Simba yatoa masharti mazito kwa Kibu, Mwamyeto

Muktasari:

  • Ambakishe Kibu pale Simba ili wamnunue Nondo kwa pesa nzuri au amuachie Kibu aende Yanga na wao Simba wamnunue Nondo kwa pesa ya chini.

LAZIMA yafanyike maamuzi magumu. Simba wamemwambia wakala wa mastaa wawili Bakari Nondo Mwamnyeto na Kibu Denis achague moja au akose yote.

Ambakishe Kibu pale Simba ili wamnunue Nondo kwa pesa nzuri au amuachie Kibu aende Yanga na wao Simba wamnunue Nondo kwa pesa ya chini.

Sasa hapo ndipo wakala huyo wa wachezaji hao, Carlos Slyvester alipobaki akikuna kidevu.

Iko hivi; mabosi wa Simba watakuwa na kikao leo na wakala wa wachezaji hao baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam kwa ajili ya kujadili dili la Mwamnyeto kutua Msimbazi lakini pia kwa sharti  la kumbakisha Kibu anayewinda na watani zao Yanga.

Hivi karibuni Mwanaspoti liliripoti kuwa Kibu yupo kwenye rada za kuwindwa na Yanga na mambo yakienda vizuri atasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo msimu ujao lakini Simba wanakomaa abaki ingawa presha zimekuwa nyingi kutoka ndani nan je ya klabu.

Viongozi wanadai kwamba kuna presha za makusudi za kuwatumia mpaka watu wa ndani ya klabu kutaka mkwanja na thamani ya Kibu iongezwe kiaina.

Picha limeanza upya baada ya Simba kuonyesha kutokubaliana na Kibu kwenda Yanga, hivyo imempa mtihani mzito wakala wa wachezaji hao kuhakikisha wote wawili wanacheza Msimbazi msimu ujao, ingawa Yanga nao wanaona kama kuna udalali wa kisirisiri kutaka kuipandisha thamani na dau la usajili mpya wa Mwamnyeto ingawa wanajipa kiburi kwamba haendi kokote.

Simba wanapambana kuhakikisha Kibu licha ya kwamba hana namba za kuvutia uwanjani, lakini anasalia Msimbazi kwani kwa mastraika wazawa bado anaonekana lulu na wakimuuzia adui ni hatari kubwa.

Alipotafutwa wakala huyo, alisema ni kweli amepokea ofa kutoka Simba na Yanga, wanaendelea kuzifanyia kazi, timu ambayo itafikia maslahi basi itafanikisha saini ya mteja wake ingawa lolote linaweza kutokea.

“Kwa pande zote mbili Simba na Yanga mazungumzo yapo na yanaendelea vizuri pia sio ofa hizo tu, zipo nyingine kutoka nje ya Tanzania lakini hatuwezi kuweka wazi kwa sasa,” alisema na kuongeza;

“Kwa timu zote mbili bado makubaliano hayajafikiwa mambo yakienda sawa moja kati ya timu hizo kilakitu kitawekwa wazi mtafahamu kwani mchezo wanaocheza wachezaji ni wa wazi,” alisema Carlos.

Kibu ambaye msimu huu anamiliki bao moja kwenye mechi za Ligi Kuu ni kati ya wachezaji wanaoonekana wana bei kubwa sokoni, akielekea kumaliza mkataba mwishoni mwa 2023/24.

Kati ya timu zilizoingia vitani kuhitaji saini yake ni Yanga inayotajwa kupeleka ofa ya Sh300 milioni, Ihefu FC  yenyewe katika ofa yake iko tayari kutoa kiasi cha Sh500 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu lakini kwa awamu huku waajiri wake wakiweka mezani Sh 300 lakini wakitoa kwa awamu.

Wakati Simba wakitoa sharti hilo kwa wakala wa Mwamnyeto yeye Kibu anaonekana hataki kusalia kabisa kikosini, sababu zikitajwa kuchukizwa na kuchukuliwa kama mchezaji wa kawaida wakati amekuwa akipambana kwaajili ya timu.

Imeelezwa beki Mwamnyeto naye hataki kusalia Yanga, baada ya kuona uongozi wa timu hiyo hautaki kumpa thamani yake wakati ameisaidia timu hiyo kunyakua mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa nahodha.

Jina la Mwamnyeto kuhusishwa na Simba sio kitu kigeni Agosti Mosi, 2020 Yanga iliwapiga bao watani wao kwa kumsaini mchezaji huyo kwa mkataba wa miaka miwili.

Hivyo hivyo kwa upande wa Kibu kwa mara ya kwanza anajiunga Simba msimu wa 2021/22 na akaifungia timu hiyo mabao manane na kutoa pasi tatu zilizozaa mabao.