Wameuwasha moto wiki ya kwanza EPL

Wednesday August 14 2019

 

By Fadhili Athumani

WIKENDI hii ilikuwa ni wikendi ya burudani fulu mziki. Moto wa Ligi Kuu ya England (EPL), uliwashwa balaa. Katika wikendi hii ya kwanza ya EPL, ulimwengu wa soka ulishuhudia hat-trick ya kwanza ya msimu, jumla ya mabao 27 yakitikisa nyavu na mechi mbili tu zikimalizika kwa sare. Palichimbika!

Ni washindi wa pili wa msimu uliopita, Liverpool ndio waliofungua msimu wa 2019/2020 kwa staili hii ya kuweka heshima mjini walipoitandika Norwich City 4-1 pale Anfield siku ya Ijumaa.

Kuona hivyo, mabingwa watetezi Manchester City wakajibu mapigo kwa kuikandamiza West Ham mbele ya macho ya mashabiki na wake zao. Vijana wa Pep Guardiola wasiokuwa na huruma walishinda 5-0. Tottenham Hotspurs wakapiga shoo ya kibabe wakitoka nyuma na kuiliza Aston Villa 3-1.

Nalo gharika kubwa likamshukia ‘Super Frank’ Frank Lampard pale Old Trafford kwa kichapo cha mbwa mwizi cha mabao 4-0.

Hakuna aliyemtegemea Ole Gunnar Solsjaer angemkaribisha Lampard kwenye ulimwengu wa EPL kikatili hivyo. Chelsea hawakuwa na uwezo kabisa mbele ya Mashetani Wekundu. Nilikwambia Arsenal nao walishinda?

Wakiwa pale St. James Park, Washika Bunduki

Advertisement

walifyatua risasi moja tu iliyoizamisha Newcastle United. Hebu tuwacheki wanaume watano waliouwasha moto kwenye wikendi hii ya kwanza.

5. ERIK PIETERS

Erik Pieters alipiga shughuli ya kiutu uzima katika mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya Burnley alipotoa asisti mbili kwa Ashley Barnes katika ushindi wa 3-0 walioupata dhidi ya Southampton.

Beki huyu wa kushoto wa Uholanzi alianza mechi hii akiwa na asisti saba tu za EPL katika kapu lake alizozifanya akiwa Stoke City hii ikimaanisha kuwa Pieters (29), amekuja kivingine msimu huu.

Si hivyo tu, kazi kubwa aliyoifanya kwenye safu ya ulinzi iliwahakikishia Clarets ushindi wa asilimia 100 na kuwaacha mashabiki wakiimba jina lake pale Turf Moor.

4. HARRY MAGUIRE

Kama uliamini hata kwa sekunde moja kuwa United walikosea kumnunua beki huyu wa zamani wa Leicester City na kumfanya beki ghali zaidi duniani, ulimkosea heshima sana!

Ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa EPL katikati ya beki ya Mashetani Wekundu ndani ya Old Trafford akiwa na jezi nyekundu dhidi ya klabu kubwa kama Chelsea, alituma salamu.

Shughuli aliyoipiga Maguire (26) ilitosha kuikumbusha dunia kuwa huko sokoni hakamatiki bila ya Pauni 90 milioni. Achana na mabao 4-0 waliyopata, kazi kubwa aliyoifanya ndio iliyoamua matokeo. Muingereza huyu alijenga ngome imara ya ulinzi akishirikiana na beki wa kushoto Aaron Wan-Bissaka na mikono salama ya David De Gea iliyowazuia watoto wa Frank Lampard waliokuwa wanashambulia kama nyuki hasa kipindi cha kwanza.

Takwimu zinaonyesha kuwa, katika mchezo huo uliopigwa siku ya Jumapili, Maguire alizuia mipira saba ya hatari akisimama katika njia ya washambuliaji wa Chelsea mara nne na kuzuia mipira ya vichwa mara tano.

3. HARRY KANE

Kipindi cha kwanza hakuonekana kabisa. Harry Kane alipotezwa vibaya na mabeki wa Villa lakini Tottenham Hotspurs walipomkumbusha kuwa wanamhitaji zaidi, hakuwaangusha.

Vijana wa Mauricio Pochettino walijikuta wakipigwa bao la haraka katika dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza mfungaji akiwa John McGinn aliyetupia goli lake la kwanza EPL.

Usajili mpya wa Spurs, Tanguy Ndombele akajibu mapigo kwa bao la kusawazisha. Harry Kane akaiweka Spurs kifua mbele katika dakika ya 86, kabla ya kupachika bao lake la 127 kwenye EPL dakika nne baadaye.

2. MOHAMED SALAH

Liverpool waliteleza kiulaini mbele ya Norwich City katika mechi ya ufunguzi wa EPL iliyopigwa siku ya Ijumaa usiku. Kilikuwa ni kipigo cha kutangaza Ubabe. Vijana wa Jurgen Klopp walishinda 4-1 - mabao yote yakipatikana kipindi cha kwanza - kazi kubwa ikifanywa na ‘mfalme’ Mohamed Salah.

Mshambuliaji huyo alikuwa mwiba

mchungu kwa mabeki wa Norwich akifunga bao moja katika dakika ya 19 na kufanya ubao usomeke 2-0, baada ya bao la kujifunga la Grant Hamley, kabla ya kuchangia lingine.

1. RAHEEM STERLING

Manchester City walitumia sauti kuu kutuma salamu. Waliwakumbusha watu kuwa wao ndio mabingwa wa soka pale England walipoikandamiza West Ham kwa mabao 5-0 pale London Stadium.

Shoo nzima ya jeshi la bluu bahari la Pep Guardiola iliongozwa na miguu ya Muingereza Raheem Sterling. Hakuna aliyeamini kilichowapata wagonga nyundo wa London. Siku ya pili ya msimu, watu wameanza kuhesabu hat-trick.

Rekodi haikumsaliti. Ni kwamba, kwa mabao yake matatu, Sterling anakuwa mchezaji wa nane na wa kwanza tangu Didier Drogba afanye hivyo mwaka 2010 alipofunga hat-trick katika wikendi ya kwanza ya msimu wa EPL.

Nadhani kwa sauti moja tutakubaliana kuwa winga huyu alikuwa mchezaji bora wa wikiendi ya kwanza ya EPL msimu wa 2019/2020.

Advertisement