HAYA TETEMA: Chama la Peter Crouch halikabi, linakabwa tu

Sunday April 21 2019

 

LONDON, ENGLAND . MWANASOKA mwenye kimo chake aliyewahi kutokea kwenye Ligi Kuu England, Peter Crouch amesema ameandika na kufuta mara nyingi kuhusu wachezaji sahihi wanaopaswa kuingia kwenye kikosi chake bora cha ligi msimu huu.

Staa huyo alisema kwa sababu asili ya nafasi yake ndani ya uwanja ilikuwa ushambuliaji basi chama lake alilotaka lina wachezaji wengi wenye akili ya kushambulia tu, ndio maana kikosi chake hicho ukikumbana nacho utapigwa mabao hadi unachakaa unaambiwa.

Hii hapa timu ya msimu huu ya fowadi huyo wa zamani wa Liverpool huku akiwaomba radhi wale wachezaji wengine ambao, hawakupata nafasi kwenye timu yake.

KIPA

Alisson Becker, Liverpool

Crouch amedai kwamba timu yake hiyo ya zamani ilikuwa ikiteseka sana kupata kipa wa kiwango cha dunia tangu alipoondoka Pepe Reina. Lakini, msimu huu mambo yamekuwa tofauti baada ya kumnasa Alisson, ambaye amekuja kuleta mabadiliko makubwa kwenye goli la Liverpool. Crouch alidai kuwa anawapenda David de Gea na Ederson, lakini mbele ya kipa wa mpira Alisson hao wengine benchi linawahusu tu.

Advertisement

MABEKI

Aaron Wan-Bissaka, Crystal Palace

Kwenye kikosi hicho cha msimu cha Crouch, amemchagua Aaron Wan-Bissaka kuwa beki wake wa kulia hasa baada ya kuonyesha kiwango kikubwa sana msimu huu. Umri wa beki huyo ni miaka 21 tu, lakini amekuwa akicheza mpira mkubwa sana ndani ya uwanja akiwa chaguo bora kabisa kwa beki ya kulia kwa msimu huu kutokana na uwezo wake wa kushambulia pia.

Virgil van Dijk, Liverpool

Ukuta wa Liverpool kwa msimu huu umekuwa imara zaidi kutokana na kuwapo kwa beki wa kati, Virgil van Dijk. Kiwango cha Mdachi huyo ni matata na ndio maana anapata nafasi ya moja kwa moja katika kikosi cha Crouch cha msimu huu kwenye Ligi Kuu England. Van Dijk si mchezaji wa kufanya makosa mara kwa mara anapokuwa kwenye majukumu yake uwanjani.

Aymeric Laporte, Manchester City

Wakati mwingine utakapokitazama kikosi cha Manchester City chini ya kocha Pep Guardiola unaweza kufikiria kwamba, kinacheza bila ya kuwa na mabeki kutokana na wachezaji wake wengi kuwa na uwezo wa kuuchezea mpira kama washambuliaji au viungo. Kwenye kikosi hicho cha Etihad kuna mtu anaitwa Aymeric Laporte, ambaye ni kiboko kwa kukaba na hivyo kumfanya Crouch amwingize kwenye kikosi chake.

Andrew Robertson, Liverpool

Crouch amedai kwamba amemchagua Andrew Robertson kucheza beki ya kushoto kwenye kikosi chake kwa sababu tu anavutiwa kwa namna anavyocheza ukiweka kando uwezo wake wa ndani ya uwanja. Andew Robertson amekuwa moto pia akicheza beki ya kushambulia na jambo hilo limekuwa likiwafanya Liverpool kila wakati kuwa kwenye eneo la wapinzani wao na matokeo yake kufunga mabao.

VIUNGO

Eden Hazard, Chelsea

Kwenye kikosi cha Crouch, sehemu ya kiungo ya timu yake, mmoja wanaopatikana hapo ni staa wa Chelsea, Eden Hazard. Kwenye safu hiyo ya viungo watatu, Hazard atacheza upande wa kushoto, eneo ambalo amekuwa akimudu vyema anapokuwa kwenye majukumu yake ya kila siku huko kwennye kikosi cha Stamford Bridge. Kwa sababu Crouch amekuwa na mtazamo wa kuwa na timu inayoshambulia mwanzo mwisho, Hazard amepata nafasi. Hakuna kukaba.

Christian Eriksen, Tottenham

Umekuwa mwaka mgumu kwa Tottenham Hotspur kutokana na majeruhi ya mara kwa mara kwa wachezaji wake muhimu, Harry Kane na Dele Alli. Hata hivyo, Spurs hawajawahi kuwa na masikitiko mengi kwa sababu kwenye timu yao kuna fundi wa mpira anaitwa Christian Eriksen. Kiwango cha mchezaji huyo ni matata kabisa na ndiyo maana timu hiyo imekuwa na uhakika wa kumaliza ligi ndani ya Top Four. Eriksen ameingia kwenye kikosi cha Crouch akishikilia kiungo ya kati.

Raheem Sterling, Manchester City

Raheem Sterling yupo kwenye ubora wake msimu huu na huenda akashinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu England. Huduma yake moto imeifanya Manchester City kuwa kwennye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao wa ligi msimu huu na kutokana na hilo Crouch hakusita kumwingiza kwenye kikosi chake akikamilisha safu ya viungo watatu, ambapo Mwingereza huyo atacheza kwenye upande wa kulia. Ubora wa Sterling msimu huu hakuna kocha au yeyote atakayepanga kikosi chake kisha akaliweka kando jina lake.

WASHAMBULIAJI

Sadio Mane, Liverpool

Kikosi cha Crouch ukikutana nacho ni kushambuliwa mwanzo mwisho, hawataki mambo ya kukaba wao na ndio maana katika timu hiyo wanapatikana mastaa moto kabisa akiwamo Sadio Mane. Akitumia fomesheni ya 4-3-3, Mane ni mmoja wa washambuliaji watatu wanaounda kwenye kikosi hicho cha Crouch akishambulia kutokea upande wa kushoto.

Sergio Aguero, Manchester City

Kwa misimu yote aliyokuwa kwenye Ligi Kuu England, Sergio Aguero amekuwa akionyesha ubora wake kwenye kufunga mabao kama anavyofanya msimu huu akiing’arisha Manchester City kwenye mbio za kufukuzia kutetea taji hilo. Crouch hakuona shida katika kumjumuisha fowadi huyo kwenye kikosi chake cha msimu huu kwenye Ligi Kuu England akisimama kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati.

Son Heung-min, Tottenham

Asipokuwapo Harry Kane huko kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur basi majukumu ya kufunga yanabebwa vyema kabisa na staa wa Kikorea, Son Heung-min. Amekuwa akicheza kwa kiwango bora sana msimu huu akisaidia timu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwasukuma nje Manchester City. Kwenye kikosi hiki cha Crouch, Son atashambulia kutokea kulia katika safu ya washambuliaji watatu ambao ukikabiliana nao, yeyote anaweza kukufunga.

BENCHI

Kwenye kikosi cha Crouch, wachezaji watakaoanzia benchi ni pamoja na kipa Ederson, beki Trent Alexander-Arnold, kiungo Bernardo Silva, David Silva na washambuliaji Mohamed Salah, Harry Kane na Pierre Emerick-Aubameyang.