Baghdad mtoto wa maskini aliyebeba Algeria

Saturday April 11 2020

 

ALGIERS ALGERIA. USIKATE tamaa, ukiona mambo hayaendi na maisha yanazidi kuwa magumu, jua ndio unakaribia kufika kwenye kilele cha mafanikio yako. Jua Mungu anakwenda kufungua milango ya utajiri wako ambao aliifunga kwa muda ili kukupima imani yako.

Kama kweli wewe ni mfuatiliaji wa soka basi itakuwa umewahi kumshuhudia au kumsikia Baghdad Bounedjah, miongoni mwa nyota waliotajwa sana kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) kule nchini Misri mwaka 2019.

Alichofanya huko ni kuiwezesha nchi yake kutwaa taji hilo kubwa Africa mbele ya wenyeji Misri. Hata hivyo, kinachovutia zaidi, ni akiwa anafikisha miaka 20 alikuwa bado anacheza ligi za mchangani lakini sasa ndiye shujaa wa Algeria.

Baghdad ni nani?

Alizaliwa Novemba 24, mwaka 1991, katika Mji wa Oran, unatajwa ni wa pili kwa kuchangia uchumi wa nchi hiyo.

Alikulia hapo akiwa hana mbele wala nyuma huku akiamini ipo siku atatoboa kwenye soka licha ya umri wake kuzidi kwenda.

Advertisement

Wakati anakua, ili kutimiza mahitaji yake mengine muhimu, ilimpidi ajishughulishe na kazi ndogo ndogo ajipatie kipato kwani timu aliyokuwa akiichezea utotoni haikumpa chochote kama malipo. Maisha yake yalikuwa magumu lakini katu hakuonyesha kukata tamaa.

Safari ya maisha

Haikuwa rahisi hata kidogo kwake kuja kujulikana na wapenda soka, kwani mpaka anafikisha umri wa miaka, 20, hakuwa na mbele wala la nyuma. Katika umri huo, nyota wengi Algeria walikuwa na timu Ulaya ama wakicheza ngazi za juu nchini kwao, lakini yeye alikuwa akicheza ligi za mchangani ambazo hazikuwa zinatazamwa kwa wingi.

Maisha yake ya soka yalianzia kwenye klabu ya RCG Oran na alicheza kuanzia timu ya watoto hadi akapandishwa timu ya wakubwa mwaka 2009 na alicheza kwa misimu miwili tu na baadae akajiunga na USM El Harrach ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Kuu nchini humo.

Hata hivyo, safari yake ya kutoka RCG Oran kwenda USM El Harrach haikuwa ya hivi hivi.

Mwaka 2011, kwenye moja ya mechi akiichezea timu yake ya RCG Oran, alibahatika kuonwa na kocha wa USM El Harrach, Boualem Charef, baada ya kumshuhudia Baghdad akicheza na kugundua mchezaji huyo alibarikiwa kipaji cha hali ya juu sana ambacho kimenogeshwa na juhudi alizonazo kuanzia kwenye kujitolea linapokuja suala la kukaba bila kujali kuwa yeye ni straika. Pia umakini ambao anao pale anapokuwa mbele ya goli, hali iliyosababisha kocha huyo kumchukua na kumpeleka kwenye majaribio USM El Harrach.

Baghdad alifaulu na kusajiliwa na aliweka rekodi ya kupata mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa, hii ilikuwa ni mwaka 2011.

Usajili wake ulionekana kupingwa sana na mashabiki wa timu hiyo kwa kile kilicho elezwa mchezaji huyo hakuwa anajua chochote kuhusu Ligi Kuu nchini Algeria, kwani alitokea Ligi za madaraja ya chini, lakini kocha wake alimtuliza Bagdad na kumwaminisha yeye ni bora sana.

Baghdad aliwanyamazisha mashabiki waliokuwa wanambeza kwenye mechi yake ya kwanza tu ya Ligi Kuu, pilipocheza USM El Harrach dhidi ya MC Oran na alifunga bao dakika ya 78. Kuanzia hapo mashabiki wakaanza kujenga imani kwenye miguu yake.

Juhudi zake ambazo alitoka nazo tangu anacheza mchangani kamwe hakuziacha, aliendelea kujituma kila siku kwa kuwa aliamini bado kuna sehemu anahitaji kufika.

Waswahili wanasema, mwenye jitihada hupata, miezi michache tu baada ya kucheza klabuni hapo kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Algeria naye pia aligundua kipaji cha hali ya juu kwa mchezaji huyo na kumwita kwenye kikosi chake baada ya straika Rafik Djebbour kuumia, kikosi hiki kilikuwa kinakwenda kucheza mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mwaka 2012.

Hapo nako kulizua mjadala mkubwa kwani mchezaji huyu hakuwa anajulikana kiasi cha kuitwa timu ya Taifa.

Hilo halikumzuia kuendelea kusimamia kwenye kile anacho kiamini na mwezi Novemba ndani ya mwaka huo huo wa 2011 akajumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa cha Algeria chini ya miaka 23, ambacho kilikuwa kinakwenda kushiriki michuano ya AFCON kwa vijana nchini Morocco.

Etoile du Sahel

Kiwango alichoonesha kwenye klabu yake na hata kwenye timu ya Taifa kulimfanya ale shavu la maana kwa miamba ya soka kule nchini Tunisia, Etoile du Sahel baada ya kuvutiwa naye na kumsajili Septemba mwaka 2013. Katika msimu wake wa kwanza tu ndani ya kikosi hicho alifanikiwa kufunga mabao 14 na kumaliza ligi akiwa mfungaji bora. Maisha ya hapa yalizidi kumwendea vizuri na kufanikiwa kupata Makombe mawili ya Tunisia Cup mwaka 2014 na 2015 pamoja na kombe moja la Shirikisho Barani Afrika mwaka 2015.

Mwaka 2015 ukawa ni mwaka wa mafanikio zaidi kwake baada ya kiwango cha ajabu alichoonesha kwenye michuano ya Caf, alipelekea klabu nyingi barani Ulaya kuhitaji saini yake lakini badala yake akaamua kuchagua ofa nono iliyotolea na matajiri wa mafuta kutoka nchi ya Qatar na kujiunga na Al Sadd na ndiye mchezaji kinara mpaka sasa.

Timu ya Taifa

Hapa ndipo watu wengi wamelijulia jina lake, tena hasa kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2019 iliyochezwa Misri, katika wa fainali uliopigwa kati yao na Misri yeye ndiye aliyefunga bao pekee la Algeria na kunyakua ubingwa. Pia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee ambaye hachezi Ulaya kujumuishwa kwenye kikosi cha Timu Taifa ya Algeria.

Kwa mujibu wa wachezaji wenzake, wakiwa vyumbani hadi kwenye gari baada ya mchezo huo wa fainali kumalizika Bagdad alikuwa analia tu na walipomuuliza wala hakuwaambia maneno mengi alisema “Hatimaye ndoto ya masikini imetimia.”

Maisha binafsi

Kwa kuwa alichelewa kwenye maisha mpaka sasa jamaa hana mtoto wala mchumba wake hajulikani, pia ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola 5 milioni.