Simba SC, Yanga zatenga Sh4 bilioni kusajili nyota wapya

Thursday March 26 2020

 

By CHARLES ABEL

KABLA hata msimu wa 2019/2020 haujamalizika, vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga vimeanza harakati za kimyakimya za usajili ili kuimarisha vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao.

Klabu hizo zimewaweka katika rada zao baadhi ya wachezaji huku zikiwa na mpango wa kuwatema wengine ambao wameonekana kutokuwa na viwango vya kuridhisha katika vikosi vyao.

Kwa muda mrefu, masuala ya usajili kwa klabu za Yanga na Simba yamekuwa na matokeo ya tofauti ambapo kuna wakati zimekuwa zikifanya usajili unaoleta tija lakini zipo nyakati ambao mchakato wa usajili huwa shubiri pale wachezaji wanaposhindwa kutimiza kile kilichotegemewa ndani ya uwanja.

Kuna taswira ya wazi kwamba usajili wa dirisha kubwa utakaofanywa na klabu hizo mbili kongwe mara baada ya msimu huu kumalizika, utakuwa wa aina yake kutokana na mazingira halisi ya ubora na mahitaji ya vikosi vyao kwa sasa, bajeti na nguvu ya kiuchumi na gharama au thamani ya nyota zinaohitaji kuwasajili ili wazitumikie msimu ujao.

Vita ya fedha

Msimu uliopita Simba walitawala dirisha la usajili kutokana na nguvu kubwa ya kiuchumi waliyonayo ambayo iliwapa jeuri ya kusajili nyota wenye majina makubwa ambao ama walikuwa katika rada au walisafanya mazungumzo ya kujiunga na timu nyingine hasa Yanga.

Advertisement

Hata hivyo, mambo yamebadilika kwa sasa ambapo nguvu ya fedha ambayo Yanga wanayo kutokana na wadhamini wake (japo wametishia kujitoa) imeifanya iweke mikakati mizito ya kuhakikisha inanasa wachezaji bora na wa kiwango cha juu katika dirisha lijalo la usajili.

Usajili wa wachezaji kama Bernard Morrison, Ditram Nchimbi na Haruna Niyonzima ambao iliufanya katika dirisha dogo huku ikiwaacha kundi kubwa la wachezaji wake wa kigeni ambao ilikuwa tayari kuwavunjia mikataba ili wapishe ujio wa wapya, ni kiashirio tosha kuwa Yanga inaenda kivingine katika usajili wa dirisha kubwa mara baada ya msimu kumalizika.

Lakini bado Simba wameendelea kuwa na nguvu kubwa ya kifedha ambayo bado inawapa jeuri ya kutamba katika dirisha la usajili na kunasa wachezaji ambao wapo katika mpango wao.

Afrika bado sana

Pamoja na kuonekana ni klabu zenye nguvu ya kifedha na ambazo zitatamba katika dirisha la usajili, ni wazi kwamba Yanga na Simba bado hazina na hazitakuwa na uwezo wa kuwapata nyota wa daraja la juu barani Afrika ambao watakuwa chachu kwao kufanya vizuri katika mashindano ya klabu Afrika.

Ni jambo lililo wazi kwamba kwa bajeti ya klabu hizo mbili kubwa nchini, kuweza kushindana na klabu za Kaskazini mwa Bara la Afrika, Afrika Kusini na baadhi za DR Congo, ni vigumu kwa Simba na Yanga kuchomoza na kunasa wachezaji wa daraja la juu mbele ya timu hizo.

Kwa msimu unaoendelea, Bajeti ya Simba ni takribani Shilingi 6 bilioni na Yanga ni zaidi ya Shilingi 4 bilioni ambazo ndizo zimetumika kuendeshea klabu kwa kufanya usajili na kugharamia huduma nyingine kama vile kambi, posho, mishahara, bonasi, matibabu na kadhalika.

Kiwango hicho cha fedha za bajeti kinaweza vipi kuzifanya Simba na Yanga ziweze kushindanna na timu kama Al Ahly ambayo miezi miwili iliyopita ilimnunua nyota wa Senegal aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini Austria, Aliou Badji aliyenaswa kwa ada ya uhamisho, kiasi cha Euro 2.2 milioni ambayo ni sawa na Shilingi 5.5 bilioni za Kitanzania?

Kiasi kikubwa cha fedha ambacho Yanga na Simba zinaweza kutoa kumsajili mchezaji huwa hakizidi Sh 200 milioni ambacho kwa klabu kama TP Mazembe, Wydad Casablanca, Raja Casablanca, Al Ahly, RS Berkane, Esperance, Mamelodi Sundowns na nyinginezo za Kaskazini mwa Afrika, hicho ni kiasi kidogo na cha kawaida.

Wazawa hawa kuoga noti

Pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wazawa wanaoshiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ni wazi kwamba idadi ndogo ndio ambao wataweza kuchota fedha za usajili kutoka katika timu hizo.

Taarifa juu ya ripoti za mahitaji ambayo makocha wa Simba na Yanga wamewasilisha kwa uongozi kama mapendekezo ya usajili kwa wachezaji wa ndani, zimeonyesha kuwa hazitofauti sana na wachezaji wanaotakiwa na upande mmoja ndio hasa wameonekana kuvutia upande mwingine jambo ambalo linaweza kuchochea vita ya kuwania saini zao mara baada ya msimu kumalizika.

Timu zote mbili zimeonekana kuwa na uhitaji wa beki wa kati, beki wa pembeni, kiungo mshambuliaji, winga na mshambuliaji wa kati.

Kutokana na kiwango bora walichokionyesha katika timu zao msimu huu, wachezaji ambao wanatajwa kuwindwa na timu zote mbili ni Bakari Mwamnyeto, Lucas Kikoti, Reliant Lusajo na Sixtus Sabilo.

Usajili unaweza kuwa na faida kwa timu hizo ikiwa utaendana na mahitaji yalivyoainishwa na benchi la ufundi, kinyume chake utazaa timu matatizo tu.