa mara mbili na kufunga.
Hata hivyo, Aunty anasema, hakukata tamaa kwani aliamini anaweza na sasa amebuni mbinu mpya ya kuuza sabuni za kuogea zinazoondoa vipele alizozipa jina la Murua, ambazo mpaka sasa zinamsogeza sana kimaisha, pia hivi karibuni amefungua tena bar inayojulikana kwa jina la Cookie Drink. “Nadhani nyuma tulikuwa tunabweteka sana, tulitegemea sana kuletewa na kupewa, kitu ambacho tulikuwa tukikosea sana kwa sababu mimi nimejaribu na nimeweza na ninajilaumu nilichelewa wapi muda wote,” anasema Aunty ambaye anamiliki bar yake hiyo iliyoko Kinondoni Koma Koma.
MUDA WAKE
Anasema anafika kwenye biashara yake kuanzia saa kumi na kufunga saa nane au tisa usiku.
IRINE UWOYA
Msanii maarufu wa wa Bongo Muvi ambaye ametesa kwenye gemu kwa muda mrefu.
Anasema kipindi cha nyuma jina lake lilikuwa kubwa sana lakini akajisahau kabisa kulitumia kufanya mambo muhimu ya kumwingizia pesa, lakini sasa hivi naye ameamka na kuamua kuwa mjasiriamali kwa kufungua maduka mawili ya kuuza nguo na ushonaji kitu ambacho hawezi kulala njaa tofauti na mwanzo alivyokuwa akisubiria pato la filamu au kupewa na mtu.
“Hakuna hela nzuri kama ya kwako mwenyewe, kwanza inakupa amani sana na hata wakati wa kuitumia unajua unatumia kitu ambacho umekitolea jasho, pia ni heshima kubwa kwa mwanamke kutafuta hela mwenyewe, kusubiri za mtu ni kazi sana,” anasema Uwoya ambaye duka lake la nguo lipo Msasani jijini Dar es Salaam.
MUDA WAKE
Anasema muda mwingi huwa kwenye biashara zake kuanzia saa nne asubuhi hadi 12 jioni.
KAJALA MASANJA
Msanii wa Bongo Muvi. Kutokana na maisha yake wengi walidhani staa huyu wa filamu nchini asingeweza kabisa kufikiria kuhusu kufanya biashara yoyote ya nje ya sanaa.
Hata hivyo, kama hujui tu, Kajala ameamua kujiingiza kwenye ujasiria mali wa kuuza sabuni za kufulia na kufanya usafi majumbani.
“Kwa sasa hakuna maisha bila kujishughulisha, nilikaa na kuamua sasa ni kipindi cha kujituma zaidi bila kusubiri kuletewa na mtu yeyote na ninashukuru sasa hivi nauza sabuni ambayo natengeneza mwenyewe kwa mikono yangu na mambo yanaenda sawa kabisa,” anasema Kajala.
Kuhusu biashara ya usafi anasema, huwa biashara ndiyo inamfuata mteja nyumbani na huwa anatoa namba za simu na kuacha vipeperushi, halafu mteja anampigia kwa ajili ya kwenda kumfanyia kazi.
MUDA WAKE
Anasema hana muda maalumu wa kufanya kazi zake, kwani siku akiamka anakuwa makini kikazi kwani ofisi yake iko mikononi mwake.
SHILOLE
Msanii wa Bongo Fleva. Yeye mbali na kuachia nyimbo mara kwa mara na kupanda stejini kunakomwingizia pesa, nje ya kazi hiyo anamiliki mgahawa wa chakula.
MUDA WAKE.
Anasema mara nyingi anakuwaga muda wa mchana katika biashara yake.