Barca kuwabeba Neymar, Griezmann kwa pamoja

Saturday June 22 2019

 

BARCELONA, HISPANIA. BARCELONA wameamua kufanya kweli baada ya kuripotiwa kwamba wanataka kuwasajili masupastaa Neymar na Antoine Griezmann wote kwa pamoja kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.


Mabingwa hao wa La Liga wamekuwa wakihusishwa kuwa na mpango wa kusajili mastaa hao wawili baada ya Neymar kudaiwa yupo tayari kuachana na Paris Saint-Germain kama ilivyo kwa Griezmann anayetaka kuachana na Atletico Madrid.


Awali ilidaiwa kwamba Barca wanaweza kuweka nguvu yao kwenye usajili wa Neymar na kuwaachia PSG nafasi ya kumnasa Griezmann kwenda kuziba pengo la Mbrazili huyo huko Paris, lakini kumekuwa na taarifa mpya kwamba wababe hao wa Nou Camp wanataka kubeba masupastaa wote hao.


Taarifa zaidi zimedai kwamba Barcelona wanaweza kutumia kiasi cha Pauni 300 milioni kwa ajili ya kuwasajili mastaa hao ili kuja kupafanya Nou Camp kuwa mahali pagumu kwa timu pinzani zitakazoenda kucheza uwanjani hapo msimu ujao.


Hata hivyo, mpango wa kuwanasa wakali hao kwa pamoja kutategemea na namba ambavyo timu hiyo itakavyopiga bei mastaa wake Ivan Rakitic, Philippe Coutinho na Ousmane Dembele, ambao wote wamedaiwa kwamba wapo sokoni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Advertisement