Kinachokwamisha dili la Gyokeres Arsenal ni hiki

Muktasari:
- Inaelezwa mazungumzo ya Arsenal kuhusu kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden yamekwama kutokana na kutokubaliana juu ya ada ya uhamisho.
LONDON, ENGLAND: SIKU chache baada ya wawakilishi wa Arsenal kuondoka, Ureno bila ya kufikia makubaliano na mabosi wa Sporting Lisbon juu ya mauziano ya Viktor Gyokeres, tovuti ya Independent imefichua ukweli juu ya nini kulichotokea katika mazungumzo hayo.
Inaelezwa mazungumzo ya Arsenal kuhusu kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden yamekwama kutokana na kutokubaliana juu ya ada ya uhamisho.
Arsenal iliweka mezani ofa ya Euro 65 milioni kama ada ya uhamisho lakini ikaweka pia nyongeza ya Euro 15 milioni ambayo itailipa kutokana na mafanikio ya mchezaji kama idadi ya mechi fulani, mabao na mataji.
Kwa ujumla Arsenal iliiahidi Sporting kuwa ipo tayari kulipa Euro 80 milioni kama ada ya uhamisho lakini ofa hiyo ilikataliwa.
Sporting imeshikilia msimamo wao inataka kulipwa Euro 70 milioni moja kwa moja kama ada ya uhamisho kisha Euro 10 milioni zinazobakia ndio ilipwe kwa mafungu mafungu kwa kuzingatia kiwango cha mchezaji kama baada ya kucheza mechi 50 italipwa Pauni 5 milioni au baada ya kufunga idadi fulani ya mabao itaongeza kiasi fulani.
Baada ya majadiliano na kuona Sporting haitaki kupunguza bei, wawakilishi wa Arsenal ndio wakaamua kuondoka na kurudi England.
Lengo la kurudi England inadaiwa ni kujadili upya na ikiwezekana iwasilishe ofa nyingine na kuona ikiwa Sporting itakubali au laa.
Katika dirisha hili Arsenal imekuwa ikikumbana sana na hali kama hizi, kwani mpango wao wa kumsajili Benjamin Sesko wa RB Leipzig, pia ulikwama kutokana na Euro 10 milioni tu.
Hata hivyo, jambo zuri katika dili hili la Gyokeres ni mchezaji mwenyewe anatamani kuondoka na ameshawachagua wao licha ya timu nyingi kumhitaji.
Rais wa Sporting, Frederico Varandas, ameripotiwa kukerwa na jinsi jambo hili linaenda akiwalaumu wawakilishi wa staa huyo kuwa ndio wamechangia hali yote hii.