Lawi rasmi ni Mnyama, mkanda mzima upo hivi!

Muktasari:

  • Lawi ambaye anamudu kucheza beki wa kati ataungana na Che Malone kucheza eneo hilo baada ya Henock Inonga na Keneddy Juma kutajwa kuondoka ndani ya kikosi cha Simba mwishoni mwa msimu.

DILI LIMEKAMILIKA: Ndivyo ilivyo baada ya klabu ya Simba kumsajili beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi kwa  mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Lawi ambaye anamudu kucheza beki wa kati ataungana na Che Malone kucheza eneo hilo baada ya Henock Inonga na Keneddy Juma kutajwa kuondoka ndani ya kikosi cha Simba mwishoni mwa msimu.

Mwanaspoti limepata Habari kutoka ndani ya Simba kuwa beki huyo alisafiri kutoka Tanga jana na kutua Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini mkataba na timu hiyo na tayari ameshaondoka kwenda kujiunga na timu yake  kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi zilizobaki.

“Tumemaliza na Lawi wa Coastal Union baada ya makubaliano ya pande zote mbili kufikia makubaliano, Ni beki mzuri hatuna shaka na uwezo wake, kwani hata kocha Juma Mgunda ameridhishwa naye kwa sababu ni mchezaji ambaye amepita chini yake amesisitiza asajiliwe.” Kimesema chanzo hicho na kuongeza;

“Lawi tayari kasaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba msimu ujao tunaamini atafanya kazi nzuri kama ilivyo sasa ndani ya kikosi cha Coastal Union."

Zoezi la usajili wa beki huyo limefanyika jijini Dar es Salaam, baada ya mchezaji huyo kuondolewa kambini mapema jana na leo karudi kuungana na timu tayari kwa ajili ya mchezo wa Ligi dhidi ya Singida Fountaine Gate kesho.


Beki huyo ambaye ni panga pangua kikosi cha kwanza cha Coastal Union ameisaidia timu yake kuwa kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 25 na kufanikiwa kukusanya pointi 34.