Man United wao ni Mbeumo tu

Muktasari:
- Man United inajiamini itakamilisha dili hilo na Brentford kwa ajili ya mchezaji Mbeumo, licha ya ofa zao mbili kugomewa. Brentford iligomea ofa ya Man United ya kwanza ya Pauni 55 milioni kwa ajili ya fowadi huyo, kabla ya kugomea ya pili ya Pauni 62.5 milioni kama ambayo Man United ililipa huko Wolves kumnyakua staa wa Kibrazili, Matheus Cunha.
BRENTFORD, ENGLAND:MANCHESTER United bado ipo kwenye meza ya mazungumzo na Brentford kwa ajili ya ofa ya kumsajili mshambuliaji Bryan Mbeumo.
Man United inajiamini itakamilisha dili hilo na Brentford kwa ajili ya mchezaji Mbeumo, licha ya ofa zao mbili kugomewa. Brentford iligomea ofa ya Man United ya kwanza ya Pauni 55 milioni kwa ajili ya fowadi huyo, kabla ya kugomea ya pili ya Pauni 62.5 milioni kama ambayo Man United ililipa huko Wolves kumnyakua staa wa Kibrazili, Matheus Cunha.
Man United ilitarajiwa ingepanda dau hadi Pauni 65 milioni ili kufikia makubaliano na Brentford kwa ajili ya mchezaji Mbeumo, huku timu hizo zikiwa kwenye mazungumzo ya kukubaliano malipo yatakuwa kwa awamu ngapi.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim anataka Mbeumo anaswe kwenye timu haaka kabla ya timu hiyo haijaanza ziara ya mechi za pre-season huko Marekani, Julai 22, ambako itakwenda kucheza na West Ham United, Bournemouth na Everton.
Man United imeshawasajili Cunha na beki kinda Diego Leon, ina matumaini ya kumwongeza Mbeumo kwenye kikosi chao muda wowote kuanzia sasa ikiwa ni mwendelezo wa kocha Amorim katika kukijenga kikosi chake kije kivingine kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.
Straika mpya pia anahitajika huko Old Trafford na baada ya kumkosa Liam Delap, aliyejiunga Chelsea na Viktor Gyokeres anayekaribia kujiunga na Arsenal, kocha Amorim atalazimika kufanya machaguo mengine kwenye nafasi hiyo, huku mpango wa Namba 9 mpya ukimhusiska mkali wa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike. Man United imempa ofa pia staa wa zamani wa Chelsea, Dominic Calvert-Lewin, ambaye ni mchezaji huyo kwa sasa baada ya mkataba wake kumalizika huko Goodison Park.
Sambamba na hilo, kwenye dirisha hili Man United itapiga bei mastaa kibao ikiwamo Marcus Rashford, Antony, Alejandro Garnacho, Tyrell Malacia na Jadon Sancho.