Karia: Mchezaji bila kupimwa moyo hakuna kucheza Ligi

Muktasari:
- Karia ameyasema hayo baada ya TFF pamoja na Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (TMSA) kuingia makubaliano rasmi na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuanzisha na kusimamia kwa pamoja Programu ya Moyo kwa wanamichezo.
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema msimu wa 2025/26 hakuna mchezaji ambaye atasajiliwa bila ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo kwa wachezaji wote wa Ligi Kuu na Ligi ya Championship.
Karia ameyasema hayo baada ya TFF pamoja na Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (TMSA) kuingia makubaliano rasmi na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuanzisha na kusimamia kwa pamoja Programu ya Moyo kwa wanamichezo.
Karia amesema wamejifunza kutoka mataifa mbalimbali kama Italia, Ujerumani na Qatar, ambayo yamepata bahati ya kuwatembea na kujionea jinsi walivyowekeza katika sports cardiology buildings na mifumo yao ya uchunguzi wa afya za wanamichezo.
“Hii ni sehemu ya sera za kimataifa za ulinzi wa maisha ya wachezaji. Sisi kama TFF, hatuwezi kubaki nyuma na tunajiunga na vyama vyote vya mpira duniani katika utekelezaji wa sera hii na kuanzisha sera mpya kua kilamwanamichezo kabla ya kujiunga na michezo lazima achunguzwe afya ya moyo na kuendelea kuchunguzwa kwa vipindi tofauti hii ni kwa ngazi zote hadi mashuleni,” amesema Karia na kuongeza;
“Tunafahamu kuwa bila programu hii, changamoto tunazopata ni nyingi kama kutojua hali ya afya za wachezaji wetu, kupoteza vipaji kwa vifo visivyotarajiwa,
kupunguza morali ya jamii kuwekeza katikamichezo na hata kuathiri sifa ya nchi kimataifa pale mchezaji anapopoteza maisha kwenye uwanjawa kimataifa.”
Alisema kuanzishwa kwa Jengo la Sports Cardiology ni ndoto inayotimia katika zama mpya za michezo Tanzania na ni hatua ya kihistoria.
“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa, kwa maono yake, na kwa kuweka afya ya wanamichezo kama kipaumbele ambapo amekua akitoa mchango wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na kujumuika na wanamichezo wetu uwanjani na kutoa motisha mbali mbali pale timu zinaposhinda natumai ataunga mkono harakati hizi za nchi yetu katika kujiandaa na michuano hii mikubwa ya kimataifa ya CHAN yanayoanza Agosti na AFCON 2027,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema mpango huu wa Kardiolojia ya Michezo haujalenga tu wachezaji wakubwa wa kitaifa wanapanua huduma hizo hadi kwa wachezaji wa shule, vyuo, vijana wa akademi, wanajeshi, timu za mitaani, na wanamichezo wote wa ngazi mbalimbali kama mbio, netiboli, kuogelea na michezo mingine.
“Tunaanzisha mfumo thabiti wa ufuatiliaji wa afya ya moyo kwa muda mrefu, tukiunganisha teknolojia ya kisasa na wataalamu bingwa wa moyo pamoja na kushirikiana na chama cha madaktari wenzetu wa michezo ambao wamekuwa wakifanya kazi hii kwa umahiri na kwa muda mrefu katika sekta hii,” amesema Dk Kisenge na kuongeza;
“Tuna furaha pia kutangaza kuanzishwa kwa ujenzi wa jengo la kwanza la kihistoria nchini la Kardiolojia ya Michezo au sports cardiology Tanzania kua unaaanza rasmi.
Jengo hili litatumika kama kitovu cha huduma, mafunzo na tafiti za masuala ya moyo kwa wanamichezo.