Pep ana bonge la ofa mezani

Tuesday May 21 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND

MAISHA yanataka nini tena. Pep Guardiola mambo yananyooka na Man City kwa sasa imepanga kufanya chochote kinachowezekana kuhakikisha anaendelea kubaki kwa muda mrefu hata kwa kutumia pesa. Man City imepanga kumbakiza Guardiola kwa miaka mitano zaidi huko Etihad.

Na kama atakubali basi Guardiola atavuta Pauni 100 milioni na mshahara wake wa mwaka ukiongezeka kutoka Pauni 15 milioni hadi Pauni 20 milioni.

Kwa sasa Guardiola bado amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake. Licha ya kuwapo kwa taarifa za kwamba huenda timu hiyo ikakumbana na adhabu ya kufungiwa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, kocha huyo Mhispaniola ameweka wazi amepanga kuwa kwenye timu hiyo hadi mwisho wa mkataba wake.

Kulikuwa na taarifa kwamba anafukuziwa na Juventus baada ya kumfuta kazi Kocha Max Allegri, lakini Guardiola alisema: “Nitabaki hapa kwa misimu miwili zaidi kama watanihitaji. Natosheka na kufanya kazi hapa, hivyo siendi kokote.”

Mahali pekee ambapo Guardiola alikaa kwa muda mrefu ni Barcelona alikodumu kwa miaka minne kabla ya kwenda kuchukua kazi ya kuinoa Bayern Munich miaka mitatu.

Advertisement

Advertisement