Wachambuzi, makocha waichambua Yanga mpya

HUKO Yanga ni kicheko na matumaini ya kuona madini kutoka kwa mastaa wao wa kigeni, baada ya kuupiga mwingi kwenye mechi ya kilele cha Wiki ya Mwananchi. Kilele cha wiki hiyo inayofanyika kila mwaka kilikuwa kwenye Uwanja wa Mkapa, ambapo Yanga ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Aigle Noir ya Burundi.

Mabao ya winga mpya Tuisila Kisinda a.k.a TK Master na Michael Sarpong, yalitosha kuwafanya mashabiki wa Yanga kutoka uwanjani hapo huku mioyo yao ikiwa na furaha na kuhitimisha kilele cha maadhimisho hayo kwa shangwe.

Yanga ilipata bao la kwanza katika dakika ya 38 kupitia kwa Tuisila, ambaye alimchambua kipa wa Aigle Noir kufuatia pasi safi ya Fei Toto.

Mpira ulianzia kwa Deus Kaseke kisha ukatua kwa Fei Toto na kusukuma pasi muarua kwa kiungo mpya Mukoko Tonombe kisha Fei, ambaye aliona kuna uwazi katikati ya mabeki wa kati wa Noir na kupenyeza pasi ambayo iliyomfanya kipa Mtanzania Erick Johola kutoka golini na Kisinda kufunga kwa kumchambua.

Kabla ya kufunga bao hilo, Kisinda hakuonyesha kama yupo mchezoni na alikimbia kwa kasi na kumuacha beki wa kulia wa timu hiyo ya na kufunga kiufundi.

Yanga ilipata bao la pili kupitia kwa Sarpong kwa kichwa maridadi kutokana na pasi safi ya Ditram Nchimbi aliyemzidi mbio Osman Ndikumana wa Aigle Noir.

Kabla ya kupiga asisti hiyo, Nchimbi alipokea pasi ya Kibwana Shomari baada ya kuwa kwenye kasi na eneo zuri la kumimina krosi. Lakini, gumzo kubwa kwa sasa ni mashabiki wa Yanga kutambia aina ya mabao ambayo chama lao liliyapata kwenye mchezo huo, yakionekana kuwa ya kiufundi hivyo, kuwatambia watani zao wa jadi, Simba.

Hata hivyo, Mwanaspoti limezungunza na wachambuzi na makocha wazoefu wa soka ambao, wamekichambua kikosi cha Yanga hasa Tuisila, Mukoko na Sarpong na kufunguka haya.

Mchambuzi mahiri wa soka nchini, Alex Kashasha a.k.a Mwalimu Kashasha, alianza kwa kuwapongeza timu ya kusaka wachezaji wenye ubora wa Yanga (Skauti) kwamba, wamefanya kazi yao inavyostahili.

Alisema wachezaji karibu wote waliosajiliwa na kucheza mchezo huo wa kirafiki, wameonyesha kuwa na ubora na kukata kiu ya mashabiki.

Kashasha, ambaye pia ni mchambuzi wa Gazeti la Mwanaspoti, alisema usajili mpya wa Yanga umekidhi matatizo mengi yaliyokuwa yakiitesa msimu uliopita eneo kwenye eneo la ushambuliaji.

“Ukimtazama mtu kama Tuisila (Kisinda) kutokana na staili yake ya uchezaji, ana uwezo wa kumiliki mpira, anajua muda wa kutoa pasi kwa mwenzake, lakini hata kwenye kufunga ni mzuri na kama lile bao la juzi amefunga kwenye eneo ambalo wengi wanashindwa.

“Idara ya ushambuliaji Yanga ilikuwa butu na iliwapa shida, lakini uwezo wa wachezaji wapya umesaidia na bila shaka watakapokaa na kocha kwa siku hizi chache itakuwa na muunganiko mzuri,” alisema Kashasha.

Pia, alisema kuwa ili kufahamu mchezaji mzuri ni lazima utazame anavyomudu mpira kila anapoupata, kuziba nafasi tupu zilizokuwa mbele yake kwa maana mpira wa sasa ni nafasi na muda ndio vitu vinavyotazamwa na wachezaji wengi waliosajiliwa kwa kuonekana kuwa na sifa.

Kashasha aliongeza kuwa: “ Yanga imepata watu ambao wana thamani ya kuitwa wachezaji wa kulipwa kutokana na kila mmoja kuwa na vitu vya kipekee hata wachezaji wazawa waliosajiliwa walionyesha uwezo mzuri.

Hata hivyo Kocha, Kennedy Mwaisabula anaamini wapenzi wa Yanga watakuwa wamepata mzuka na usajili uliofanywa sio kwa kuangalia matokea bali namna wachezaji walivyocheza kwa muungano kama wamekuwa pamoja muda mrefu. “Tuisila kwangu ndio mchezaji bora kwenye mchezo ule, alikuwa msumbufu anatembea na mpira hiyo ni hazina kubwa ndani ya Yanga kwa sasa,” alisema.

Kuhusu Sarpong alisema ni mchezaji mpambanaji, ambaye hakati tamaa mapema na usajili huo utawafanya kumsahau Benard Morisson kwa haraka zaidi.

Naye straika wa zamani wa klabu hiyo Edbily Lunyamila aliliambia Mwanaspoti kuwa, kikosi hicho kimeonyesha uwezo mkubwa licha ya kuwa na muda mfupi wa kukaa pamoja.

“Kwanza bado hawajaanza kuchanganya kwa maana ya kombinesheni, lakini wameonyesha uwezo mkubwa. Hii ndio Yanga ambayo mashabiki wanataka kuiona uwanjani.

“Usajili wa sasa umedhihirisha ni kitu gani kinahitajika na hata wachezaji wameonyesha huko walikokuwa walikuwa wanafanya nini.

Angalia yule Tuisila na Mukoko waliotoka AS Vita, jamaa wanajua mpira hivyo wanakupa taswira ni namna gani Yanga mpya itakavyokuwa uwanjani,” alisema Lunyamila ambaye alicheza Yanga kwa mafanikio na kuweka rekodi zake kibao tu.

Kwa upande wa Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema kwa sasa kazi imebaki kwa kocha na benchi la ufundi kutengeneza muunganiko.

“Kila kocha ana mifumo yake, kazi itakuwa hapo tu ni namna gani ya kuwatumia ili kupata ambacho tumeanza kukiona kwenye Wiki ya Mwananchi. “Vijana wanaonekana kabisa wana vitu adimu kwenye miguu yao, lakini ndio mwanzo tu tusubiri.”

Kocha wa zamani wa Toto Africans, ambaye ni shabiki lialia wa Yanga, John Tegete alisema kikosi cha Yanga ni kizuri na chenye ushindani lakini, akawaomba waamuzi kuwa makini na kuchezesha kwa kufuata sheria za soka.

“Lakini, niseme tu kuwa heshima ya Yanga imeanza kurudi. Ukiangalia wachezaji wote wazawa na wale wa kigeni utaona wana sifa nzuri za kiufundi,” alisema Tegete.