Yanga kwenda Zenji kufuata makali ya Wastana

KIKOSI cha Yanga,  kinatarajiwa kusafiri keshokutwa Jumatano mchana kuelekea Zanzibar ambako wataweka kambi ya siku mbili  kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers.
Yanga inatarajia kucheza mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers, Agosti 10 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga,  Dismas Ten amesema timu yao itasafiri Jumatano  mchana kuelekea Zanzibar ambako watacheza michezo miwili ya kirafiki kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam,  Ijumaa.
Ten  amesema wakiwa visiwani humo,  wataanza kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Mlandege FC siku ya  Jumatano kisha watacheza na Malindi,  Alhamisi.
"Tunaamini mwalimu ataendelea kukijenga kikosi chetu ili tufanye vizuri,  Jumamosi, tunachoomba Wazanzibar  waipokee timu yao,  nilivutiwa na vile ambavyo mashabiki wa Yanga walijitokeza taifa, " amesema.
Ten amesema viingilio kwenye mchezo wa Jumamosi ni 5,000 kwa mzunguko huku VIP ikiwa 15,000 na lile eneo maalum  zaidi ikiwa 50, 000.
"Yanga imerudi kwenye zama zake hivyo ni jukumu letu kujitokeza kwa wingi   Jumamosi ili kuisapoti, kipindi kile tuliteleza hivyo hatutegemei kurudia makosa ya awamu ile," amesema.
Yanga wanakumbukumbu ya kuondolewa mwaka jana  na Township Rollers wakiwa chini ya George Lwandamina aliyetimkia ZESCO United,   kwa jumla ya mabao 2-1.
Matokeo hayo yalipatika kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa, Machi 6  jijini Dar es Salaam walipoenda Botswana walitoka suluhu,  Machi 17 ndani ya mwaka huo.