Wananchiii... ewaaa!

Friday October 23 2020
yanga 2 pic

GUU la staa wa Yanga, Mukoko Tonombe dakika ya 70 lilizua sekeseke iliyoipa ushindi timu hiyo na mashabiki wakapumua; “Ewaaa..” Kabla ya kuanza kushangilia wakitaja jina la ‘ Ticha..ticha..ticha.”

Hiyo ni mechi ya kwanza ya kocha mpya wa Yanga, Cedrick Kaze ambaye kwa kiasi kikubwa alibadilisha sura ya kikosi hicho tofauti na kilivyozoeleka tangu kuanza kwa msimu huu.

Kwenye kikosi cha kwanza cha jana, Kaze aliwapa nafasi kwa mara ya kwanza Farid Mussa, Haruna Niyonzima na akamuweka nje Michael Sarpong huku akimuanzisha straika Mburkina Fasso, Yacouba Sogne.

Yanga ilionekana kucheza soka la kuchangamka, mipango na kuvutia zaidi ya mechi zilizopita tangu kuanza kwa msimu huu. Kaze alimkosa staa Muangola Carlos Carlinhos aliye majeruhi lakini umiliki wa mpira kwenye mechi ya jana uliwakosha mashabiki ambao walikuwa wakisifia mpaka kwenye mitandao ya kijamii huku wakitamba kwamba Kaze akipewa muda Yanga itanoga.

Yanga walikuwa wakishangilia kwa kutaja neno Ticha wakimaanisha jina la utani walilompachika Tonombe ambaye kila akishangilia huwa anawakalisha mastaa wenzie chini na kufanya kama anawafundisha kitu kwa sekunde kadhaa ingawa jana walishangilia wakiwa wamesimama huku wakidansi.

Yanga walilazimika kusubiri dakika 70 kupata bao hilo, ambapo Shomari Kibwana alimrushia Farid naye akamsogezea Mukoko ndani ya boksi, kisha kiungo huyo akafumua shuti lililombabatiza beki wa Polisi na kutumbukiza nyavuni. Beki huyo aliurukia ili kuuzuia ukamgonga mguuni na kutumbukia kwenye paa la nyavu na kuwapa Yanga bao pekee la ushindi.

Advertisement

Kipa Manyika Peter Jr akabaki akiduwaa bila kujua cha kufanya kwani mpira ulimpita kwa kasi usoni. Awali alidhani ni mpira wa chini.

Kipindi cha kwanza Yanga walionekana kutawala mchezo huku wakikosa umakini kwenye umaliziaji na kumfanya Kaze asimame mara nyingi kutoa maelekezo ya mbinu mbadala za kutumia nafasi.

Dakika ya 23 Fei Toto alipata nafasi nyingine ya kupiga shuti kali lakini kizuizi alikuwa Manyika tena akipangua kwa ustadi shuti hilo.

Mpaka mapumziko hakuna timu ambayo ilifanikiwa kupata bao lolote huku vikosi vyote vikionekana kushindana kutawala mchezo na kutumia akili za ziada kupenya ukuta wa mpinzani.

Kipindi cha pili Yanga waliendelea kutawala mchezo lakini shida ilibaki bado kwenye kutupia nyavuni. Polisi walilazimika kufanya mabadiliko ya kwanza dakika ya 56 wakimtoa Juma nafasi yake ikichukuliwa na Hamad Kimbangwa wakati Yanga nao dakika tatu baadae wakimtoa kiungo Niyonzima nafasi yake ikichukuliwa na mshambuliaji Ditram Nchimbi.

Dakika ya 60 Marcel Kaheza almanusura aipatie Yanga bao mpira wake wa kona ukamshinda kipa wa Yanga Metacha Mnata na kutoka nje kidogo.

Dakika ya 63 Yanga walifanya mabadiliko mengine wakimtoa mshambuliaji Yacouba Sogne nafasi yake ikichukuliwa na Mghana Michael Sarpong aliyejiunga na Yanga akitokea Rayon ya Rwanda.

Dakika ya 68 Sarpong alifanya kazi nzuri ya kuwatoka mabeki wa Polisi lakini pasi yake ilikuwa ndefu kwa Farid ambaye Kaze anaukubali uzoefu wake alioupata nchini Hispania akichezea kikosi cha vijana cha Teneriffe.

Kocha Kaze alisema alitaka wachezaji wake wacheze pasi za haraka haraka, lakini jambo hilo linahitaji muda hivyo anatarajia timu itakuwa bora zaidi.

Metacha, Shomari, Yassin, Lamine, Mwamnyeto, Mukoko, Kisinda, Fei Toto, Yacouba/Sarpong, Niyonzima /Nchimbi, Farid/Mauya.

 

Advertisement