Zahera:Hatukufuata mabao Mwanza

Muktasari:


Yanga imerejea jijini Dar es Salaam ikitokea jijini Mwanza walikoweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia.


Wakati Yanga ikirejea jijini Dar es Salaam kocha mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera amesema lango la kambi yai huko haikuwa kushinda kwa mabao mengi.
Zahera amesema katika mechi zao mbili dhidi ya Pamba na Toto zote za Mwanza ambazo hazipo ligi kuu haikuwa kuangalia ushindi kwa mabao mengi.
Zahera amesema alichokuwa anaangalia ni jinsi kuimarika kwa wachezaji wake katika kila mazoezi waliyokuwa wanafanya.
Kocha huyo Mkongomani akizungumzia mchezo dhidi ya Zesco United itakayopigwa Septemba 14 katika Uwanja wa Taifa, amesema hana wasiwasi kuelekea mechi hiyo baada ya kukamilisha kazi ya kutengeneza walichotaka wakifanye wakiwa kambini.
Amesema wakiwa kambini wamepata muda mzuri wa kufanyia kazi mapungufu ya wapinzani wao ikiwa ni pamoja na kuangalia mikanda mitatu ya mechi za wapinzani wao zikiwemo mechi mbili walizocheza dhidi ya Zanaco ya Zambia.
Ikiwa Mwanza Yanga ilicheza mchezo wa kwanza dhidi ya Pamba na kulazimisha sare ya bao 1-1 huku mechi ya mwisho wakishinda 3-0 dhidi ya Toto Africans.
Katika mechi hizo mbili na kambi yao hiyo Zahera ameonekana kuangalia sana kuegemea katika kuboresha safu yao ya ushambuliaji ambapo katika mabao manne waliyovuna ni matatu yakufungwa na mshambuliaji mmoja David Molinga huku moja likifungwa na Abdulaziz Makame.
Hata hivyo mabao hayo ya Molinga hayatakuwa na mchango wowote kuelekea mechi dhidi ya Zesco kufuatia Mkongomani huyo kutokuwa na vibali vya kucheza mechi zote mbili huku faida pekee ikiwa kwa Makame ambaye anaweza kupata nafasi endapo atapangwa.