Zahera amfungukia Eymael

ALIYEKUWA kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema amechukizwa na kitendo cha kocha, Luc Eymael kuwatukana mashabiki wa Yanga kwani hilo sio jambo zuri katika maendeleo ya soka.

Zahera amesema kocha huyo alianza kufanya kosa kubwa kuzungumza hadharani kwamba hawataki tena wasaidizi wake na kama wakiendelea kuwa hapo basi ataondoka jambo ambalo amesema anapaswa kuzungumza na viongozi.

"Kosa la pili ambalo alilifanya ni jana, wazungu wengi Ulaya hawawezi kufundisha yaani anapata bahati ya kupata dola 6000 wakati Ulaya hawezi kupata hata dola 2000 halafu unakuja kutukana watu wa Afrika huku, hiki kimenikasirisha, nimeumia," amesema

Zahera alifunguka zaidi na kusema kocha huyo amewadharau watu wote, lakini anavyolalamika mara hana WiFi, gari na nyumba inaonyesha kabisa kwamba hata yeye kwao ni masikini.

"Inapaswa viongozi wa Afrika wawe makini katika kuangalia aina ya makocha, wakija Afrika wanapata pesa nyingi sana, unajua Congo kwanini walituachia timu? walikuwa wameridhika na vyeti vyetu kwa sababu na sisi tuna vyeti,".

"Mimi naangalia sana Ligi nikiwa huku Ulaya, kocha (Luc) analalamika marefa wanafanya vibaya lakini najua kabisa kwamba TFF (Shirikisho la Soka nchini) walifungia marefa wote ambao walifanya vibaya," amesema.

Zahera alidumu msimu mmoja na Yanga akiwa anapambana nayo ikiwa inatembeza bakuli, msimu huu mambo yalivyoanza kuwa safi kocha huyo alitimuliwa na nafasi yake ilichukuliwa na Eymael.

Hata hivyo, uongozi wa Yanga umetoa taarifa ya kumfuta kazi kocha huyo huku TFF nayo ikiadai kuchukua hatua kali zaidi juu ya Luc kwa kauli zake za kibaguzi.