Casemiro aambiwa staafu tu baba!

Muktasari:

  • Kilikuwa kiwango cha ovyo sana kutoka kwa Man United, lakini gwiji wa zamani wa Liverpool na Ligi Kuu England, Carragher amemwonyeshea kidole Casemiro na kudai shida ilianzia kwake.

MANCHESTER, ENGLAND: Jamie Carragher amemtolea uvivu Casemiro na kumwambia muda wake umekwisha, afungashe virago akampumzike baada ya kucheza ovyo kwenye mechi iliyowashuhudia Manchester United wakikubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England usiku wa juzi Jumatatu.

Kilikuwa kiwango cha ovyo sana kutoka kwa Man United, lakini gwiji wa zamani wa Liverpool na Ligi Kuu England, Carragher amemwonyeshea kidole Casemiro na kudai shida ilianzia kwake.

Hakika, Casemiro atakuwa na usiku wa kumbukumbu mbaya kwenye mechi hiyo baada ya kulambwa chenga na Michael Olise wakati anakwenda kufunga bao la kwanza, huku Mbrazili huyo alibaki akigalagala ardhini.

Kwa jumla, Casemiro alipitwa mara nane katika mechi hiyo, kitu ambacho kinaweka rekodi kwa mchezaji wa Ligi Kuu England kupitwa mara nyingi kwenye mchezo mmoja.

Baada ya mechi hiyo, Carragher alisema sasa umefika wakati wa Casemiro kukubali yaishe na kuachana na soka, akisema kitu ambacho kiungo huyo anapaswa kufanya kwa sasa ni kuhamia tu kwenye ligi ya Marekani (MLS) au Saudi Pro League huko Saudi Arabia, kwa sababu amechoka.

Carragher alisema: “Nilisema wakati wa mapumziko, Ten Hag anapaswa kumtoa Casemiro. Najua alikuwa na watoto wadogo kwenye benchi, lakini nadhani Casemiro, amekuwa ovyo sana, alipaswa afahamu yeye ni mchezaji mwenye uzoefu na ajue tu, amebakiza mechi tatu za kucheza kwenye ushindani mkubwa. Mbili za ligi na moja ya fainali ya Kombe la FA.

“Baada ya hapo, anapaswa tu kujua, anatakiwa kwenda MLS au Saudia. Niko siriazi. Amezeeka, watu wanayemzunguka, wanapaswa kumwaambia aachane na soka. Aachane na soka kabla ya soka halijamwaacha.”

Casemiro alikuwa moja ya usajili wa kwanza wa kocha Erik ten Hag kwenye kibarua chake Man United na alimnasa kwa uhamisho wa Pauni 70 milioni kutoka Real Madrid, mwaka 2022.

Ni mmoja kati ya wachezaji wa Man United wanaolipwa mshahara mkubwa, akiweka kibindoni, Pauni 350,000 kwa wiki. Alitarajia kuleta uzoefu wa kutosha kwenye kikosi cha Man United baada ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano na La Liga mara tatu alipokuwa na Los Blancos.

Na sasa, bila ya shaka, Man United chini ya bilionea Sir Jim Ratcliffe, aliyelenga kufanya mapinduzi makubwa kwenye kikosi hicho, atamfungulia mlango wa kutokea kiungo huyo mwishoni mwa msimu huu.