Yusuf Mlipili aliamsha dude upya pale Msimbazi

Muktasari:

  • Msimu uliopita Mlipili alikuwa katika kikosi cha Simba kilichocheza mechi mbili za Kimataifa Kombe la Shirikisho Afrika na kuondolewa na Al Masry kwa sheria ya bao la ugenini.

BAO  alilofunga beki, Yusuf Mlipili kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi 2019 dhidi ya Azam FC, limemrudisha kwenye chati beki huyo wa Simba

Mlipili alisema mashindano ya Kombe la Mapinduzi huenda yakawa yamemsaidia kupata nafasi hata ya kuwa mchezaji wa akiba katika mechi za ligi ambazo katika mzunguko wa kwanza hajacheza hata mechi moja.

Anasema msimu uliopita wakati akijiunga na Simba akitokea Toto Africans hakuwa mchezaji mwenye kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara chini ya Kocha Joseph Omog lakini alipocheza Kombe la Mapinduzi na mabadiliko ya kocha yalimfanya kuingia katika kikosi cha kwanza.

“Nafikiri ni upepo mbaya tu umepita kwangu na changamoto ambayo nimekutana nayo ambayo natakiwa kuikabili ili niweze kuishinda na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kama ilivyokuwa msimu uliopita wakati nafika hapa Simba,” alisema.

“Nimetumika katika mechi nyingi za Kombe la Mapinduzi naimani Kocha Aussems huenda kuna akawa amekiona kwangu na akaniamini kunipa nafasi ya kucheza katika mechi za ligi na nyingine za ushindani kama Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Changamoto nimekutana nazo lazima nikubali nashindania na wachezaji wenye uzoefu na majina makubwa kama Pascal Wawa, Juuko Murshid na Erasto Nyoni nina kazi kubwa ya kuifanya nikiwa mazoezi na kwenye mechi ili kumshawishi kocha na kupata nafasi dhidi yao,” alisema Mlipili

Msimu uliopita Mlipili alikuwa katika kikosi cha Simba kilichocheza mechi mbili za Kimataifa Kombe la Shirikisho Afrika na kuondolewa na Al Masry kwa sheria ya bao la ugenini.