Yanga: Lazima mtu apasuke

HAKUNA namna yoyote inayoweza kuwabeba Yanga kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC) leo dhidi ya Kagera Sugar zaidi ya ushindi. Wakipoteza mechi hiyo ya robo-fainali ni kama wamemaliza msimu kwani hawatakuwa na nafasi nyingine ya kushiriki kimataifa kwavile Simba wameshabeba Kombe la Ligi Kuu Bara juzi Jijini Mbeya.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema kwamba; “Ni mechi muhimu kwetu na lazima tufanye kitu, ushindi na kwenda kwenye nusu fainali ni muhimu sana na tunaelewa ugumu wa Kagera hasa rekodi ya mechi zetu mbili zilizopita na dhidi yao Kagera.”

Eymael amesisitiza kwamba kwa aina ya usajili mpya wanaofanya kwasasa ni lazima wapate nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kwani ni ndoto ya mastaa hao na hakuna namna zaidi ya ushindi wa leo dhidi ya Kagera.

Yanga itaingia katika mchezo huo utakaoanza saa 1:00 usiku ikiwa na madeni mawili ambayo moja ni kupata ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa na kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Na pili ni hamu ya kulipa kisasi dhidi ya Kagera Sugar ambayo iliwachapa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu walipokutana Januari 15 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

Timu hizo mbili zinaingia uwanjani zikiwa zimetoka kupata matokeo yanayowiana ambapo Yanga imevuna pointi nne katika mechi zake mbili zilizopita kama ilivyo kwa Kagera Sugar.

Ikijivunia ufanisi na ubora wa hali ya juu wa kiungo wake Deus Kaseke ambaye hivi sasa amekuwa moto wa kuotea mbali, Yanga inapaswa kumchunga zaidi nyota wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu ambaye amekuwa mwiba kwa nyavu za timu pinzani pindi anapokuwa uwanjani.

Mhilu kwa sasa ndiye anashika nafasi ya pili kwa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu akiwa na mabao 13.

Mecky Maxime, Kocha wa Kagera, ameiambia Mwanaspoti kwamba anaelewa kila kitu kuhusu mechi hiyo wao wataenda uwanjani kufanya kazi yao na watacheza soka lao muhimu ikiwa ni ushindi na kusonga mbele kwani wana mpango mzito na Kombe la FA baada ya kukosa ubingwa wa Ligi.

Kocha huyo mzawa amekuwa akihusishwa na kujiunga na Yanga msimu ujao kama msaidizi wa Luc Eymael na mara kadhaa amekiri kuwepo kwa mchakato huo.

Leo pia Namungo itaivaa Alliance mjini Lindi.