Simba hii mtapigwa nyingi

Muktasari:

Lakini sasa kama kuna kitu kitakachowapasua vichwa wapinzani wa Simba katika Ligi Kuu Bara ni aina ya mfumo aliotua nao kocha huyo, kwani iwapo timu pinzani itazembea kidogo tu mbele ya vijana wa kocha huyo, basi lazima ipigwe nyingi.

KAMA kuna jambo litakalowafurahisha wanachama na mashabiki wa Simba, basi ni taarifa kwamba mabosi wao wameamua kumpa mkataba wa muda mrefu Kocha Mkuu Mpya, Mfaransa Pierre Lechantre aliyetambulishwa rasmi jana Ijumaa jijini Dar es Salaam.

Lakini sasa kama kuna kitu kitakachowapasua vichwa wapinzani wa Simba katika Ligi Kuu Bara ni aina ya mfumo aliotua nao kocha huyo, kwani iwapo timu pinzani itazembea kidogo tu mbele ya vijana wa kocha huyo, basi lazima ipigwe nyingi.

Timu pinzani zinaweza kupigwa nyingi pengine kuliko kichapo walichopewa Singida United juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa, walipokung’utwa mabao 4-0 huku Mfaransa huyo akishuhudia vijana wake wakipiga mpira mwingi wa kiufundi.

Kocha Lechantre aliyetua mapema wiki hii huku dili lake la kuifundisha Simba likisainiwa mchana wa jana, ametamka kwamba baada ya kukiona kikosi hicho anataka kufanya kazi moja tu ya kuibadilisha Simba kuwa isiyofungika kirahisi huku yenyewe ikitupia wavuni kadiri inavyotaka.

Alisema falsafa yake ni kucheza soka la kushambulia na la kuvutia, kitu ambacho kwa aina ya wachezaji alionao Simba anaamini itamrahisishia kazi, huku akiainisha kuwa yeye hupenda kutumia mfumo wa 3-5-2 ulioizamisha Singida juzi.

Mfaransa huyo wa pili kuifundisha Simba akitanguliwa na babu Patrick Liewig, alisema licha ya kwamba hii inakuwa mara yake ya kwanza kufundisha Tanzania, lakini amekuja kuungana na Bilionea Mohamed Dewji ‘MO’ katika mradi mpya wa kisasa wa klabu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu.

Alisema amekiona kikosi cha Simba na kumsifia msaidizi wake Masudi Djuma kuwa amefanya kazi nzuri, lakini amegundua dosari chache ambazo ndizo atakazoanza nazo kwa kuipunguzia makosa yanayoweza kusababisha kupoteza.

“Nimekuja kufanya kazi, nafurahi kuwa hapa, hii ni mara yangu ya kwanza kufika nchi hii, ingawa nimewahi kufika Uganda, nataka kufanya kazi hapa hicho ndicho ninachoweza kusema,” alisema Lechantre.

Mbinu zake

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu, Lechantre alisema anachotaka kuifanya Simba ni kuwa timu ngumu kufungika, lakini katika kikosi atakachokiongoza anataka kicheze soka la kushambulia na kuvutia akipanga kutumia mfumo wa 3-5-2.

Mfumo huo ndio uliotumia na Djuma tangu akichukue kikosi hicho na kutoa dozi kwa Ndanda FC mabao 2-0 na kisha juzi kuifumua Singida 4-0.

Msaidizi wake

Mwanaspoti limebaini Lechantre amesaini mkataba mmoja na msaidizi wake raia wa Tunisia, Mohamed Habib Aymen, atakayehusika na mazoezi ya viungo mwenye Stashahada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kocha ni nani?

Lechantre alizaliwa Aprili 2, 1950 na alikuwa straika aliyezicheze Paris FC, Stade de Reime, Olympique Marseille, FC Sochaux, Monaco na Lille kabla ya kustaafu Julai, 1989.